July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kuokota chupa humuingizia Sh. 300,000 kwa mwezi

Chupa za plastiki

Spread the love

UWEPO wa Dampo la Murieti lililopo kata ya Terati, mkoani Arusha, umekuwa neema kwa wakazi wanaoishi kuzunguka dampo hilo kutokana na kunufaika kwa kufanya biashara ya kuuza chupa aina ya plastiki, glasi zilizotumika na mifuko.

Biashara ya chupa za plastiki ambazo hutumika kwa maji, soda na vimiminika vya aina tofauti imezidi kushamiri na kushika nafasi hasa katika miaka ya hivi karibuni.

Chupa hizo ambazo hutupwa kama taka huokotwa na kuuzwa tena. Masoko makubwa ya chupa hizo ni Dar es Salaam na nchi jirani kama Kenya ambako huzipokea kama malighafi viwandani na kuyeyusha ili kutumiwa tena.

Biashara hii imesaidia kuweka mazingira safi na kuyatunza. Pia imepunguza idadi ya taka ngumu hasa zile zinazotokana na plastiki ama glasi.

Kutokana na ukosefu wa ajira nchini, ukusanyaji wa taka hizi umekua ni fursa ya watu kujiajiri kwa kuzikusanya kwa wingi, ili kujipatia fedha.

Wako watu wanaoendesha maisha yao, kusomesha watoto kwa kupitia kazi ya ukusanyaji wa chupa hizi.

Dampo la Murriet ni eneo maarufu jijini Arusha hasa ukizingatia limepakana na eneo la Morombo ambalo ni maarufu pia, linapatikana mita kadhaa kutoka hapo.

Baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na dampo hilo wanatumia nafasi hiyo kujikusanyia lundo la chupa hizo tayari kwa kuziuza.

Biashara hii imesaidia kupunguza ugumu wa maisha hasa kwa wenye hali ya chini ukizingatia kuwa watu hao hulipwa kutokana na kiwango walichokusanya.

Mkusanyaji na muuzaji, Maria Michael, anasema biashara hiyo imemsaidia kuihudumia familia yake ya watoto watatu na pia kujipatia mahitaji yake muhimu.

“Nikikusanya kwa bidii mwisho wa mwezi napata karibu sh 200,000 hadi 300,000. Kwa wastani kuna siku nyingine unaweza kupata 10,000 kwa siku hadi 30,000 kulingana na ukusanyaji.

Maria anasema wamekuwa wakiuza chupa hizo kwa kilo, chupa za plastiki kilo sh 400, chupa za glasi kilo 50 huuzwa kwa sh 1,500 wamekua wakiwauzia watu wanaosafiri nje ya mkoa.

James Laizer, mfanyabiashara anayekwenda katika dampo hilo na kununua mifuko ya plastiki marufu kama salfeti anasema hununua mifuko minne kwa sh 100 na kwamba baada ya hapo anaisafirisha katika migodi ya machimbo ya Merereni ambapo huyatumia kuchotea udongo wa chini ya ardhi na kuupandisha juu.

Akieleza faida alizowahi kuzipata tangu ameanza biashara hiyo kwa muda wa miaka miwili sasa, anasema inamsaidia kulipa ada za watoto wane ambao husoma shule za sekondari.

“Pesa ninayoipata imenisaidia kumalizia nyumba yangu ambayo ilikua bado haijakamilika, kwa sasa nimeikamilisha.

‘Nina watoto wanne. Watatu wako sekondari na mmoja yuko shule ya msingi, wote hawa namudu kuwasomesha kutokana na fedha ninazozipata hapa,” anasema.

Ofisa Usafi na Mazingira Halmashauri ya Jiji la Arusha, James Lobikoki, amesema wanatambua uwepo wa watu hao wanaokusanya chupa hizo na wanasaidia kupunguza taka ngumu katika dampo hilo la kisasa ambalo limegharimu sh. bilioni 3.

Lobikoki anasema wana mpango wa kuwasajili watu hao na kutengeneza utaratibu muhimu ikiwemo kuhakikisha wana vifaa vya kujikinga na madhara.

“Uchambuzi wa taka za plastiki kuziweka mahali kuwatafutia soko nyingine zinaenda Nairobi kulikua na tatizo la kuzuiwa mpakani, lakini tuliwandikia barua wakakubali kuzipokea kama malighafi na si taka.

“Tunawashauri wadau waanzishe viwanda vya kuyeyusha chupa hizo na kutengeneza bidhaa zinazotokana na plastiki kama sahani, vikombe, vyombo mbalimbali badala ya chupa hizo kusafirishwa kama malighafi mikoani ama nje ya nchi,”anasema Lobikoki.

Waswahili wanasema “kazi ni kazi, ilimradi ni halali na mkono unaenda kinywani.”

Mwandishi wa habari hii ni Juma Said

error: Content is protected !!