Friday , 9 June 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Kubenea uso kwa uso na AG
Habari za SiasaTangulizi

Kubenea uso kwa uso na AG

Spread the love

SAED Kubenea, Mbunge wa Ubungo ameibua sakata la serikali kushtakiwa nje ya nchi kwasababu mbalimbali, ikiwemo kuvunja mikataba ya wawekezaji. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Mbunge huyo ameitaka serikali ieleze kwa kina, mkakati wa kukabiliana na changamoto hiyo.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo tarehe 18 Juni 2019, Kubenea amehoji kwamba, serikali ina mkakati gani kuhakikisha inalipa wadai wake, ikiwemo wakandarasi iliyoingia nayo mikataba ya kimataifa, ili kuondoa mzigo wa madeni na kushtakiwa nje ya nchi?

Aidha, Kubenea ameihoji serikali kwamba, imeokoa kiasi gani cha fedha kufuatia agizo lake la kutotumia wanasheria binafsi katika usimamiaji wa kesi zake?

Pia amesema, baadhi ya mashirika na taasisi za umma zimekiuka agizo hilo, na kuhoji kuwa, serikali ina  kauli gani juu ya taasisi hizo?

“Moja ya malengo ya kuagiza kesi za serikali kusimamiwa na mawakili, ni kupunguza gharama za uendeshaji kesi.  Sasa gharama za kushtakiwa nje imekuwa kubwa, serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inalipa wadai wote na wakandarasi wote, kwenye mikataba ya kimataifa ili kuondoa mzigo wa madeni na kustakiwa nchi za nje?” amehoji Kubenea na kuongeza:

“Serikali ilitangaza kuwa, wanasheria wote waliomo katika mashirika ya umma, watafanya kazi chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupunguza gharama ya uendeshaji kesi, je utekelezaji wa agizo hili umefikia wapi na kiasi gani kimeokolewa tangu serikali iache kutumia mawakili wa nje?”

Akijibu maswali hayo, Dk. Adelardus Kilangi,  Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) amesema, sasa hivi ofisi yake iko makini kwa kuhakikisha kwamba, haiingi katika mikataba mibovu ili kukwepa changamoto ya uvunjaji mikataba inayopelekea serikali kushtakiwa nje ya nchi.

Amesema, serikali imeingia katika majadiliano na mashauriano na baadhi ya wadai wake, ili kumaliza kesi hizo kwa njia ya makubaliano badala ya kwenda katika njia za kimahakama.

“Kesi mbalimbali zilizoko nje zinazotokana na kuvunja mkataba, kwa sasa hivi tuna umakini sana tunapoingia mikataba kiasi kwamba, hatutaingia kwenye kushtakiwa kwa kuvunja mkataba, kwa sasa tunazingatia masilahi ya umma,” amesema Dk. Kilangi na kuongeza:

“Mikataba yetu inatengenezwa vizuri kuhakikisha kwamba, hakutakuwa na matatizo, kwa kiasi kikubwa tumeingia katika majadiliano kuona namna gani tutamaliza kesi hizo kwa njia ya mashauriano na makubaliano badala ya kwenda katika njia za kimahakama.”

Kuhusu baadhi ya mashirika ya umma kuendelea kutumia wanasheria binafsi, Dk. Kilangi amesema, kesi zote husimamiwa na mawakili wa serikali, isipokuwa kuna baadhi ya kesi ofisi yake hutoa kibali maalum za kutumia mawakili binafsi.

“Baadhi ya mashirika kuendelea kutumia mawakili binafsi hii inawezekana.  Wakati wa maelekezo haya ya kesi zote kusimamiwa na mawakili wa serikali yanatolewa,  mashirika yalikuwa yamekubaliana na mawakili binafsi, kwa vyovyote vile kwa sasa hivi wanafanya kazi kwa pamoja na ofisi yangu,” amesema Dk. Kilangi na kuongeza.

“Lilipotolea lile agizo, hakutakuwa na kesi yoyote ambayo itasimamiwa tena na mawakili binafsi isipokuwa na sababu ambazo waziri amezieleza.”

Naye Balozi Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria, amesema serikali kupitia wizara yake imeziagiza taasisi na mashirika ya umma kuwasilisha mashauri yote ya madai dhidi yake, kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa ajili ya kuratibu usimamizi na uendeshaji wake.

Aidha, Balozi Mahiga amesema serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hutoa kibali kwa mashirika ya umma cha kutumia wanasheria binafsi kutokana na sababu mbalimbali hususan katika mashauri yanayofunguliwa nje ya nchi.

Kuhusu fedha zilizookolewa kufuatia utekelezaji wa agizo hilo, Balozi Mahiga amesema katika mwaka wa fedha wa 2018/19 serikali iliokoa kaisi cha Sh. 9.1 Bilioni  ambazo zingelipwa kwa mawakili binafsi.

Hata hivyo, amesema serikali ikishakamilisha zoezi la kuratibu idadi ya mashauri dhidi yake, itapata thamani halisi ya fedha zilizookolewa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaTangulizi

Ngoma bado mbichi mkataba wa Bandari

Spread the love  SAKATA la mkataba wa uendeshaji, uendelezaji na uboreshaji wa...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mkataba unaweza kuvunjwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mikataba ya utekelezaji bado haijasainiwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

Habari za Siasa

Lussu: Mkataba wa DP bandarini si wa miaka 100

Spread the loveMAKAMU Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, amesema hakuna ukweli wowote...

error: Content is protected !!