August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea awakosha wananchi

Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, akizungumza na wapiga kura wake

Spread the love

ZIARA ya kiserikali iliyofanywa na Saed Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo katika eneo la Manzese na kisha kuhitimishwa kwa mkutano wa hadhara, imewafurahisha wakazi wa eneo hilo na kusema imewafungua macho kuhusiana na mambo mengi waliyokuwa hawayajui, anaandika Charles William.

Kubenea alifanya mkutano katika eneo la Manzese Bakhresa, baada ya kufanya ziara ya kukagua miundombinu ya maji safi na majitaka katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Manzese akiwa ameambatana na maofisa wa serikali akiwemo mtendaji wa kata hiyo pamoja na diwani Ramadhani Kwangaya (CUF).

“Nimezunguka katika maeno mengi ni machafu, watu wanatiririsha majitaka kutoka katika hoteli zao kuelekea katika makazi ya wananchi. Kuna hatari ya kuzuka kwa magonjwa ya milipuko, nimemuagiza mtendaji achukue hatua za haraka kushughulikia suala hilo kwani ni lazima afya za wananchi zilindwe,” amesema.

Kubenea pia aliutumia mkutano huo, kuelezea masuala ya maendeleo yaliyotekelezwa Muungano wa Vyama vya Ukawa, katika Manispaa ya Kinondoni pamoja na halmashauri ya jiji la Dar es Salaam linaloongozwa na Meya wa Chadema na Naibu Meya kutoka CUF.

“Kinondoni tulikuta majoho yanayovaliwa na madiwani yanafuliwa na kwa gharama ya Sh. 800 milioni kwa mwaka, tukasema suala hilo halikubaliki na tukavunja mkataba huo. Sasa hivi tuna kampuni inayofua kwa milioni Sh. 350 milioni na hivyo kuokoa zaidi ya Sh. 3 bilioni,” amesema.

Kubenea pia amefafanua uamuzi wa halmashauri ya jiji la Dar kuipa zabuni ya kukusanya mapato ya maegesho (parking) kampuni kutoka Kenya na kusema hatua hiyo, itaongeza mapato maradufu tofauti na kampuni ya wazawa ambayo ilikuwa ikitafuna mabilioni ya fedha.

“Kabla ya Ukawa kuchukua jiji, mapato yote ya jiji yalikuwa ni Sh. 13 bilioni, ambapo Sh. 6 bilioni zilikuwa ni mapato ya jiji na Sh. 7 bilioni zilikuwa ni ruzuku ya serikali lakini sisi tumempata muwekezaji atakayekusanya Sh. 57 bilioni kutokana na tozo ya maegesho ya magari katika manispaa ya Ilala pekee,” alisema huku wananchi wakionesha mshangao.

Kuhusu hasara inayotokana na uendeshaji wa Mahakama ya Jiji mbunge huyo amesema, ilikuwa ikiingiza Sh. 275,000/= tu kwa miezi sita huku matumizi yakiwa ni zaidi ya Sh. 20 milioni na hivyo wamechukua uamuzi wa kusimamisha shughuli zake kwa muda.

“Haiwezekani matumizi yote ya mahakama hiyo ikiwemo wino, printer na makaratasi vitokane na jiji lakini hakuna chochote kinachoingia, mgambo wanaishia kukamata Mama’ntilie na kuchukua mali zao bila kuwafikisha katika mahakama hiyo,” amesema Kubenea.

Wakizungumza mara baaada ya kumalizika kwa mkutano huo, baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa na kazi zinazofanywa na mbunge huyo pamoja na Boniface Jacob, aliyekuwa Meya wa manispaa ya Kinondoni.

“Hii ndiyo maana ya kuchaguliwa, lazima urudi kwa watu mara kwa mara kuwaeleza yanayoendelea. Tulikuwa hatujui vitu vingi kuhusu mali za jiji la Dar pamoja na mapato ya manispaa lakini amekuja na diwani wetu na kutujulisha yote yanayoendelea,” amesema Said Muhsin, mmoja wa wananchi waliohudhuria mkutano huo.

“Mikopo ya kina mama na vijana ilikuwa haijulikani inatolewaje na kina nani wananufaika ila diwani wetu, meya pamoja na mbunge wanasimamia kuhakikisha zinatolewa kwa uwazi. Hapa Manzese tu wananchi zaidi ya 100 tumeshapata mikopo kupitia halmashauri pamoja na mfuko wa mbunge,” amesema Husna Mussa.

Wananchi hao wamemtaka Kubenea kufanya mikutano ya hadhara mara kwa mara, kuwachambulia masuala yanayoendelea Bungeni kwani hakuna tena matangazo ya moja kwa moja ‘live’.

error: Content is protected !!