Friday , 2 June 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Kubenea amchongea Tarimba kwa wanakinondoni
Habari za Siasa

Kubenea amchongea Tarimba kwa wanakinondoni

Spread the love

SAED Kubenea, mgombea Ubunge Kinondoni jijini Dar es Salaam kupitia ACT-Wazalendo, amemchomgea Abbas Tarimba, mgombea ubunge jimbo hilo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa wananchi ili wasimchague. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kinondoni … (endelea).

Kubenea amewaomba wananchi wa Kinondoni kutomchagua Tarimba katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 kwa maelezo atakwenda kutekeleza masilahi ya chama chake badala ya wananchi watakaomtuma.

Mgombea huyo ubunge wa ACT-Wazalendo ametoa kauli hiyo jana Ijumaa tarehe 25 Septemba 2020 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kigogo jijini Dar es Salaam.

Kubenea alisema, wakati Tarimba akiwa Diwani wa Hananasif wilayani Kinondoni, aliungana na msimamo wa CCM wa kutolipa fidia wananchi waliotakiwa kubomolewa makazi yao kwa ajili ya kupisha miradi ya ujenzi wa barabara na upanuzi wa Mtoa wa Ng’ombe.

“CCM wanapewa fedha na Benki ya Dunia kujenga barabara na kupanua Mto wa Ng’ombe kutoka Chuo Kikuu wakasema hatuwezi kulipa fidia hili zoezi mfanye wenyewe.”

“CCM wakakataa kulipa fidia sisi wana Ukawa katika Baraza la Madiwani tukapitisha azimio katika mradi huu wananchi walipwe fidia,” alisema Kubenea.

Kubenea aliyekuwa mbunge wa Ubungo kupitia Chadema alisema, wakati Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni haijagawiwana kuwa na halamshauri mbili ya Ubungo na Kinondoni, madiwani wa CCM walipingana na madiwani wa upinzani ambao walikuwa wanapigania wananchi wapewe fidia.

Hata hivyo, Kubenea alisema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kushirikiana na Chama cha Wananchi (CUF) vilikuwa vinaongoza halmashauri hiyo, vilipitisha azimio la kukopa fedha katika Benki ya CRDB kulipa fidia wananchi ili Benki ya Dunia (WB) itoe fedha za utekelezaji wa mradi huo.

“Tukaenda benki ya CRDB tukakopa fedha kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wa Kinondoni, bila sisi msingelipwa fidia sababu jambo lile lilisimamiwa na Serikali Kuu lakini sisi tuliamua kulipa fidia.”

“Hiyo kazi yetu ya kwanza tuliifanya Kinondoni ambapo Tarimba akiwa diwani wa CCM alikataa kulipa fidia aje hapa aseme kwamba sio kweli,” alisema Kubenea.

Akizungumzia ahadi zake, Kubenea aliwaomba wananchi wa Kinondoni wamchague kwa kuwa atamaliza tatizo la mafuriko ndani ya miaka mitano.

Kubenea alisema ataiomba Benki ya Dunia fedha za upanuzi wa Mto Msimbazi na Mto wa Ng’ombe.

“Ukiwa na mbunge anayejua kazi yake, maendeleo lazima yapatikane. Kinondoni kuna tatizo la mafuriko, nawaambia ndani ya miaka mitano nitalimaliza kwani kuna fedha za Benki ya Dunia za kupanua Mto Msimbazi wao wanawaita mabeberu lakini sisi tutakwenda kuwapigia magoti kuomba fedha za upanuzi huo,” ameahidi Kubenea.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Lusinde: CCM hatuliachii ng’o jimbo la Moshi Mjini

Spread the loveMJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Livingston...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar: Bakharesa hajavamia shamba letu

Spread the love  IKULU Visiwani Zanzibar, imeeleza kuwa eneo la kiwanda cha...

Habari za SiasaTangulizi

Zanzibar watangaza rasmi kuwa shamba la Razaba ni mali yao

Spread the love  SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imetangaza rasmi kwamba shamba...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Mwinyi azindua Kamati ya Maridhiano Visiwani

Spread the love  RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Hussein...

error: Content is protected !!