Sunday , 19 May 2024
Makala & Uchambuzi

Kushika dola si kazi

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
Spread the love

VYAMA vingi vya siasa vimejaa ubinafsi, tamaa ya madaraka na kutaka kushinda uchaguzi ili kutawala. Ajenda hiyo ni rahisi mno. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Ni sawa na ule usemi usemao kubeba mimba si kazi kazi ni kulea mtoto. Kushika dola si kazi, kazi ni kutawala na kukidhi maslahi ya wananchi wanyonge.

Viongozi wa vyama hujirudisha wenyewe nyuma, moja ya ufafanuzi wa chama kushika hatamu uliowahi kutolewa na Muasisi wa CCM, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wake alisema kuwa, serikali ni chombo chenye maguvu ambayo yanataka kudhibitiwa.

Ndio maana vyama vya siasa vinashindana ili kinachoshinda vishike hatamu za kuongoza yale maguvu ya kutii maagizo ya viongozi.

Lakini neno hatamu ni ile kamba inayomwongoza farasi kwani mbali na maguvu yote aliyonayo farasi lakini ukishashika ile hatamu basi itamuongoza unavyotaka atatii.

Ukitaka akimbie atakimbia, ukitaka akate kona atakata. Hii ndiyo maana ya chama kushika hatamu za uongozi.

Hivyo viongozi wa vyama vya siasa wana wajibu mkubwa wa kuiambia serikali na kuikosoa ili itende kile kinachotakiwa na wananchi.

Vyama vingi vilivyoogopa kufanya mabadiliko ndani ya chama vimeng’oka kirahisi madarakani hivyo ni funzo kwa vyama vingine vya siasa vinavyotaka kushika dola.

Lazima vyama vyao viwe na muundo na mfumo imara utakaokifanya kuimarisha chama kwani chama legelege huzaa serikali legelege.

Vyama vinapopata misukosuko mikubwa kulingana na tawala na ili kubaki imara, vinapaswa kubadili mbinu na si kupiga yowe.

Jambo kubwa katika maendeleo ya nchi ni kuendeleza demokrasia yenyewe na sio muundo unaoiendesha demokrasia.

Baadhi ya vyama vya siasa vinashindwa kutumia demokrasia katika kuchuana kugombea uongozi hata vijana au wanawake ndani ya vyama hivyo kutokana na uimla na ubabe.

Ningependa kuungana na mawazo ya Mwalimu Nyerere kwa kusisitiza msingi wa chama cha siasa chochote iwe CCM ama vyama pinzani dhidi yake ni kuendelea kukubalika kwa wananchi ili viaminiwe kuongoza nchi.

Hivyo kinapaswa kuwa na masharti ambayo yatimizwe na wanachama na viongozi wa ngazi mbalimbali na kila mara vijichunguze vyenyewe kwa umakini kama vinafuata.

Vyama vya siasa vinapopata matokeo mabaya au mazuri, viketi chini na kujichunguza na uchunguzi wenyewe lazima uanze kwenye shabaha zake.

Uchunguzi huo ufuatiwe na wapi wamefaulu na wapi waliposhindwa na mwisho lazima chama kijiunde upya pale ambapo ni lazima ili kuendelea kutekeleza shabaha zake kwa ufanisi zaidi. Kuhamasisha vurugu au kupuuza wananchi wa kawaida ni hatari.

Baadhi ya vyama vya siasa vina tabia ya kutoa manung’uniko na sababu zenye majibu ya visingizio badala ya kufanya tathmini za kisayansi za kushindwa au kufaulu.

Viongozi hutumia muda mwingi kuwa wapiga debe na kulalamika tu. Lazima vyama vya siasa muda wote vitambue shabaha zao na kuzidi kuzisambaza kwa wanachama wao ili nao wazielewe na hatimaye kuweka mikakati ya utekelezaji.

