August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea ajitosa kunusuru wajawazito Kimara

Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, akizungumza na wapiga kura wake

Spread the love

SAED Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo ameahidi kuishawishi Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ilifanyie ukarabati jengo la wazazi la zahanati ya Mavurunza lililopo kata ya Kimara jijini Dar es Salaam, anaandika Pendo Omary.

Kubenea amechukua hatua hiyo alipoitembelea zahanati hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara za mbunge huyo katika kata ya Kimara ambapo pia alikabidhi jenereta lenye thamani ya Sh. 5.6 milioni ili kusaidia zahanati hiyo kuendelea kufanya kazi wakati umeme wa Tanesco unapokatika.

Doroth Mushi, Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo amesema wamesimamisha huduma katika zahanati hiyo kutokana na jengo la wazazi kuwa na ufa mkubwa unaohatarisha usalama wa wagojwa na wafanyakazi.

“Zahanati hii ilianza mwezi Oktoba 2010 na mpaka sasa wastani wa wanawake 70 wamejifungulia hapa kwa usalama. Lakini kwa sasa jengo la wazazi ni bovu lina ufa mkubwa ambao unahatarisha usalama wa mama, mtoto pamoja na mtoaji huduma,” amesema Doroth.

Doroth amezitaja changamoto zingine zinazoikabili zanahati hiyo kuwa ni ukosefu wa maji safi na salama kutoka Dawsco, ambapo wanalazimika kutumia maji ya chumvi ambayo hayafai kutumika katika kusafishia vitendea kazi.

Uhaba wa dawa, uwepo wa barabara mbovu ambayo inatumika kukifikia kituo hicho hasa wakati wa mvua na ukosefu wa jengo ambalo lingetumika kutoa huduma ya kliniki kwa watoto ni changamoto nyingine katika utoaji wa huduma wa zahanati hiyo.

Akijibu taarifa iliyotolewa na Doroth mbele ya wajumbe wa bodi ya zahanati hiyo, wananchi na viongozi wa serikali ya mtaa na kata, Kubenea amesema, “Yapo mambo ninaweza kuyafanya kama Mbunge na yapo mambo ambayo yanapaswa kufanywa na halmashauri ya Ubungo. Hayo ya Halmashauri nitahakikisha ninayapeleka na kuyasimamia kwenye vikao, likiwemo suala la maji na ukarabati wa jengo la wazazi.

“Kuhusu eneo la kutoa huduma ya kliniki ya watoto nitatoa fedha kwenye mfuko wa jimbo ili lijengwe tenti na kununua viti na meza kama mlivyoomba. Kuhusu barabara, mwaka huu hakuna fedha iliyotengwa Ila ndani ya miezi miwili nitahakikisha barabara inachogwa na mwaka ujao nitahakikisha fedha zinategwa.”

Aidha, kubenea ametembelea mradi wa urasimishaji makazi ambapo mtaa wa Kulungule A unatumika kama mfano katika mradi huo na kuahidi kuhamaisha wananchi kushiriki ipasavyo katika kupima maeneo yao na kupata hatimiliki.

Samwel Katimbi, Mkurugenzi msaidizi wa mradi huo amesema “lengo la mradi ni kuona wananchi wa eneo hili wanapata hatimiliki kwa maendeleo ya kiuchumi na kupunguza migogoro ya ardhi. Kituo hiki kitaendesha taratibu zote za upimaji na kupokea malipo ya hati.”

error: Content is protected !!