May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kujifukiza elfu 5 Muhimbili

Spread the love

 

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam (MNH), imefunga mashine nne za kutoa dawa kwa njia ya mvuke ili kusaidia wagonjwa kupata tiba ya mfumo wa upumuaji kwa kutumia dawa zilizoidhinishwa na Serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mashine hizo zilizotengenezwa nchini na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), zimezinduliwa leo Alhamisi tarehe 4 Machi 2021, na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru.

Amesema mashine tatu zimefungwa Upanga na moja Mloganzila ambapo zitaanza kutumika rasmi kesho Ijumaa kwa utaratibu maalumu ambapo wagonjwa watakaoruhusiwa ni wale watakaokubali kwa hiari yao wenyewe na wale wanaoweza kutembea na kusimama wenyewe kwenye mashine kwa muda usiozidi dakika tano.

Profesa Museru amesema, huduma iko wazi kwa wananchi watakaopenda kufika kuitumia atatakiwa kuchangia kiasi cha Sh.5,000.

Amesema hatua hiyo ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukabiliana na magonjwa yanayohusiana na mfumo wa upumuaji.

“Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto ilielekeza kuimarishwa matumizi ya dawa za tiba asili na tiba mbadala kwa wagonjwa walioko hospitalini kama nyongeza kwenye tiba za kibingwa wanazopewa.”

“Katika kutekeleza hilo, hospitali imekuja na utaratibu wa kuwaruhusu wagonjwa kwa hiari yao kutumia dawa za tiba asili za kunywa na mvuke (steam therapy) zilizoidhinishwa na Serikali sambamba na tiba za kibingwa wanazopewa,” amesema Profesa Museru.

Amesema, hatua ya ufungwaji wa mashine hizo, utakwenda sambamba na kutoa fursa kwa wataalamu wa Muhimbili kufanya utafiti kubaini ufanisi wa baadhi ya dawa zinazogunduliwa na baadhi ya wataalamu wa tiba asili nchini ili hatimaye kuja na majawabu.

“Katika hospitali zetu za Upanga na Mloganzila tuna madaktari wa aina mbalimbali takribani 400, baadhi yao kupitia matumizi ya huduma hii ya tiba mvuke, watafanya utafiti na kuwa katika nafasi ya kutuambia kama tiba hizi zinasaidia kwa kiasi gani.”

“Kwa kuwa, ugonjwa huu wa Covid 19 ni mpya hakuna aliye na majibu sahihi, kwa hiyo ni muhimu kwamba hizi njia zinazojitokeza za kupambana na matatizo haya sisi tuliopo hapa tusizipuuzie bali tuzifanyie utafiti na kutoa majibu,” amesema Prof Museru.

Naye Mratibu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala wa Mikoa na Wilaya kutoka Wizara ya Afya, Dk. Vumilia Liggyle amepongeza hatua ya Muhimbili kufunga mashine za kutoa tiba mvuke na ametoa wito kwa hospitali na taasisi nyingine nchini kuiga mfano wa huo ili kuendelea kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.

error: Content is protected !!