January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea aiumbua NEC, akamata kadi feki za kupigia kura

Spread the love

MGOMBEA  Ubunge wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Ubungo,  Saed Kubenea, amedai kuwa zaidi ya kadi milioni mbili za kupigia kura zinatengenezwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kwa ajili kuongeza  kura za ziada za kukiwezesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda katika uchaguzi Oktoba 25, mwaka huu.

Kubenea alidai tayari amepata kadi 100 ambazo alidai amepatiwa  baadhi ya maafisa wa Tume ambao walimuahidi kumpatia kadi nyingine zaidi. 

“NEC wameweka mkakati wa kukisaidia CCM kupata ushidi katika kufanikisha hilo wametengeneza kadi ambazo hazijajazwa taarifa zozote  ambazo wanatarajia kuzitumia kwa kuingiza taarifa za watu ambao hawastahili ili wapige kura,” alisdai na kuongeza:

“Tunashukuru kuna wasamaria wema ndani ya Nec ambao hawakubaliani na hujuma hizo, wameamua kutuambia na wametuahidi kutupa kadi nyingine zaidi, na huyo aliyenipa hizi 100 aliniambia hata nikitaka kadi hizo 100,000 atanipa.”

Kubenea alisema tayari amekabidhi kadi hizo kwa mwanasheria na kwamba kabla ya  kuzikabidhi, aliapishwa kwanza.

“Naomba Nec  iache kufanya kazi za CCM, kama itaendelea kufanya hivi itaipeleka nchi kwenye machafuko, tunaomba ifanye kazi kwa uadilifu na ninamuomba Mwenyekiti wa Tume hiyo asiipeleke nchi pabaya, hatutaki kuona watu ambao hawakuandikishwa wanaingizwa kwenye daftari,” alisema.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji, Damian Lubuva, alisema hawezi kuzungumzia chochote kwa kuwa hajaziona kadi hizo.

“Kama Chadema wamesema kadi hizo ni za kwetu ni vema wangezileta kwetu ili tuone kama kweli ni zetu, kwa kuwa wamezungumza hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari na mimi sijaziona kadi hizo siwezi kuzungumza chochote mpaka nidhibitishe,” alisema Jaji Lubuva na kuongeza:

“Hata nikizungumza hapa itaonekana tunabishana Tume na Chadema,  wao kama kweli wanazo watuletee tuthibitishe.”

Naye mgombea ubunge wa Chadema Kawe, Halima Mdee, Halima Mdee, aliitaka Tume hiyo kuhakikisha inahakiki taarifa za wananchi katika vituo vya kupigia kura walivyojiandikishia na si katika kata.

Alisema taarifa ambazo amepata ni kwamba baadhi ya ofisi za wakurugenzi  wameambiwa  na Nec kwamba wananchi wao watahakiki taarifa zao katika ofisi za kata na si katika vituo walivyojiandikishia kama inavyotakiwa kutokana na  uchache wa vitabu.

Jaji Lubuva alisema changamoto za uhakiki wa wapiga kura ni suala ambalo linashughulikiwa kwa kushirikiana na wakurugenzi na kwamba watahakikisha kila aliyejiandikisha anahakikiwa.

error: Content is protected !!