July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Kura ya amani tuepushe machafuko’

Spread the love

KATIBU Mkuu wa Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA), Grace Tendega amesihi wanawake wote nchini kushiriki uchaguzi kwa amani na salama ili kuiepusha nchi kuingia katika machafuko. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Akihutubia umma wa wanawake waliokusanywa na BAWACHA kwa ajili ya kukutana na mgombea urais kupitia chama hicho, Edward Lowassa, Tendega amesema uchaguzi ni amani sio vurugu.

Amesema umuhimu wa wanawake kushiriki uchaguzi kwa amani unakuja hasa kwa sababu ni wao wanawake pamoja na watoto wanaoathirika zaidi pale panapotokea machafuko.

“Tusikubali vurugu kwa sababu sisi wanawake ambao ndio wengi nchini petu, ndio huathirika sana pakitokea machafuko,” amesema katika hotuba ya utangulizi ya kongamano la wanawake kwenye ukumbi wa Millenium Tower, Makumbusho, Dar es Salaam.

Tendega amesema BAWACHA, Chadema na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wanaamini kuwa wapo wanawake wengi Tanzania wanaendelea kuwa masikini kwa sababu tu serikali haijawapatia fursa za kujiendeleza kiuchumi na biashara, upungufu unaopaswa kurekebishwa.

Amesema ni matarajio ya wanawake hasa wale wa makundi yanayoishi katika mazingira magumu, kuwa serikali itakayoundwa na UKAWA, itachukua hatua makini za kuwatoa wanawake katika shida zinazowakabili.

Aliwataja Mama Lishe, madada poa, wauza matunda na wengineo ambao wengi wazo ndio wasimamizi wa familia zilizotelekezwa na wanaume kwa sababu mbalimbali zikiwemo za wanaume kukosa kazi baada ya sera ya ubinafsishaji iliyotekelezwa na Serikali ya CCM chini ya Benjamin Mkapa.

Kongamano hilo ambalo Mwenyekiti wa BAWACHA, Halima Mdee na mke wa Lowassa, Mama Regina, walikuwepo, lilitarajiwa kuhutubiwa na Lowassa ambaye alipoingia ukumbini alishangiliwa kwa wimbo “CCM sio chama Lowassa asingehama.”

error: Content is protected !!