August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kutoweka Ben Saanane bado kitendawili

Bernard Saanane, Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

SIKU 25 sasa zimepita tangu kijana Bernard Saanane ambaye ni Katibu wa Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (UTG), atoweke katika mazingira ya kutatanisha huku ndugu, jamaa na marafiki zake wakimsaka bila mafanikio, anaandika Charles William.

Ben ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema Taifa anadaiwa kuonekana kwa mara ya mwisho tarehe 18 Novemba mwaka huu, tangu hapo hapatikani kupitia mawasiliano ya simu yake na hata mitandao ya kijamii, jambo ambalo limezua hofu kwa familia na watu wake wa karibu kiasi cha kuripoti jambo hilo katika kituo cha polisi Tabata.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Malisa Godlisten, Mwenyekiti wa UTG – taasisi ambayo pia Ben ni kiongozi wake amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na ndugu wa Ben wamemtafuta kijana huyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo hospitalini, vituo vya polisi na magereza lakini wameshindwa kumpata.

“Baada ya kutomuona kwa muda mrefu hatimaye tarehe 05 Desemba, 2016 tulitoa taarifa makao makuu ya Jeshi la Polisi pamoja na kituo cha polisi cha Tabata ambapo tulipewa RB Na. TBT/RB/8150/2016 huku pia tukipewa ruhusa ya kumtafuta maeneo mbalimbali.

Tulimtafuta katika hospitali ya Amana, Temeke, Mwananyamala na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, tukikagua vyumba vya wagonjwa mahututi, orodha ya wagonjwa wasiotambulika waliolazwa na katika vyumba vya kuhifadhia maiti lakini hatukumpata,” ameeleza Malisa.

Ameongeza kuwa baada ya hatua hizo waliamua kumtafuta Ben katika vituo vya polisi wakiamini kuwa huenda akawa anashikiliwa, ambapo walikagua katika vituo vikubwa vya polisi vyote vya Dar ikiwemo Oysterbay, Mabatini, Urafiki, Magomeni, Buguruni, Chang’ombe na Sitakishari hata hivyo hawakuweza kumpata na ndipo walipomtafuta katika magereza na Ukonga na Segerea ambako pia walimkosa.

“Baada ya sintofahamu hiyo, tulienda Ofisi za uhamiaji katika uwanja wa ndege jijini Dar kujua kama Ben amesafiri nje ya nchi au la, baada ya kuhakiki taarifa wakatujulisha kuwa rekodi zinaonesha hajasafiri katika kipindi cha Novemba wala Desemba 2016, ndipo tukaenda Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) ili tupate taarifa za mawasiliano yake ya mwisho ambazo zingetusaidia kupata mwanga wa mahali alipo.

TCRA wakatueleza jukumu hilo ni kpuni ya simu kupitia Jeshi la Polisi waaopaswa kuandika barua kuomba mawasiliano ya Ben. Tulifika polisi 7 Desemba 2016 na kuandika maelezo upya ambao waliahidi kuandika barua hiyo kwenye mtandao husika wa simu ili kupata mawasiliano yake, hata hivyo mpaka sasa hatujapata mawasiliano hayo kwa madai kuwa kampuni husika ya simu haijawasilisha taarifa hiyo Polisi,” amesema.

Katika hatua nyingine Malisa ameshangazwa na namna viongozi wa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vilinavyolipa uzito mdogo suala la kupotea kwa Ben Saanane na kupatikana kwa maiti saba za watu katika mto Ruvu, mkoani Pwani.

“Tarehe 08 Desemba, 2016 iliokotwa miili ya watu kijiji cha Mtoni, wilaya ya Bagamoyo, kutokana na kupotea kwa Ben tulisafiri hadi huko tukakuta maiti hizo zimeshazikwa tena bila hata ya kuacha vielelezo kama nguo za marehemu wala vipimo vyao vya vinasaba (DNA) ili kutoa nafasi kwa watu waliopotelewa na ndugu zao kwenda kuhakiki. 09 Desemba iliokotwa maiti nyingine ambayo tulifanikiwa kuikagua na kujiridhisha kuwa siyo ya Ben Saanane,” amesema.

Malisa amesema licha ya miili hiyo kuokotwa katika mto Ruvu lakini hakuna Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mbunge wala Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi aliyefika katika eneo la tukio jambo linalosikitisha na kuzua taswira hasi.

“Inastaajabisha watu saba wamepoteza uhai katika mazingira ya kutatanisha lakini serikali haijachukua hatua yoyote. Ikimbukwe ni serikali hii ambayo mawaziri wake watatu walitoa matamko ndani ya siku moja baada ya mwanafunzi mmoja wa Sekondari ya Mbeya kuadhibiwa kikatili na walimu wa mafunzo kwa vitendo.

Inashangaza pia kuona watumishi wa umma, wakuubwa serikali akiwemo Waziri Mkuu na mawaziri wengine wakihaha usiku na mchana kutoa matamko na kufuatilia suala la kupotea kwa Faru aitwaye John lakini vifo vya watanzania wenzetu saba havijapewa uzito. Faru John hawezi kuwa na thamani kubwa kuliko maisha ya watanzania saba,” amesisitiza.

Malisa akiwa ameambatana viongozi wengine wa UTG akiwemo Bob Chacha Wangwe ambaye ni makamu mwenyekiti, Noel Shao, Naibu Katibu Mkuu na wengineo amevitaka vyombo vya usalama vitoe mawasiliano ya Ben kama yalivyoombwa huku pia wakikitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho Ben alikuwa muajiriwa wake kitoe taarifa na kuchukua hatua za kina juu ya kupotea kwa mtumishi huyo.

“Hatujaridhishwa na namna Chadema inavyochukua hatua katika suala hili, Ben amekuwa mtumishi wa chama hicho kwa muda mrefu, hatuoni kama ni sahihi chama hicho kutotoa tamko lolote hadi leo ikiwa ni siku 24 tangu apotee,” amesema.

error: Content is protected !!