SAED Kubenea, mgombea ubunge wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam kupitia ACT-Wazalendo amewataka wananachi kuchagua viongozi wenye uchungu na taifa lao. Anaandika Yusuph Katimba, Dar es Salaam…(endelea).
Amesema, wabunge wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), chini ya mwenyekiti wao wa sasa, John Magufuli wanatenda tofauti na CCM chini ya Hayati Benjamin William Mkapa (awamu ya tatu) na Jakaya Mrisho Kikwete (awamu ya nne).
Akizungumza na wakazi wa jimbo hilo, eneo la Soko la Afrika Sana leo Jumatano tarehe 7 Oktoba 2020, Kubenea amesema, wabunge waliotokana na chama hicho waliisimamia serikali na Bunge litekeleze wajibu wake, lakini wa sasa wanaimba mwimbo wa mwenyekiti wao ndani ya Bunge.
“Ushahidi wa hilo, ni Mkapa na Kiwete. Wakati wa Mkapa Bunge lilikuwa Bunge kwelikweli, ni kipindi hicho ambacho mawaziri walikuwa hawakai bungeni, kiti kilikuwa moto.”
“Mnakumbuka stori ya minofu ya samaki (mapanki) iliyomuondoa Joseph Mbilinyi, aliyekuwa Naziri Waziri wa Fedha? mkanukubuka sakata la sukari liliyomuondoa Iddi Simba?,” amesema Kubenea.
Akizungumza kuhusu Bunge kuwa ‘moto’ kutokana na CCM na wabunge wa upinzani kuisimamia serikali, ametoa mfano wa sakata la Richmond.
“Wakati wa Kikwete ni tofauti na sasa, wakati huo mnakumuka sakata la Richmond lililomuondoa madarakani aliyekuwa Waziri Mkuu (Edward Lowassa) na mawaziri wengine wawili.”
Mawaziri wengine ni wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.
Kubenea amesema, “Operesheni Tokomeza iliondoa mawaziri wanne akiwemo David Matayo, lakini katika Bunge la 11 la Spika Ndugai (Job Ndugai), Bunge lilimezwa na serikali. Wambunge wa CCM wamepoteza hadhi na sifa ya kuisimamia serikali.”
Operesheni tokomeza ilitokea mwaka 2014 ambayo mwisho wa uchungizi wa taarifa yake bungeni, mawaziri wanne waling’omba.
Mawaziri waliong’olewa ni Khamisi Kagasheki wa Maliasili na Utalii, Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Amesema, Wananchi wanapaswa kuchagua wabunge walio tayari kufa kwa ajili ya nchi yao na wasidanganywe kauli zinazotolewa kwamba, wakichagua mpinzani hawatopata maendeleo.
“Maendeleo ya chii kwa sehemu kubwa yanategemea fedha za mikopo hivyo yatafika kila mahali. Benki ya Dunia (WB) ilitengeneza interchange ya Ubungo na imejenga bila kujali mbunge wake anatoka upinzani.”
“Chagueni mbunge ambaye hatosaliti, atatumia ubunge wake kukandamiza wengine na ambaye hana rekodi ya kufukuzwa fukuzwa.”

“Tarimba (Abbas Tarimba, mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM) alifukuzwa kwa bakora kwenye Klabu ya Yanga, Tarimba alikuwa muasisi wa Yanga Kampuni alifukuzwa, Yanga Afrika ilikuwa inatembeza bakuli licha ya kuwa na mashabiki milioni 20, sasa imebebwa na GSM na imekuwa imara baada ya Tarimba kuivuruga.”
Amesema, anayo dhamira ya kweli ya kusimamia maendeleo ya wananchi na ndio maana licha ya kuwindwa kuhamia CCM, hakufanya hivyo.
“CCM ni kichaka fulani, sisi waadilifu hatuwezi kwenda huko. Naomba mnichague mimi ili tujenge kiwanda cha mbolea kinachotokana na taka, CCM wameshindwa sisi tutajenga tuzalishe ajira kwa watoto wetu,” amesema.
Amewaambia wakazi wa eneo hilo kwamba, kwa miaka yote CCM walishindwa kujenga soko hilo kisasa, lakini Kinondoni chini ya upinzani limejengwa hivyo, na mengine yatafanyika.
“Mlikuwa mnafanya biashara katika mazingira magumu, miaka 20 karibu soko hili halikuweza kujenga na madiwani wa CCM. Tulipokuwa madiwani wa UKAWA tukiongoza Halmashauri ya Kinondoni, ndio tulipitisha mradi wa solo hili mwaka 2017,” amesema.
Kubenea ameanza kampeni zake za mtaa kwa mtaa aliyoiita ‘mobile kampeni’ aliyoianza jana ambapo atakuwa anawafuata wakazi wa jimbo hilo kwenye maeneo yao.
Leave a comment