RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli, amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaosimamia mchakato wa kura za maoni, kutafuta wagombea wa chama hicho nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi kuwa wawazi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam …(endelea).
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo Jumatatu tarehe 20 Julai 2020, katika hafla ya uapisho wa viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni iliyofanyikia Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Soma zaidi:
Mchakato wa kura za maoni kwa chama hicho unafanyika kwa siku mbili leo na kesho Jumanne.
Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, amesema wanachama 10,367 wa CCM wametia nia kugombea ubunge na uwakilishi nchi nzima ambapo waliokamilisha taratibu na kuzirejesha ni 10,321.
“Nilikua napata taarifa leo kwa ajili ya kugombe nafasi mbalimbali katika nchi nzima, walikuwa ni 10,367 na katika hao wamekamilisha taratibu na kurudisha fomu ni 10,321, kwa hiyo hawakurudisha 46 katika nchi nzima,” amesema Rais Magufuli.
Mwenyekiti huyo wa CCM amewataka wasimamizi wa kura za maoni, waendeshe michakato hiyo kwa uwazi bila mizengwe, ili mtia nia anayestahili kupendekezwa kugombea katika uchaguzi huo, apate haki yake.
Rais Magufuli amesema zoezi la kuhesabu kura lifanyike kwa uwazi mbele ya wajumbe, kama ilivyofanyika katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), wa kutuea mgombea Urais wa Tanzania na Zanzibar.
Mkutano wa NEC ulifanyika tarehe 10 Julai 2020 jijini Dodoma, ambapo ulimteua Dk. Hussein Mwinyi, kuwa mgombea Urais wa CCM Zanzibar na Rais Magufuli kuwa mgombea Urais wa Tanzania.
“Matumaini yangu watakaosimamia kura za maoni watasimamia kwa uwazi bila mizengwe yoyote ili kila mwenye haki apate haki yake.”
“Ningetamani viongozi watakaosimamia kwa leo na kesho zikimaliza kupigwa kura, zikafanyike kama ilivyokuwa halmashauri kuu, zihesabiwa hadharani,” amesema Rais Mgufuli.
Rais Magufuli amewapongeza WanaCCM waliotia nia, huku akiwasisitiza wasimamizi wa zoezi hilo, kutenda haki kwa ajili ya kuimarisha umoja wa chama hicho.
Leave a comment