November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kumtetea mkandarasi kwamponza Waziri, JPM amtolea uvivu

Spread the love

RAIS John Magufuli amemchimba mkwara Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele kwamba atamfukuza kazi endapo mkandarasi wa ujenzi wa daraja la Mto Sibiti lililoko mpakani mwa mkoa wa Singida na Simiyu, kampuni ya China Henan International Corporation haitamaliza ujenzi huo kwa wakati. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa daraja la mto Sibiti na barabara unganishi ya mkoa wa Singida na Simiyu, leo tarehe 10 Septemba, 2018, Rais Magufuli ameonyesha kutoridhishwa na maelezo ya Waziri Kamwele kuhusu utendaji kazi wa mkandarasi huyo.

“Waziri Isack Kamwele naomba mjipange, nimeshangaa ulipoanza kuongea mambo ya mkandarasi nikajiuliza na wewe umeanza kula hela, tutafukuzana hapahapa. Maroli mawili ndiyo yatajaza vifusi hapa, contractor (mkandarasi) gani huyu, yaani ametoka China na maroli mawili tu, mkiona hafai mfukuzeni,” amesema Rais Magufuli na kuongeza:

“Waziri, Katibu Mkuu, TANROAD, ninataka daraja hili likamilike, nimekuja kuweka jiwe la msingi nataka nikipita tena nipite juu ya daraja. Mkiona hafai fukuzeni, muache kuchezea fedha za watu.”

Aidha, amemtaka mkandarasi kuacha kutoa sababu kuhusu uchelewaji wa mradi huo kwa kuwa wananchi hawataki kusikia sababu, bali wanataka ujenzi wa daraja hilo ukamilike.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesema ujenzi wa daraja la mto Sibiti ulioanza tangu mwaka 2013 utakuwa wa kwanza kuufuatilia, na kuagiza kuwa, ifikapo mwezi Machi mwaka 2019 ujenzi wa mradi huo umeshakamilika.

“Mkandarasi huu ujenzi ni namba moja kuufuatilia, nitakuwa napiga simu mara kwa mara kujua utekelezwaji wake. Nataka mwezi wa tatu mwaka kesho huu ujen zi ukamilike,” amesema.

error: Content is protected !!