Vyama vya siasa nchini vinakabiliwa na mgawanyiko mkubwa kutokana na tabaka la kiuchumi na kijamii. Tofauti ya masikini na matajiri kuwepo miongoni mwa wanachama ndani ya vyama vya siasa kunachangia kuwagawa wanachama wa vyama hivi.

Kama watu wachache wanaishi maisha ya kifahari na walio wengi hawapati mahitaji yao ya lazima wataanza kuhaha kutafuta mahema mapya.

Vyama vijifunze taabu iliyowapata CCM kwamba yalikuwa matokeo ya kuwambatia matajiri na kuruhusu wanachama wake wajipatie mali hata nje ya sharia.

Kuruhusu matajiri kutumia fedha zao ovyo ndiyo inayozaa tabia ya kuendelea kupatikana kwa viongozi mbalimbali kwa misingi ya rushwa. Utaratibu huu ni sumbu mbaya ndani ya chama.

Ieleweke tatizo la rushwa linalokabiliwa kwa sasa ni matokeo ya mfumo ndani ya CCM na serikali zake. Hivyo mabadiliko ya mfumo mpya kudhibiti rushwa uwe pia kwa vyama vingine vya siasa.

Chama cha siasa ni chombo kinachowaunganisha watu kwa hiyari zao watu wenye itikadi moja na shabaha moja.

Hivyo kila chama, kinahitaji kila baada ya kipindi kifupi kuchambua shabaha zake. Kwani tuna vyama vingi huku kila chama hudai kinaitakia mema nchi lakini mema yote hayawezi kutekelezwa kwa pamoja na kwa wakati mmoja. Ni wajibu yaliyopangwa kutekelezwa wanachama wote wajue.

Kila chama cha siasa kilichosajiliwa kisiwe kama klabu ya mpira, viongozi wake wakubali hakuna bwana mwingine zaidi ya wanachama wake.

Kuna dhana iliyojengwa na vyama vya siasa umma uamini kuwa unapokifadhili chama fedha na magari unaweza kuwaweka viongozi wa juu wa chama mfukoni.

Vyama vya siasa vyote lazima viwe na mikakati imara ya kujitegemea kifedha ili kisifungwe minyororo na matajiri. Vikao vya juu hadi vya chini vya vyama vitumike kujenga hali bainifu kulingana na mabadiliko mapya.

Mazoea ya kujitathmini kila baada ya kipindi au shughuli kubwa ya kidemokrasia ni utaratibu wa kujiimarisha ili kubaini upungufu. Vyama vyote vya siasa hapa nchini vina watu wengi ambao huingia kwenye vyama kwa matumaini ya kupata vyeo na fedha kwa faida zao.

Kundi hili lina mchango mkubwa wa kudhoofisha demokrasia na kuvidhoofisha vyama kila wanapokosa kutimiza malengo yao. Tayari wapo waliohama kwa kushindwa kufikia malengo ya madaraka.

Ukomavu wa viongozi kutambua kuwa wameshindwa kumshauri kiongozi aliyewateua na kujiuzulu ni utamaduni ambao hajazoeleka, lakini unaufanya umma kutambua kuwa cheo ni dhamana.

Kitendo hiki ni tunu kubwa katika kujenga demokrasia. Wanachama na viongozi wasiotumia uhuru huo kuogopa kuchukiwa au kupoteza nafasi zao ni ubinafsi ambao ni adui wa haki na ukweli.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Makala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Potofu huzaa potoshi/ potoshi huzaa potofu?

Spread the loveDayosisi 7 za KKKT katika kanda ya Ziwa na Magharibi,...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the loveTAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mpina mwiba CCM, ahofia kuzibwa mdomo

Spread the loveWAKATI Chama cha Mapinduzi (CCM), kikijinasibu kuwa kinara wa demokrasia...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mabeyo ametuepusha

Spread the loveNIMEGUSWA na uadilifu, utiifu na uaminifu wa Mkuu mstaafu wa...

error: Content is protected !!