August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea apandishwa kizimbani Dodoma

Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo

Spread the love

SAED Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), amefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Dodoma na kusomewa shtaka la kumshambulia mbunge Juliana Shonza wa Chama Cha Mapinduzi, anaandika Dany Tibason.

Wabunge nane wa Chadema walikamatwa na polisi juzi mjini Dodoma kwa madai ya kumshambulia Shonza ambaye ni mbunge wa viti maalum (CCM) mkoa wa Songwe, hata hivyo baada ya mahojiano ni Kubenea pekee aliyefikishwa kortini.

Waliokamatwa na kuhojiwa ni pamoja na Pauline Gekul, Suzan Kiwanga, Joseph Selasini, Saed Kubenea, Frank Mwakajoka, Cecil Mwambe na wengine wawili.

Kubenea anadaiwa kufanya shambulizi la kudhuru mwili, kinyume cha kifungu Na. 240 cha Sheria ya Makossa ya Jinai sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Akisoma mashtaka hayo mbele ya James Karayemaha, hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Wilaya, Wakili wa serikali Beatrice Nsana ameiambia mahakama kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo tarehe 3Julai mwaka huu, katika viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, Kubenea anayetetewa na mawakili watano ambao ni Jeremiah Mtobesya, James Ole Millya, Fred Kalonga, Izack Mwaipopo na Dickson Matata alikana kosa hilo.

Hakimu Karayemaha alisema kuwa dhamana ya mshtakiwa iko wazi kwa sharti la kuwa na mdhamini mmoja mwenye kitambulisho, barua kutoka serikali ya mtaa na Sh. 1 milioni.

Kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika kesi hiyo itatajwa tena tarehe 26 Julai mwaka huu.

Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Freeman Mbowe Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani amewaeleza wanahabari kuwa ni kilichofanyika ni mwendelezo wa kuwafedhehesha na kuwadhalilisha wabunge wa upinzani.

“Spika ameshabikia kitendo hiki na kusema anaruhusu wabunge wa Chadema washtakiwe kwa kosa la kubuni. Bila hata uchunguzi majina ya watu waliopo bungeni na wasiokuwepo bungeni kama Cecil Mwambe ambaye hakuwepo kabisa hata Dodoma wakadai naye alimpiga Shonza.

“Leo wamemtafuta mbunge mmoja (Kubenea) na kumshtaki kama chambo, lakini hakuna mbunge hata mmoja wa Chadema aliyemshambulia Shonza,” amesema Mbowe.

error: Content is protected !!