January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea ammlilia Edson Kamukara

Mkurugenzi wa HHPL, Saed Kubenea akishindwa kujizuia akiwa anamuaga aliyekuwa mfanyakazi wake, Edson Kamukara

Spread the love

MKURUGENZI mtendaji wa Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), Saed Kubenea, ametaka waaandishi wa habari kuchunguza kifo cha Edson Kamukara, aliyekuwa mhariri mwanzishi wa gazeti hili.

Akizungumza wakati wa kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu Kamukara, Kubenea alisema, ni kweli kwamba Edson hayuko nasi tena. Ni kweli kuwa Edson amefariki dunia, lakini kwamba kipi kimesababisha kifo chake, ni jambo ambalo linahitaji uchunguzi, tena wa kina zaidi.” Anaripoti Erasto Stanslaus … (endelea).

Yafuatayo ni maelezo ya Kubenea katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam.

Kampuni ambayo imekuwa mwajiri wa Edson Kamukara kwa miezi mitatu kamili sasa – HHP Limited – imepata pigo. Ni masikitiko makubwa. Ni uchungu usio na kiwango. Ni ukiwa usiozibika.

Tumeondokewa na ndugu. Tumeondokewa na rafiki. Lakini zaidi, tumeondokewa na mchapapakazi. Tulimpenda sana Edson.  Tuseme kweli; naye alitupenda. Tulifanya naye kazi kwa uelewano mkubwa. Tulithamini mawazo yake kama yeye alivyothamini ya kila mmoja wetu. Tutamkosa. 

Edson alikuwa mwandishi wa habari wa viwango vyake. Alitenda kazi yake huku akijifunza. Hakuchoka kujifunza. Hakuchoka kuuliza. Lakini pia hakuchoka kufundisha. Alikuwa mwelekezaji wa waandishi wa habari waliokuwa chini yake na wao walimpenda na kumkimbilia wakati wote. Watamkosa.

Kifo cha Edson Kamukara, mwandishi wa habari mwenzangu na mfanyakazi katika kampuni ninayoingoza ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), kilitokea juzi Alhamisi, nyumbani kwake Mabibo jijini Dar es Salaam. 

Edson alikuwa mhariri mwanzilishi wa gazeti letu linalochapishwa kwenye mtandao liitwalo MwanaHALISI Online. Ameondoka wakati linaanza kuwa maarufu. Wakati linaanza kukua kwa kasi. Wakati linaanza kuimarika na kuvutia wengi. Tutamkosa sana.

Niliongea na Edson kwa simu mara ya mwisho Jumapili iliyopita, wakati akiwa nyumbani kwao Bukoba, mimi nikiwa njiani kwenda Dodoma kikazi. Ni katika mazungumzo yetu hayo, alinieleza kuwa alikuwa anasumbuliwa na malaria.

Tulizungumza mengi kuhusu kazi zetu na hasa kuhusu moja ya stori zake za mwisho kuandika ambayo alikuwa anaendelea kuifuatilia. Nilimshauri ajipumzishe zaidi na kuhakikisha anapata matibabu ya kutosha. Lakini leo hatunaye. 

Edson ni mmoja wa waandishi wachache nchini walioamini kwamba maadili ya uandishi hayatungwi na serikali wala wanasiasa wenye uchoyo wa kuandikwa kwa mapambo; bali wanataaluma wenyewe. 

Edson alikuwa mpole. Alikuwa muwazi, mkweli na muungwana kiasi cha kuwa rahisi kwa mtu yeyote kufanya naye urafiki. 

Edson Kamukara ameishi kipindi chake na amefanya kipande chake cha kazi. Laiti kila mmoja wetu angefanya kazi yake hadi siku chache au saa chache kabla ya kuaga dunia. 

Tulivyo wazima sisi, ndivyo Edson Kamukara alivyokuwa mchana wa juzi; siku ya Alhamisi. Alivyo yeye sasa ndivyo tutakavyokuwa sisi siku moja.

Sisi tuliobaki, tutaendelea kumuenzi. Uadilifu wake, ucheshi wake, uzalendo wake na misimamo yake kupigania maadili ya taaluma ya uandishi wa habari na kupigania haki, vitaendelea kutuchochea kutenda kazi zetu huku tukimkumbuka na kumtolea mfano.

Mwisho, ninawapa pole sana ndugu zake na marafiki zake. Mungu awazidishie nguvu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu. 

Edson Kamukara alale pema peponi.

Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.

error: Content is protected !!