Sunday , 25 February 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kubenea ahoji: Who is Makonda?
Habari za SiasaTangulizi

Kubenea ahoji: Who is Makonda?

Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, akizungumza na wapiga kura wake
Spread the love

MBUNGE wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, amemvaa Waziri Mkuu wa Jamhuri, Kassim Majaliwa kuhusiana na kauli yake kuwa “serikali inachunguza vitendo vya utekaji,” anaandika Pendo Omary.

Akichangia mjadala juu ya hotuba ya wizara ya Sheria na Katiba, bungeni mjini Dodoma jana Jumanne, Kubenea alisema, serikali inayohitaji kuaminiwa, ni sharti iwe wazi.”

Amesema, serikali imekuwa ikisisitiza kuaminiwa na Bunge na kwamba inafuatilia kwa karibu matukio yote ya utekaji na utesaji, lakini haionyeshi dalili za kutaka wananchi waiminiwa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, serikali kupitia kwa waziri mkuu Kassim Majaliwa imesisitiza tuiamini. Na kwa kweli, humu ndani ukiuliza nani haiamini serikali hii, huwezi kumpata. Hii ni kwa kuwa serikali hii ni yetu sote. Ndio maana tuko hapa kuisimamia, kuishauri na kupitisha bajeti yake,” ameeleza.

Amesema, “lakini serikali inayotaka kuaminiwa ni lazima iwe wazi. Aliyetaka kumpiga risasi Nape Nnauye, anafahamika. Ni afisa kutoka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Hajakamatwa na serikali, haijamtaja wala haijatengana naye.”

Kubenea alikuwa akirejea kauli iliyotolewa na waziri mkuu bungeni wakati akijibu swali juu ya kuwapo kwa vitendo vya utekaji na utesaji nchini. Swali juu ya kushamiri kwa vitendo hivyo, liliulizwa na Kiongozi wa Upinzani, Freeman Mbowe.

Akizungumza kwa hisia kali, Kubenea amesema, “kuna watumishi wa umma wamefanya makosa makubwa ya kijinai. Miongoni mwao, ni Paul Makonda, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.

“Makonda ambaye jina lake halisi, ni Daudi Albert Bashite, aliongozana na watu wenye silaha za kivita. Akavamia kituo cha televisheni cha Clouds.

Akatumia nguvu kuwanyanganya wafanyakazi wake CD. Kosa la unyang’anyi adhabu yake, inafahamika kuwa ni miaka 30.

“Lakini ofisi ya DPP (Mkurugenzi wa Mashitaka) ambayo pamoja na kuwa na kazi ya kuendesha mashitaka, imepewa jukumu la kushauriana na Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) kufanya uchunguzi na kuwasilisha kesi mahakamani.”

Kubenea alihoji, “…who is Makonda (Makonda ni nani)? DPP amenyamazia makosa hayo ya kijinai yaliyotendwa naMakonda, huku serikali ikihubiri kutaka kuaminiwa.

“Makonda anakabiliwa zaidi ya mashitaka tisa ya kijinai ambayo yanaweza kuthibitishwa mahakamani, lakini mkurugenzi huyo wa mashitaka ameyamaza. Katika mazingira hayo, nani ataamini serikali. Nani ataamini serikali inayojifunika blangeti,” alihoji.

Amesema, kifungu cha 8 (a) na (b) vya makosa ya jinai, kinapiga marufuku kutishia watu na kuingia kwenye eneo la watu ukiwa na silaha.

Kifungu cha 123 cha Kanuni ya adhabu, kinakataza udanganyifu. Makonda amefanya udanganyifu wa jina, elimu na vyeti anavyotumia.

Hata hivyo, serikali imeeleza bungeni kuwa kesi dhidi ya Makonda haiwezi kufunguliwa na serikali kwa kuwa tayari Meya wa Ubungo, Boniface Jacob amefungua shauri kwenye Tume ya Maadili.

Akijibu hoja ya Kubenea, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Geoger Masaju, aliliambia Bunge kuwa “hatuwezi kufungua kesi mbili. Tayari Meya wa Ubungo, ameshafungua kesi dhidi ya Makonda. Tusubiri kesi isikilizwe na hukumu itolewe.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Samia atoa pole ajali iliyoua 25, kujeruhi 21 Arusha

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu...

Habari MchanganyikoTangulizi

25 wafariki dunia katika ajali Arusha

Spread the loveWatu 25 wamefariki dunia papo hapo mkoani Arusha katika ajali...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Biteko afuta likizo watumishi Tanesco, bosi Morogoro yamkuta

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dk. Doto...

Habari za Siasa

Mbarala ajitosa kumrithi Zitto, aahidi kuipa ushindi ACT-Wazalendo uchaguzi mkuu

Spread the loveKATIBU wa Idara ya Haki za Binadamu na Makundi Maalum...

error: Content is protected !!