February 28, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea, Sugu waibana serikali makosa ya mtandao

Spread the love

MBUNGE wa Ubungo Saed Kubenea (Chadema) ameitaka serikali ieleze ni lini itapeleka bungeni muswada wa kuifanyia marekebisho sheria ya makosa ya mtandao kutokana na sheria hiyo kubana uhuru wa mwananchi kupata habari. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Kubenea alitoa kauli hiyo leo bungeni alipokuwa akiuliza swali la msingi kwa kutaka kujua ni lini serikali itafanya marekebisho ya sheria ya makosa ya mtandao kutokana na sheria hiyo kuonekana kuwa inamnyima uhuru mwananchi kukosa habari.

Mbali na hilo kubenea amesema kuwa sheria hiyo pia inaenda kinyume kabisa na katiba ya nchi huku ikiwa inaleta kuwepo na vurugu au kutokuelewana na mataifa mengine kutokana na kuwepo kwa mkanganyiko katika sheria hiyo.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eliasi Kuandikwa amesema kuwa seikali haina mpango wa kupeleka mswada bungeni kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho ya sheria hiyo hadi hapo kutakapokuwepo na uhitaji wa kufanya hivyo.

Naye Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi (Chadema) aliuliza swali la nyongeza Bungeni alitaka serikali ieleze ni lini itaondokana na kutumia sheria mbovu na kuzitumia kwa matakwa ya kisiasa kwa ajili ya kuwaonea wapinzani.

Akiuliza swali la nyongeza Bungeni leo amesema kuwa kuwepo kwa sheria mbovu za makosa ya mtandao ilimpelekea kufungwa gerezani kutokana na yeye pamoja na watu wake kujadili juu ya kuteshwa wa watu, kupigwa, kuuliwa na baadhi ya watu kukutwa wamekufa na kufungwa katika viroba.

“Sheria mbovu za habari zimetungwa kwa ajili ya kuwaonea watu ikiwa ni pamoja na kuwapa shida wanasiasa hasa wa upinzani, kwa mfano mimi nilifungwa kutokana na kuwawepo kwa majadiliano mimi na watu wangu juu ya kuteswa kwa watu, kupotea, kuuliwa na baadhi ya watu kukutwa wamekufa na wamefungwa kwenye viroba.

“Jambo hilo lilikuwa likijadiliwa na watu wengi ukizingatia viongozi wa dini waliweza kuzungumzia mambo hayo lakini kwangu mimi nilifungwa kwa sheria hiyo mbovu sasa nataka kujua ni lini sheria hiyo italekebishwa ili isipingane na katiba ya nchi kama ilivyo kwa sasa,” alihoji Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu.

Hata hivyo Naibu wazri amesema kuwa sheria hiyo ni muhimu katika nchi ya Tanzania na badala ya kuwaathiri wananchi imesaidia kupunguza uhalifu wa mtandao kwani wananchi wameweza kujua na kuelewa faifa na hasara za kutumia mtandao.

error: Content is protected !!