June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea ashtukia janja ya CCM

Spread the love

SAED Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam, amefichua hujuma zinazotaka  kufanywa na Aron Kagurumjuli,  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ili kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi wa Meya baada ya kugawanywa kwa halmashauri hiyo, anaandika Shabani Matutu.

Kubenea pia amelaani kitendo cha Halmashauri ya Kinondoni kutokuwa na Baraza la Madiwani tangu septemba 16 mwaka huu baada ya kuvunjwa kwa baraza hilo bila mgawanyo wa madiwani kuwekwa wazi.

“Chama cha Wananchi (CUF) kwa kushirikiana na Chadema tuna madiwani wa kutosha ambapo kwa vyovyote vile, tunatakiwa kushinda umeya kuendelea kuchapa kazi kama tulivyoanza lakini CCM inataka kuvuruga uchaguzi huo na kutuwekea mizigo isiyohudhuria vikao wala kutoa mawazo ya kujenga halmashauri’’amesema.

Kubenea amesema kuwa Chadema ina madiwani Saba wa  viti maalum kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ambapo wanne wanatakiwa kuwa Kinondoni na watatu wanatakiwa kupelekwa Ubungo lakini Mkurugenzi wanne Ubungo na watatu Kinondoni ili kupunguza kura.

Kubenea amedai kuwa hujuma nyingine inayotaka kufanywa na CCM ni kumchukua Profesa  Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kutoka Manispaa ya Ilala na kumhamishia Kinondoni ili aweze kupiga kura jambo ambalo si sahihi.

“Profesa Ndalichako hapo awali alisaini kutokea Ilala na sio Kinondoni huku Naibu Spika wa Bunge Ackson Tulia akiwa mkazi wa Kibamba lakini wote hao wanataka kuhamishiwa Kinondoni ili kuongezea kura za CCM na kuhamisha baadhi ya madiwani wa Chadema ili kupunguza kura,” amesisitiza.

Henry Kilewo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam amesema Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na CCM lazima watambue kuwa Chadema haitakubali hujuma wanayoipanga ifanikiwe na kwamba watapambana hadi haki itendeke kama ilivyotokea hapo awali.

“CCM wanajua hawawezi kushinda na kuongoza Manispaa ya Kinondoni, wanalazimisha kutuingizia mizigo ya mawaziri na Naibu Spika ambao tangu waletwe kwaajili ya kupiga kura katika uchaguzi wa mwanzohawajawahi kuhudhuria hata kikao kimoja,” amesema Kilewo.

Kubenea ziarani

Kubenea amefanya ziara katika eneo la soko, Stendi ya Simu 2000 na Ubungo Stendi ambapo amezungumza na uongozi wa maeneo hayo sambamba na kusikiliza kero za wafanyabiashara wa maeneo hayo.

Kubenea amesema kuwa wafanyabiashara wameathiriwa na kauli ya Rais John Magufuli, ya kuwataka wafanyabiahara kuendelea kufanya biashara zao bila kubugudhiwa kiasi cha kwamba hata waliokuwa katika eneo hilo la soko waliondoka na kurudi tena barabarani.

Aidha amesema kitendo cha magari ya Msata, Mlandizi na Mbezi kutofika katika eneo eneo la stendi ya Simu 2000 kinawakosesha wateja wafanyabiashara wa eneo hilo na kuahidi kutafutia ufumbuzi suala hilo.

Echilia Hamis, Meneja wa Soko hilo la simu 2000, amesema wamekuwa na changamoto kubwa ikiwa ni pamoja na kukosa wafanyabiashara ambapo awali kulikuwa na takribani magari 400 yaliyokuwa yakilipia ushuru na kusaidia kuongeza kipato cha halmashauri.

Akiwa katika eneo la kituo cha mabasi Ubungo, alipokea kero za wafanyabiashara wa eneo hilo pamoja na abiria ambapo wametaka walinzi shirikishi kuondolewa kwa kuwa wanawanyanyasa, huku mawakala wa mabasi wakiomba kutengewa eneo la ofisi yao.

Kubenea ameahidi kurejea tena katika eneo hilo siku ya Jumatatu ya tarehe 10 Oktoba ili kuweza kujadili baadhi ya mikakati ya kutafutia suluhu ya kudumu matatizo ya eneo hilo.

error: Content is protected !!