HATUA ya 16 ya michuano ya Euro imemalizika jana, kwa kigogo mwengine wa soka barani humo, timu ya Taifa ya Ujerumani kutupwa nje mara baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0, kutoka kwa Uingereza. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Kichapo hicho cha Ujerumani, kilikamilisha idadi ya timu kwenye kundi F, kuondolewa kwenye michuano hiyo, licha ya kuwa kundi gumu ‘Kundi la Kifo’ na kuwepo kwa matumaini mengi ya kuwa bingwa angetoka humo.
Kundi hilo lilikuwa na timu za Ureno ambao ni mabingwa watetezi, Timu ya Taifa ya Ufaransa ambao ni mabingwa wa kombe la Dunia, Ujerman pamoja na Hungary.
Katika kundi hilo zilipita timu tatu, kwenye hatua ya 16 bora, ambazo ni Ureno, Ufaransa ambao walikuwa vinara pamoja na Ujerumani iliyoshika nafasi ya pili.
Kwenye michezo hiyo ya hatua ya 16 bora, Ureno ilicheza dhidi ya Ubeligiji na kuondoshwa kwenye michuano hiyo mara baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0, Ufaransa nao wakakubali kipigo kwa njia ya penati 5-4, dhidi ya Uswizi, mara baada ya kufungana mabao 3-3, kwenye dakika 90.
Ujerumani ilikuwa wa mwisho kwenye kundi hili kuaga mashindano siku ya jana, kwa kukubali kichapo cha mabao 2-0, kutoka kwa Uingereza, mabao yaliyofungwa na Raheem Sterling pamoja na Harry Kane.
Michuano hiyo itaendelea Ijumaa na juma mosi kwa hatua ya robo fainali ambapo Hispania itashuka dimbani dhidi ya Uswizi, Ubeligiji dhidi ya Italy, Jamhuri ya Czech wataminyana na Denmark, na Ukrain watavaana na timu ya Taifa ya Uingereza.
Leave a comment