August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea: Mtanufaika nami

Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, akizungumza na wapiga kura wake

Spread the love

SAED Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam amewahakikishia wakazi wa Mtaa wa Mavurunza A, Kata ya Kimara jimboni humo kwamba, kero zao zitatatuliwa, anaandika pendo Omary.

Amesema kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo watapata huduma ya shule ya sekondari, soko, maji na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.

Na kwamba, changamoto nyingine ambazo zitatatuliwa ni kufanikisha huduma ya afya bure kwa wazee na kutengwa kwa eneo la kuzikia.

Kubenea anayeongoza jimbo hilo kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ametoa kauli hiyo jana alipokutana na wananchi kusikiliza kero zinazowakabili.

Kwenye mkutano huo Boniface Jacob, Meya wa Manispaa ya Ubungo alihudhuria.

Johns Mtega, mkazi wa mtaa huo alitaka kujua hatua ambazo zinachukuliwa na serikali katika kuhakikisha Kata ya Kimara inapata huduma ya shule ya sekondari, maji safi na salama na Barabara inayotoka Barabara Kuu ya Morogoro kuingia katika mtaa huo.

Kubenea amesema tayari hatua zimeanza kuchukuliwa “tumekubaliana na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ufanyike ujenzi wa dharura wa shule ya sekondari ndani ya siku 90 ili kuweza kusajili wanafunzi wa awamu ya pili watakaochaguliwa kuendelea na masomo.”

Kubenea amesema “tulifika kwenye eneo la makaburi ambapo tulikuta mgogoro. Wananchi wamejenga kwenye mkaburi hata watu kuzika pembeni kabisa mwa eneo. Nimeiagiza halmashauri, wananchi na mimi mbunge tuchangie ununuzi wa eneo jipya la kuzikia.”

Akizungumzia kuhusu kero ya barabara kubwa inayoingia katika mtaa huo Meya Jacob amesema “hii barabara ipo chini ya Wakara wa Barabara Tanzania (TANROADS).

“Tutawaandikia barua kama wameshindwa kuweka lami sisi Halmashauri ya Ubungo tunazo fedha za kutosha, tutaijenga kwa kiwango cha lami ili kuwaondolea kero wananchi.”

Aidha, Paschal Manota, Diwani wa Kata ya Kimara amewaambia wananchi kuwa, tayari amewaangiza mwenyeviti wa serikali za mitaa kushirikiana na mabalozi na uongozi wa kata kutayarisha majina na vielelezo vya wazee wote katika eneo hilo ili kuvipeleka halmashauri kwa ajili ya kuandaa utaratibu wa matibabu.

“Pia kuhusu kero ya maji, tayari mtambo wa Ruvu umekamilika kwa asilimia 97. Kinachofanyika kwa sasa ni kuhakikisha tunaunganisha bomba na wananchi wanapata maji,” amesema Manota.

error: Content is protected !!