July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kura za maoni: Vigogo CUF waanguka

Mtangazaji mkongwe wa BBC, Ally Saleh ‘Alberto’ mmoja wa aliojitokeza kuwania nafasi ya uwakilishi kupitia CUF

Spread the love

MAWAZIRI wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMS), kutoka Chama cha Wananchi (CUF); wabunge wengine kadhaa wakongwe wa chama hicho na baadhi ya wawakilishi, wameangukia pua katika kura za maoni za kutafuta wagombea wa nafasi za uwakilishi na ubunge kwa majimbo 50 ya Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Miongoni mwa mawaziri waliopigwa mweleka, ni Haji Faki Shaali, aliyekuwa waziri asiyekuwa na wizara maalumu; Haji Mwadini Makame, aliyekuwa naibu waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati.

Faki Shaali ameangushwa kwenye kura za maoni katika jimbo la Mkanyageni, sambamba na mbunge wa jimbo hilo, Mohamed Habib Mnyaa. Naye Mwadini ameangushwa katika nafasi ya uwakilishi katika jimbo la Nungwi.

Hata hivyo, mkurugenzi wa uchaguzi wa chama hicho, Omary Ali Shehe amesema, matokeo hayo ni ya hatua za awali; Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (NEC), linaweza kurejesha walioshindwa kura za maoni, kutegemeana na litakavyoona inafaa.

Kura hizo zimewatupa nje waandishi wa habari mbalimbali waliokuwa wamejitokeza kuwania nafasi za ubunge na uwakilishi, akiwamo mtangazaji mkongwe wa BBC, Ally Saleh ‘Alberto.’

Ally Salehe aliyekuwa anawania ubunge katika jimbo la Mji Mkongwe, Unguja, ameangushwa na mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Ibrahim Mohamed Sanya.

Wengine waliongushwa, ni Talib Ussi Hamad wa Mwananchi aliyepata kura 31 katika nafasi ya ubunge Jimbo la Magogoni. Mshindi katika jimbo hilo, ni Juma Kombo Hamad aliyepata kura 106 huku mbunge anayemaliza muda wake Kombo Khamis Kombo akiambulia kura 61.

Mwandishi wa Majira, Mwajuma Juma alishika nafasi ya pili, baada ya kupata kura 11 akiwania nafasi ya uwakilishi jimbo la Amani, ambapo Khamis Rashid Abeid aliibuka kidedea kwa kura 22. Mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Maua Mohamed Mussa alishika mkia katika nafasi aliyokuwa akiwania ya ubunge wa viti maalumu, kupitia wilaya ya Mjini.

Mbunge wa Jimbo la Mkanyageni, Injinia Mohamed Habibu Mnyaa
Mbunge wa Jimbo la Mkanyageni, Injinia Mohamed Habibu Mnyaa

Mtangazaji wa zamani wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), Najma Khalfan Juma alipata pigo mara mbili baada ya kuanguka katika kura za maoni nafasi ya uwakilishi jimbo la Ziwani na nafasi ya ubunge viti maalumu kupitia Wilaya ya Chakechake, Pemba.

Kwa upande wa uwakilishi wa viti maalumu Wilaya ya Mjini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej amepenya kwenye tundu la sindano kwa ushindi wa kura moja, baada ya kupata kura 91, akifuatiwa na Nunuu Salim Rashid aliyepata kura 90 na mtoto wa mbunge wa Mji Mkongwe, Rahma Ibrahim Sanya aliyepata kura 30 huku kura nne zikiharibika.

Mbunge wa Mtambile, Mohamed Abdallah Salim naye ameanguka katika kura za maoni sambamba na mwakilishi anayemaliza muda wake, Mohamed Haji Khalid huku Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), Dk Alley Soud Nassor akijitoa kabla ya uchaguzi na nafasi hiyo ya uwakilishi kunyakuliwa na Abdallah Bakar Hassan.

Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi wa CUF kutoka Jimbo la Chonga, Abdallah Juma Abdallah ameanguka katika kura hizo pamoja na mbunge wa jimbo hilo, Haroub Mohamed Khamis huku Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC), Omar Ali Shehe akishinda kwa kura tisa baada ya kumwangusha Mhasibu wa Kampuni ya simu ya Zantel, Ali Bakari aliyepata kura 97.

Kwa upande wa ubunge Jimbo la Chakechake, Yusuph Kaiza Makame ameibuka kidedea kwa kura 84 baada ya kumuangusha Fatma Omar Juma aliyepata kura 83, huku Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Juma Duni Haji akishinda kwa kupigiwa kura za ndiyo baada ya mpinzani wake Ali Juma Khamis kujitoa dakika za mwisho na kupata kura 60 kati ya 61 katika nafasi ya uwakilishi jimbo la Bububu.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui amepita katika kura za maoni nafasi ya uwakilishi jimbo la Mtoni, lakini mbunge, Faki Haji Makame ameanguka.

Katika Jimbo la Mtambwe, Mbunge wake, Khalifa Mohamed Issa ameangushwa katika kura za maoni pamoja na Mwakilishi wake Salim Abdallah Hamad huku Mbunge wa Ole Rajab Mbarouk Mohamed naye akianguka lakini Mwakilishi wa jimbo hilo, Hamad Masoud akiibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza.

Mbunge wa Micheweni, Rashid Ali Abdallah pamoja na Mwakilishi wake, Subeti Khamis Faki wamefanikiwa kuzitetea nafasi zao na kuibuka washindi katika kura za maoni, wakati mbunge wa Konde Khatib Said Haji akiibuka na ushindi, upande wa Mwakilishi, Suleiman Hamad Khamis aliangushwa.

Mwakilishi wa Jimbo la Wete, Asaa Othman Hamad naye ameangushwa katika kura za maoni, wakati Mbunge, Mwadini Abbas Jecha akitetea nafasi yake, huku Waziri wa Katiba na Sheria Abubakar Khamis Bakari akishinda kwa hekaheka nafasi ya uwakilishi lakini Mbunge wa jimbo hilo, Kombo Khamis Kombo akianguka kwenye kura za maoni kwa kura 61 na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Kombo Hamad aliyepata 106.

Wagombea uwakilishi, Ismail Jussa Ladhu na Mansour Yusuph Himid walipitishwa wakiwa ni wagombea pekee katika majimbo ya Mji Mkongwe na Kiembesamaki, mtawalia, huku kamishna wa zamani wa Bodi ya Mapato Zanzibar, Mohamed Hashim Ismail naye akiibuka na ushindi wa nafasi ya uwakilishi Jimbo la Dimani huku Khalid Said Suleiman ‘Gwiji’ akishinda katika nafasi ya ubunge wa jimbo hilo.

Waziri wa zamani wa Utalii na Maliasili katika Serikali ya awamu ya Pili, Juma Hamad Omar alipita kuwania ubunge wa Jimbo la Wawi kuziba nafasi ya Hamad Rashid Mohamed huku Mwakilishi wa jimbo hilo Saleh Nassor Juma akianguka kwenye nafasi hiyo.

error: Content is protected !!