January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea ‘avamia’ Shekilango, Manzese

Spread the love

MGOMBEA ubunge Jimbo la Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saed Kubenea leo asubuhi ametembelea masoko ya Shekilango na Big Brother ya Kata ya Mabibo ikiwa ni sehemu ya kampeni zake za kuomba kura kwa wafanyabiashara wa maeneo hayo. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Kubenea ni mwandishi wa habari na Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi Publisher LTD inayochapisha gazeti la MwanaHALISI, lililoshinda kesi wiki mbili zilizopita baada ya kufungiwa na serikali kwa muda wa miaka mitatu na siku 35 kwa madai ya kuandika habari za uchochezi.

Soko la Shekilango ni maarufu kwa uuzaji wa vyakula wakati soko la Big Brother ni maarufu kwa uuazaji wa nguo zilizotumika (mitumba).

Ziara hiyo iliibua vifijo na shangwe mara baada ya wafanyabiashara hao kumuona Kubenea akiingia katika maeneo yao ya biashara huku kila mmoja akitaka kumshika mkono na wengine kupiga naye picha.

“Leo sikuja kufanya mkutano. Nimekuja kutembelea maeneo yenu ya kazi na kuwaomba kura. Kama mtanichagua nitahakikisha nashirikiana na nyinyi katika kutatua matatizo yanayowakabili kwenye biashara zenu,” Kubenea amewambia wafanyabiashra hao.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Juma Habibu ambaye ni mfanyabiashara katika soko la Big Brother amesema, “nimefurahi sana kumuona kubenea. Kuja kutuomba kura katika maeneo yetu tunayofanyia kazi ni hatua nzuri. Aitumie nafasi hii pia kuona mazingira tunayofanyia kazi zetu ili akichaguliwa kuwa mbunge aweze kutusaidia kupata fursa ili tuboreshe biashara zetu.”

Aidha, Mwanne Hussen, mfanyabiashara katika soko la Shekilango amesema, “Mimi natarajia Kubenea akishinda ahakikishe serikali inajenga soko kubwa la kisasa zaidi ya hili ili wanawake, vijana na walemavu wanaoweza kufanya kazi wapate nafasi. Kwa sasa soko ni finyu.”

Ziara hiyo ilianza saa 5 asubuhi katika soko la Shekilango kisha Big Brother na kumalizikia Manzese darajani ambapo iliambatana na kubandika mabango katika maeneo ya wazi ya umma, kugawa vipeperushi kwa wafanyabiashara na wakazi wa maeneo hayo.

Hata hivyo, baadhi ya mabango ya Kubenea yaliyobandikwa siku za nyuma yalikutwa yamezibwa na mabango ya mgombea wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Didas Masaburi. Kubenea ametaja hatua hiyo kama ni “uvunjifu wa sheria kwa makusudi.”

error: Content is protected !!