April 11, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kukoroma kunaweza kusababisha kifo

Enos Madebere, Daktari wa Kliniki ya Usingizi katika taasisi ya CCBRT (kulia) akifafanua kuhusu ugonjwa wa kukoroma.

Spread the love

WATU wengi wanaona tatizo la kukoroma usingizini, ni jambo la kawaida, lakini linapokomaa, madhara yake ni makubwa. Anaandika Hamis Mguta…(endelea).

Dk. Elisha Madebere, Daktari wa Kliniki ya Usingizi kutoka Taasisi ya CCBRT, katika mahojiano maalum na mtandao huu amesema, ugonjwa huu ni hatari kwasababu unaweza kusababisha kifo.

Anasema, ni ugonjwa unaotokana na ufinyu wa njia ya kupumua na kuwa, mtu anapokuwa amelala, kwenye njia ya kupitisha punzi kutoka kwenye pua kufika mapafu (Trachea), hutokea pingamizi ambalo hubana njia ya hewa na kusababisha misuli ya njia hiyo kuwa ngumu katika kupitisha hewa.

“Mtu anapokuwa hayupo usingizini, sehemu nyingi za mwili anakuwa anazidhibiti yeye mwenyewe yaani akisema kwamba akohoe, anakohoa.

“Lakini mtu anapokuwa amelala, sehemu nyingi za mwili inaongozwa na mwili wenyewe na anakuwa hajitambui, hivyo anapokuwa amelala pingamizi la kupumua linatokea, ndipo inatokea hali ya kukoroma,” anasema na kuongeza;

“Hii inakuwa ni upungufu wa njia ya hewa au njia hiyo inakuwa imeziba kabisa, na hali hii huwa inaenda sambamba na mtu kusimama kupumua (Stop in breathing)  kwa muda wa sekunde 10 na kuendelea. Inaweza ikatokea mara kadhaa ndani ya saa moja, matokeo yake inaweza kupelekea kufa ukiwa usingizini.”

Miongoni mwa madhara ya tatizo hili amesema, ni kupata tatizo la kisukari licha ya kuwepo kwa vitu vingine vinavyotajwa kusababisha tatizo hilo, pia inachochea kupata ugonjwa wa kiharusi, moyo na shinikizo la juu la damu.

Dk. Enos ametaja vitu vinavyosababisha ugonjwa wa kukoroma, ambayo ni ulimi mkubwa. Amesema, mara nyingi mtu akilala ama kusinzia, misuli inayoshikilia ulimi sehemu ya nyuma zinakuwa zinadhibitiwa na mfumo wa mwili, hivyo unarudi nyuma na kukandamiza njia ya hewa ambayo humpelekea mtu kupumua kwa kutumia nguvu zaidi na kusababisha kukoroma.

nyingine ni unene, kwamba husababisha kuwepo kwa uvimbe pembezoni mwa njia ya hewa, unaosababishwa na mafuta au sababu nyingine na kupunguza njia ya hewa, hatimaye hupumua kwa nguvu na kupelekea kukoroma.

“Kuna dalili nyingi za kujua kama una tatizo la usingizi pingamizi ambazo ni pamoja na kukoroma, wakati wa usiku unaenda haja ndogo mara kwa mara au kupaliwa wakati ukiwa umelala, kusikia kichwa kinauma kwa mbali baada ya kuamka asubuhi.

“… na wakati mwingine kuhisi usingizi mzito wakati wa mchana kana kwamba ulikesha, hali hii hupelekea hata wakati ukiendesha gari na pale unaposimama kidogo kwenye foleni, unajikuta unalala.

“Wakati mwingine hasa kwa sisi wanaume, unapoteza hata nguvu za kushiriki tendo la ndoa na mwenza wako. Unaweza kuwa naye lakini hamu inapungua,” anasema.

Dk. Enos anasema, matibabu ya ugonjwa huo yanafanywa kulingana na ukubwa wa tatizo, na wakati mwingine humalizika kwa kufanya mazoezi ili kupunguza uzito.

Kwamba, wengine wanapatiwa mashine ya Cpap ambayo huitumia kila anapolala kwa ajili ya kuzuia usingizi pingamizi, wakati mwingine mtu anaposimama kupumua, mashine inaendelea kumuingizi Oxygen ndani ya mwili.

“Watu wenye matatizo kama haya, wanapaswa kufika kliniki hii ya usingizi, tutawafanyia uchunguzi wa awali. Wengine wanakuja tunawafanyia uchunguzi wa mwanzo na tunawapa ushauri wa bure tu,” anasema.

error: Content is protected !!