April 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kuvunjwa kwa Jiji la Dar giza nene latanda

Muonekano wa jiji la Dar es Salaam

Spread the love

 

RAIS John Magufuli, ametangaza kuivunja halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, kuanzia Jumatano iliyopita, tarehe 24 Februari mwaka huu.

Amesema, hatua yake ya kulivunja jiji hilo, imetokana na kile ambacho yeye amekiita, “jiji la Dar es Salaam, kutokuwa na wawakilishi wanaochaguliwa na wananchi moja kwa moja.”

Badala yake, Rais Magufuli amesema, ameipandisha hadhi iliyokuwa halmashauri ya Manispaa ya Ilala, kuwa jiji la Dar es Salaam.

Sisi tunaona uamuzi huu wa Rais Magufuli, umesheheni kasoro tatu kubwa – mbili za kisheria na moja, ni ya kiutawala.

Kwamba, kifungu cha 7 cha sheria za serikali za mitaa (Local Government), kinamtaka waziri wa Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kutoa notisi ya siku 60 kwenye gazeti la serikali – Government Gazette (GN) – kueleza dhamira yake ya kulivunja jiji.

Lengo hapa, ni kuwezesha wananchi kutoa maoni yao na kuufanya mchakato huo kuwa shirikishi. Wanaruhusiwa hata kuweka pingamizi kwa wale ambao hawakubaliani na uamuzi huo.

Hili sidhani kama limefanyika. Wananchi wa Dar es Salaam ambao walikuwa na mawazo tofauti na yale ya rais; na au wanaliokuwa wanakubaliana naye, hawakuwahi kusikilizwa.

Aidha, maamuzi haya yalipaswa kwenda bungeni kupata baraka za Bunge. Hii ni kwa sababu, Ibara 145 (1) na (2) na 146 (1) na (2) zinaeleza, kutakuwapo vyombo vya serikali za mitaa katika kila mkoa, wilaya, mji na kijiji, ambayo vitakuwa vya aina na majina yatakayowekwa na sheria iliyotungwa na Bunge au Baraza la Wawakilishi.

Bunge au Baraza la Wawakilishi, litatunga sheria itakayofafanua utaratibu wa kuanzisha vyombo vya Serikali za Mitaa; miundo na wajumbe wake, njia za mapato na utaratibu wa utekelezaji wa shughuli za vyombo hivyo.

Madhumuni ya kuwapo Serikali ya Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi. Vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki kuwashirikisha wananchi katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa jumla.

Vilevile, hata uamuzi wa rais wa kuipandisha hadhi, iliyokuwa halmashauri ya Manispaa ya Ilala, ili kuwa jiji la Dar es Salaam, nao haukuwa shirikishi.

Baraza la madiwani la manispaa ya Ilala, wala kamati za maendeleo za kata katika halmashauri hiyo, hazikuwahi kujadili jambo hili.

Kingine ambacho bado kinaweza kuleta shida, ni kuichukua halmashauri ya Manispaa ya Ilala yote kama ilivyo, kuigeuza kuwa ndio jiji la Dar es Salaam.

Ofisi za Jiji la Dar es Salaam

Baadhi ya maeneo ya iliyokuwa Manispaa ya Ilala ambayo sasa yanatambulika kama jiji la Dar es Salaam, hayana hadhi ya kuingia kwenye jiji.

Mathalani, maeneo kama Buyuni, Majohe, Kimanga, Pugu, Kitunda, Ukonga, Segerea, Gongolamboto na Chanika, yaliyopo katika majimbo ya Ukonga na Segerea, yanakuwa sehemu ya jiji la Dar es Salaam.

Lakini maeneo kama Kigogo, Mikocheni, Magomeni, Msasani, Masaki, Ubalozi wa Marekani, Ubalozi wa Kenya, Mwananyamala, Manzese na Kinondoni, kuanzia daraja la Salenda, hayako katika mamlaka ya jiji la Dar es Salaam.

Njia pekee ya kuondoa manung’uniko kwa hapa ambako serikali imefika, ni kuunda halmashauri mpya ya Manispaa ya Ilala, ambayo itawezesha kuziingiza kata zote zilizopo pembezoni na kuliacha jiji na kata zake zilizopo mjini.

Kwamba, halmashauri ya Manispaa ya Ilala, itakuwa na majimbo matatu ya uchaguzi – kama ilivyo sasa, ambayo ni Segerea, Ukonga na Ilala.

Halmashauri mpya ya manispaa ya Ilala, itabaki kuwa na mkuu wa wilaya mmoja, lakini kutakuwapo na wakurugenzi wawili; mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam na mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.

Kata ambazo zitabaki kuwa halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, ni pamoja na Jangwani, Kariakoo, Mchikichini, Kisutu, Gerezani, Kivukoni, Ilala, Upanga Mashariki, Mchafukoge na Upanga Magharibi.

Suala la kuzivunja halmashauri zote tano za jiji la Dar es Salaam na kuunda halmashauri moja, haliwezi tena kutekelezeka katika mazingira ambayo maamuzi haya yameshafanyika.

Shida kubwa ya jiji kwa jinsi muudo wake ulivyokuwa, ni kutokuwa na eneo lake la utawala. Pale Karimjee ambako ndiko kwenye ofisi za meya, ni ardhi ya manispaa ya Ilala.

Kwamba, maeneo ambayo yalikuwa yanatambulika kama sehemu ya halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, ni ambako sehemu yote ya iliyokuwa halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, kabla ya kuvunja na kuundwa Tume ya Jiji la Dar es Salaam, ni maeneo yanayomilikiwa na manispaa nyingine za Ilala, Konondoni, Temeke, Kigamboni na Ubungo.

error: Content is protected !!