MGOMBEA ubunge jimbo la Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saed Kubenea ameahidi kuboresha zahanati iliyopo kwenye Kata ya Kimara, Dar es Salaam ili iwe na hadhi ya kituo cha afya, iwapo atachaguliwa kuongoza jimbo hilo. Anaandika Pendo Omary … (endelea).
Kubenea, mwandishi wa habari na Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi Publisher LTD inayochapisha gazeti la MwanaHALISI, ametoa ahadi hiyo leo katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mtaa wa Kilungule uliopo kwenye Kata ya Kimara, jimboni Ubungo.
Amesema “najua mnapata shida katika kupata huduma za afya. Mkinichagua kuwa mbunge wenu, kazi yangu ya kwanza ni kuboresha huduma za afya katika kata hii.
“Nitahakikisha naboresha huduma za afya kwa kuhakikisha zahanati iliyopo inakuwa na uwezo wa kuhudumia kata nzima tofauti na ilivyo sasa ambapo huduma ni mbovu, hakuna umeme wala maji safi,” amesema Kubenea.
Kubenea amesema atahakikisha zahanati hiyo inapata umeme wa uhakika na kuchimba kisima chenye urefu usiopungua mita 60 tofauti na kilichochibwa kwa sasa chenye urefu wa mita 20.
“Kuhusu suala la umeme katika zahanati kwa kuanza nitatoa jenereta ili kuwasaidia wananchi hasa akina mama wanaopata huduma katika zahanati, wakati tukiendelea kufanya juhudi za kuhakikisha tunakuwa na umeme wa uhakika,” amesema Kubenea.
Hata hivyo msafara wa Kubenea kuelekea katika kampeni Jimbo la Ubungo na Kimbamba ulilazimika kutumia usafiri wa bodaboda baada ya barabara ya Morogoro eneo la Kimara Mwisho mtaa wa Matangini kufugwa kutokana na shughuri za kampeni za mgombea ubunge jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Finella Mukangara.
Hali hiyo ilimlazimu Kubenea kutumia muda wa saa moja kuhutubia mikutano miwili badala ya mitatu kama ilivyopangwa awali.
Mimi ni mkazi wa Ubungo, ila niko huku ughaibuni. Ingawa sitaweza kupiga kura, ninafuatlia yanayojiri jimboni kwangu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi. Kati ya wagombea wa ubunge, naweza kusema nafahamu habari za ndugu Saed Kubenea vizuri, ingawa hatujawahi kukutana. Kuhusu ndugu Didas Massaburi, naona kuwa anajulikana kama Dr. Mimi kama mwanataaluma ninayefundisha chuo kikuu nimekuwa nikijaribu kujua ndugu Massaburi alisomea na kuhitimu chuo gani. Hadi sasa sijaweza kupata taarifa. Je, kuna anayejua? Natanguliza shukrani.