May 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea kumaliza tatizo la takataka Kinondoni

Spread the love

SAED Kubenea, mgombea ubunge Kinondoni kupitia Act-Wazalendo ameahidi kumaliza changomoto ya uchafuzi wa mazingira kwa kuanzisha kiwanda kitachochakata takataka kuwa mbolea. Anaripori Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Kubenea alitoa ahadi hiyo jana Jumatano tarehe 17 Septemba 2020 alipokuwa akimnadi mgombea udiwani wa Tandale, Mohammed Kassim katika Uwanja wa Fisi.

Alisema Kinondoni haitakuwa na msongamano wa takataka na kwamba hizo zitageuka kuwa fursa.

“Takataka zitakuwa fursa, itakuwa mtu anaziuza kwenye viwanda na baadaye zitabadilishwa kuwa mbolea. Kinondoni haitakuwa na takataka,” alisema.

Kubenea alisema, anaijua Kinondoni na kwamba amekuwa kwenye baraza la madiwani wa manspaa ya Kinondoni kwa mwaka mmoja na nusu akiwa Mbunge wa Ubungo kupitia Chadema kati ya mwaka 2015-2020.

Alisema kuwa akiwa kwenye Manspaa hiyo alipigania wananchi wa Kinondoni wasibomolewe makazi yao ndio sababu zoezi hilo lilisitishwa.

Kubenea alisisitiza dhamira yake ya kumaliza athari za mafuriko kwenye jimbo hilo kwa kuwashawishi wadau wa maendeleo kuendelea na mradi kupanua mto msimbazi na mto ng’ombe sambamba na kuweka bustani ya utalii.

Naye Kassim akijinadi kwa wananchi, alisema akifanikiwa kuwa diwani ataupaisha mchezo wa ndondi (boxing).

Kassim alisema eneo la Tandale lina vipaji vingi vya mchezo wa ngumi hivyo atawatengenezea mazingira mazuri ya mchezo huo.

“Najua hapa Tandale kuna vipaji vingi vya mchezo wa ngumi, hata mimi mwenyewe ni mwanamichezo, nitahakikisha wanamichezo wanafahamika nje na ndani ya nchi,” amesema Kassim huku akishangiliwa na wananchi waliojitikeza kwenye mkutano huo.

Kassim alisema akichaguliwa yeye katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 28 Oktoba 2020 atahakikisha Tandale ina maendeleo ya kiuchumi, michezo na miundombinu.

error: Content is protected !!