February 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea amtaka Kamanda Sirro kujipima

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro. Picha ndogo, Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo

Spread the love

MBUNGE wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, “kujipima” kutokana na kile alichoita, “kushidwa kutimiza wajibu wake,” anaandika Mwandishi Wetu.

Amesema, “Kamanda Sirro, ameshindwa kazi. Hivyo basi, anapaswa kujipima kama bado anazo sifa za kuwa mkuu wa jeshi la polisi nchini.”

Kubenea anasema, ametoa kauli hiyo, kufuatia Sirro kudai kuwa Jeshi la Polisi limeshindwa kuchunguza shambulio la risasi alilofanyiwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antipas Lissu, kutokana na kukwamishwa na dereva wake, Simon Mohamed.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa mchana huu, Kubenea amesema, “kauli hii, inaonyesha mashaka ya utayari wa nia ya jeshi la polisi katika kufanya uchunguzi sahihi na kwa wakati kwa watu waliomshambulia Mhe. Lissu.”

Amesema, pamoja na jeshi la polisi kufahamu kuwa Simon anapata matibabu ya kisaikolojia huko Nairobi, lakini kamanda Sirro mwenyewe hawajaweza kumhakikishia dereva huyu usalama wa uhai wake hapa nchini.

“Kamanda Sirro hajaeleza ipi mipango ya jeshi lake ya kulinda maisha ya Simon ili asidhuriwe na hao wanaoitwa na serikali, ‘watu siojulikana’ na ambao jeshi hilo limesema haliwajui,” ameeleza Kubenea.

Amesema, “hakikisho la jeshi la polisi kwa maisha ya dereva wa Lissu, ni muhimu kwa kuwa ndiye aliyekuwapo kwenye eneo la tukio na kwamba tayari amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema, ‘anawafahamu’ waliomshambulia kwa risasi” bosi wake.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, kwamba hadi hivi sasa – takribani mwezi mmoja tangu Lissu ashambuliwe – jeshi la Polisi limeshindwa kuwapata hao “wasiojulikana,” ni uthibitisho mkubwa kuwa jeshi hilo halina mpango wowote wa kuwatafuta na kuwapeleka mahakamani wauaji hao.

Amehoji: “Kama hiki kinachoelezwa na IGP Sirro ndio sababu kuu ya jeshi la polisi kushindwa kutimiza wajibu wake, kwanini Kamanda Sirro ameshindwa kwenda Nairobi kumhoji Simon, badala yake anaendelea kung’ang’ania arudi nchini ambako hajahakikishiwa usalama wake?”

Kwa muktadha huu, Kubenea anasema, “ni vema Kamanda Sirro akajipima na kujiuzulu kutokana na kushindwa kutenda kazi zake kwa uweledi.”

Lissu alishambuliwa kwa risasi mchana wa tarehe 7 Septemba mwaka huu, nyumbani kwake mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kutoka kuhudhuria mkutano wa asubuhi wa Bunge.

Kwa sasa yuko mjini Nairobi anakopatiwa matibabu ya majeraha ya silaha. Lissu alishambuliwa na risasi zaidi ya 38.

error: Content is protected !!