Monday , 11 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Kubenea amng’ang’ania Mkurugenzi wa Jiji
Habari za SiasaTangulizi

Kubenea amng’ang’ania Mkurugenzi wa Jiji

Spread the love
MBUNGE wa Ubungo (CHADEMA), Saed Kubenea, amemtuhumu mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Spora Liana, kutumia madaraka yake vibaya na kwa maslahi binafsi. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam …  (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Chadema, Kanda ya Pwani, leo tarehe 17 Januari 2020, Kubenea amesema, mkurugenzi huyo ameamua kulivalia njuga suala la kuondoka kwa Meya madarakani, ili kuweza “kupitisha madudu yake.”

“Tunafahamu kuna miradi mingi imepitishwa na Jiji na kutengewa mamilioni ya shilingi, lakini utekelezaji wake, haulingani na fedha iliyotolewa,” ameeleza Kubenea.

Amesema, “baadhi ya miradi hiyo, imegubikwa na ufisadi. Mengine imetumia fedha nyingi kuliko zile zilizopangwa na madiwani” na kwamba kuna wakati mkurugenzi anasaini mikataba mikubwa kwa niaba ya halmashauri, kabla ya kupata kibali cha Kamati ya Fedha ama Baraza.

Kubena anasema, njama zote za kumuondoa Meya zinaongozwa na mkurugenzi huyo na kwamba anatumia kivuli cha Isaya kuwa meya kutoka upinzani, kufanikisha malengo yake.

Amesema, “…nchi hii inafuata mfumo wa vyama vyingi vya siasa, na kila mtu ana haki ya kujiunga na chama chochote atakacho. Mkurugenzi asitumie kivuli hicho kutogombanisha kwa sababu kabla ya figisu hizi, tulikuwa tunaliongoza Jiji kwa maelewano makubwa.”

Kwa mujibu wa Kubenea, kufuatia kutilia mashaka miradi waliyopitisha, anajiandaa kuwasilisha baadhi ya nyaraka kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa nchini tanzania (TAKUKURU), ili kuweza kufanyika uchunguzi.

Akizungumzia mkutano wa jana wa Kamati ya Fedha ya Jiji, Kubenea amesema, kikao hicho ambacho kilikuwa cha kwanza kufanyika tokea Meya wa Jiji, Isaya Mwita, kutangazwa kung’olewa kwenye nafasi yake, hakikuwa halali.

“Mkutano wa jana umeendeshwa kinyume na Kanuni. Kikao kilifanyika chini ya usimamizi wa Polisi na tena wakiwa na mtutu wa bunduki,” ameeleza Kubenea na kuongeza, kutokana na hali hiyo, wajumbe hawakupata fursa ya kujadili masuala yaliyowasilishwa kwa usahihi.

Anasema, mbali na mkutano huo kuendeshwa chini ya mtutu wa bunduki, baadhi ya wajumbe waliohudhuria hawakuwa wajumbe halali.

Amewataja wajumbe ambao siyo halali, ni Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo; Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta; Meya wa Manispaa ya Ilala, Omary Kumbilamoto na Meya wa Manispaa ya Kigamboni, Maabad Hoja.

Kutokana na hali hiyo, mbunge huyo amesema, taarifa yote iliyoletwa kwenye kikao cha fedha na maamuzi yake, siyo halali kwa kuwa kikao hicho kimeendeshwa kinyume na taratibu.

Amesema, mkutano wa jana wa Jiji ulifunguliwa na Meya Isaya na ulianza kuvurugika pale baadhi ya wajumbe walipoanza kuhoji uhalali wa mameya zinazounda Jiji.

Amesema, hata hoja ya kuruhusu vijana wa bodaboda kuingia mjini haikupata nafasi ya kujadiliwa kutokana na mkutano huo kukosa utulivu na wajumbe kutawaliwa na hofu.

Baraza la Madiwani la Jiji la Dar es Salaam, lililokutana wiki iliyopita, lilipitisha kinyume na taratibu, azimio la kumuondoa Meya Isaya (Chadema), katika kiti chake.

Kwa mujibu wa Kanuni za Jiji, Meya anaondolewa kwenye kiti chake baada ya azimio hilo kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wote. Jumla ya wajumbe wote wa Jiji wako 26 na hivyo theluthi mbili ya wajumbe waliotakiwa kupitia azimio la kumuondoa Meya wa Jiji, ni watu kati ya 17 na 18.

Katika baraza la madiwani la Jiji, Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho ndicho mmoja wa wajumbe wake aliwaslisha hoja ya kumuondoa madarakani Meya, Abdallah Chaurembo, wana jumla ya madiwani 16 tu, na hakuna diwani hata mmoja wa upinzani aliyeunga mkono hoja hiyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Jaji Kiongozi akerwa wananchi kukosa imani na mahakama

Spread the loveWATENDAJI wa Mahakama ya Tanzania, wametakiwa kuweka mikakati itakayosaidia kurejesha...

BurudikaHabari za Siasa

Samia amchangia Professa Jay mil. 50, Chadema, wasanii wamwaga manoti

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amechangia kiasi cha Sh 50 milioni...

Habari za Siasa

Biteko: Samia ni muumini wa maridhiano sio kwa kuigiza

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Mpango: Sitakufa bali nitaishi

Spread the loveMAKAMU  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk....

error: Content is protected !!