MGOMBEA Ubunge Kinondoni kupitia ACT-Wazalendo, Saed Kubenea ameiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), akiiomba imwondoe Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Kinondoni, Aaron Kagurumjuli. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Kubenea amedai Kagurumjuli anakiuka sheria na kanuni za uchaguzi, hali inayoweza kusababisha uchaguzi utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 kutokuwa huru na haki.
Hayo ameyasema leo Jumatatu leo tarehe 26 Oktoba 2020 wakati anazumgumza na wanaandishi wa habari Ofisi za Makao Makuu ya ACT-Wazalendo, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Kubenea amesema, Kagurumjuli anaonesha waziwazi kumpendelea Mgombea Ubunge wa CCM katika jimbo hilo, Abbas Tarimba.

Ameishauri NEC kufuatilia kwa ukaribu muenendo wa Kagurumjuli na matukio yanayoendelea katika mchakato wa uchaguzi kwenye jimbo hilo.
“Mimi binafsi, nimeaindikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuiomba ama imuengue kusimamia kazi hii ya kitume ama ifuatilie kwa karibu mienendo na matukio ya Kinodnoni ili uchaguzi uishe kwa usalama na amani ili anayeshinda uchaguzi ndio atangazwe mshindi,” amesema Kubenea.
Amesema, nakala ya barua hiyo ameiwasilisha kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage.

“Na barua, nimeinakili kwa mwenyekiti NEC, IGP Sirro ili imuondoe kwa kuwa ana viashiria vya U-CCM vilivyobobea na vinavyoweza kuhatarisha amani,” amesema Kubenea.
Kubenea amekumbushia kile kilichotokea katika uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Kinondoni Februari mwaka 2018 ambapo Kagurumjuli alichelewa kuwapatia barua za utambulisho mawakala wa Chadema.
Amesema, hatua hiyo Chadema waliandamana kwenda ofisi za msimamizi wa uchaguzi huo (Kagurumjuli) ambapo ilitokea vurugu iliyosababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.
Leave a comment