December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea kutumia Sh. 15 mil, kukarabati soko la Manzese  

Spread the love

MBUNGE wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, ameahidi kusaidia kiasi cha Sh. 15 milioni ili kufanyia ukarabati wa soko la kuku lililopo katika kata ya Manzese. Anaripoti Faki Sosi …(endelea).

Alitoa ahadi hiyo jana tarehe 23 Februari 2019, wakati alipofanya ziara ya kutembelea soko hilo ambapo mbunge huyo alisikitishwa na mazingira magumu yanayowakumba wafanyabiashara hao.

“Hapa siyo mahala salama kwa afya za wafanyabiashara wa soko hili na hata kwa watumiaji wa chakula hiki, kutokana na mazingira yake kutokuwa masafi,” alisema Kubenea na kuongeza, “nikiwa mwakilishi wenu, nitasimama nanyi kuboresha eneo hili,” alieleza.

Alisema, “kutokana na hali hii niliyoishuhudia leo, ninawaahidi kuwapa kiasi cha Sh. 15 milioni, zitakazotumika kukarabati soko lenu.” Aliahidi fedha hizo kupatikana ndani ya muda mfupi ujao.

Katika ziara hiyo ambayo ni mfululizo wa ziara za mbunge huyo katika jimbo lake, Kubenea alifika sokoni hapo majira ya saa nane na robo mchana nakupokelewa na viongozi wa soko hilo, wakiongozwa na mwenyekiti wake, Hamis Mgana.

Mwenyekiti huyo alimueleza Kubenea, wafanyabiashara takribani 470 wanaofanya shughuli zao katika soko hilo, wakiwamo wachinjaji 150, wanafanya biashara zao katika mazingira magumu, kutokana na ufinyu wa eneo.

Aidha, Kubenea amesema, amesikitishwa na kutokamilika kwa wakati, ujenzi wa machinjio ya kisasa ya kuku yanayojengwa katika soko hilo na kwamba hakubaliani na matumizi ya karibu Sh. 100 milioni, zinazodaiwa kutumika kwenye ujenzi wa machinjio hayo.

Ujenzi wa machinjio mapya katika soko la Manzese umesimama kufuatia kugundulika kwa ufujaji wa mamilioni ya shilingi zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Kubenea aliwaambia wafanyabiashara hao na watu wengine aliokuwa ameongozana nao kuwa mazingira ambako bidhaa hiyo inaandaliwa, hayaridhishi kwa matumizi ya binadamu.

“Hapa siyo mahala salama kwa afya za watumiaji wa chakula hiki hata kidogo. Ni lazima sisi kama viongozi tuchukue hatua,” alieleza.

Alisema, amesikia kilio chao na kuahidi kukifanyia kazi ndani ya muda mfupi ujao.

Katika ziara hiyo, mbali na kutembelea soko la Manzese, mbunge huyo uwanja wa michezo wa Manzese ambapo watumiaji wake walimuomba kusaidia ukarabati. Alikubali ombi hilo.

Aliwaomba wahusika wamuandikie barua rasmi inayoeleza mchanganuo wa mahitaji yao.

Alikuwa ameongozana na Naibu Meya wa Manispaa ya Ubungo, Ramadhani Kwangaya, ambaye pia ni diwani wa kata hiyo.

Akiwa anatembelea mitaa yote 10 ya Kata ya Manzese, kwa kutembea miguu, kote alikopita Kubenea alipokelewa kwa shangwe na wananchi.

Ameahidi kurudi tena katika kata hiyo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ujao.

error: Content is protected !!