July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kundi jipya la kigaidi latesa Ouagadougou

Spread the love

HATUA ya kundi jipla la kigaidi la Al Mourabitoune kushambulia na kuua watu 29 kwenye hoteli ya Splendid huku wengine wakijeruhiwa vibaya katika mji wa Ouagadougou, Burkina Faso Ijumaa iliyopita, limekemewa vikali.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani kundi hilo kutokana na kutekeleza mauaji ya watu wasio na hatia huku wengine wakiwa kwenye hali mbaya.

Kundi hilo limetoa taarifa na kukiri kutekeleza mashambulizi hayo. Al Mourabitoune limeeleza kwamba lina uhusiano na kundi la Al-Qaeda.

Kutokana na shambulizi hilo, wajumbe wa baraza hilo wametuma salamu za rambirambi kwa serikali ya familia za waathirika.

Taarifa hiyo ya mkono wa pole pia imeelekezwa kwenye nchi ambazo raia wake wamekuwa wakilengwa mara kwa mara na mashambulizi ya kigaidi.

Wajumbe wa baraza hilo wameelezea mshikamano wao na Serikali ya Burkina Faso na nchi zingine kwenye ukanda mzima katika vita dhidi ya ugaidi na kusisitiza kwamba, kuna haja ya kuongeza juhudi za kikanda na kimataifa kukabiliana na vikundi hivyo.

Baraza la Usalama limesisitiza kwamba ugaidi katika mifumo yote ni moja ya vitisho vikubwa zaidi kwa amani na usalama wa kimataifa.

Pia wamesisitiza haja ya kuwafikisha wahusika wa ukatili huo katika mkono wa sharia, wakisema wote waliohusika na mauaji ni lazima wawajibishwe na kuyataka mataifa yote kutimiza wajibu wao chini ya sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama kwa kutoa ushirikiano ipasavyo katika suala hili.

error: Content is protected !!