August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea azidi kuchanja mbuga, mtaa kwa mtaa

Spread the love

MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), leo ameendelea na ziara yake ya kukagua uhai wa chama chake na kutembelea wananchi wake katika jimbo lake la uchaguzi la Ubungo, anaandika Mwandishi Wetu.

Akiwa katika eneo hilo, Kubenea alikutana na wanachama na viongozi wa tawi la Kisiwani, ambako pamoja na mengine, alihimiza ustawi wa chama na kuondoa makundi miongoni mwa wanachama na viongozi.

“Nimekuja hapa kuwatembelea. Nimekuja kukagua uhai wa chama, kukutana na wanachama na wananchi kwa lengo la kusikiliza kero zao.

“Ninachowaomba tukisaidie chama chetu kuimarika ili kuhakikisha kwenye uchaguzi unaofuata, CCM kinaondoka madarakani kwa nafasi zote,” ameeleza Kubenea.

Amesema, “tumenyanyaswa sana na utawala huu. Hakuna namna ya kufanya zaidi ya kuimarisha chama chetu ili uchaguzi ujao, tuweze kuondokana na utawa huu wa mabavu na ukandamizaji.”

Wakichangia katika mkutano huo, baadhi ya wajumbe wakiwamo viongozi wa Kata ya Mburahati, walimtaka mbunge kuwasimamia ili waweze kuitisha mkutano mkuu wa kata. Kubenea ameridhia pendekezo hilo.

Mara baada ya kumalizika mkutano huo, Mbunge Kubenea aliingia mtaani ambako alikutana na wananchi na kujadiliana nao juu ya matatizo yanayowakabili.

Aidha, Kubenea alitumia ziara hiyo kuwatembelea viongozi wawili wandamizi wa chama hicho, ambao ni wagonjwa.

Viongozi waliotembelewa na mbunge, ni Peter Waka, Katibu wa Baraza la Wazee Kata ya Mburahati na Mzee Mgaya, aliyekuwa mwenyekiti mstaafu wa kata hiyo.

Akiwa njiani kuelekea kwa viongzi hao, Kubenea aliongozana na makumi ya watoto waliokuwa wakimshangilia mbunge wao.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya mbunge huyo imesema, katika baadhi ya maeneo mbunge huyo alisimama na kuwanunulia maandazi, vitumbua na sambusa, watoto hao na wengine waliokuwa wamebebwa na wazazi wao waliokuwa kwenye msafara wa mbunge.

Kesho mbunge huyo wa Ubungo, anatarajiwa kufanya ziara ya kiserikali katika kata ya Kimara ambako atakagua miradi ya maendeleo na baadaye atafanya mkutano wa hadhara huko Kilungule.

error: Content is protected !!