July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea afungua pazia Manzese

Spread the love

MGOMBEA ubunge, jimbo la Ubungo, jijini Dar es Salaam, Saed Kubenea, amezindua kampeni yake ya kutafuta ridhaa ya wananchi, kwa mkutano mkubwa wa hadhara kwenye viwanja vya Manzese, kwa Bakhressa. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Katika mkutano huo jana, Kubenea ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hali Halisi Publishers Limited (HHPL) inayomiliki gazeti la MwanaHALISI, na kuendesha mitandao ya Mwanahalisiforum, alitumia nafasi hiyo kusihi wananchi wamchague na kutarajia maendeleo.

Kubenea ambaye pia ni mwandishi wa habari mwandamizi, alisema ameanza tu kujitambulisha, ila kwa mengi aliyonayo yanayohusu matendo maovu ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), atayaeleza kwa ufasaha mikutano ijayo.

Akitandika msingi wa mwelekeo wa kampeni yake, Kubena ametaja uovu wa viongozi wakubwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akisema atafichua matendo yao ya kifisadi dhidi ya raslimali za taifa na fedha za wananchi.

Amesema amegombea ubunge ili pamoja na mambo mengine ya kurahisisha mifumo ya maendeleo ya wananchi, kupitia mijadala bungeni, afichue maovu ya viongozi wa CCM na mawakala wao na kuibana serikali mpya baada ya uchaguzi, ichukue hatua dhidi ya waliohusika.

Ilifika zamu ya wagombea udiwani kujieleza katika mkutano huo uliohusisha viongozi wa vyama vyote vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambavyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha NCCR-Mageuzi na National League for Democratic (NLD).

Wagombea udiwani waliohudhuria ni Khalid Singano anayegombea Kata ya Kigogo, Ramadhani Kwangaya (Manzese) na Shani Khalfani Beleko (Viti Maalum), Jumanne Amiri Mbunji (Tandale). Wote wanawakilisha CUF.

Beleko amesema anataka kusimamia upatikanaji wenye ufanisi wa huduma za kinamama baada ya kushuhudia hali mbaya ikiwakabili wanawake wanaohitaji huduma ya kujifungua.

Pia anakusudia kuhangaika kuanzisha mfuko wa wa fedha za kusaidia wanawake wanaojishughulisha na miradi midogo ya kuuza matunda mitaani ili wapate kujiimarisha.

Kwangaya ambaye anatetea kiti cha udiwani Manzese, amesema moja ya shida kubwa aliyopanga kuikabili ni kujenga kituo cha afya cha kisasa ambacho kimekosekana kwa miaka yote.

Pia ataimarisha michezo mbalimbali ili kuwasaidia watoto na vijana wa Manzese njia ya kuweza kujitegemea baadaye kupitia michezo.

Amesifia ushirikiano wa UKAWA uliofanikisha kutengeneza kombora linalotumika kuiangamiza CCM.

“Sisi ni UKAWA lakini hata walio CCM ambao natumaini wapo hapa wanaotaka mabadiliko, hawakatazwi kutuunga mkono katika kutekeleza alichofanyia makosa Rais Kikwete cha kumuondoa Lowassa katika mchakato wa kugombea urais,” amesema.

“Nimekuja kuondoa kero za Kata yetu ya Manzese,” amesema.

Mbunji anayegombea Tandale amesema CCM haitekelezi wanayowaahidi wananchi na kwa hilo, wanapaswa kuwekwa kando ili waingie viongozi wanaowajibika kwa wananchi.

Amesema haifai wananchi kuendelea kugeuzwa wajinga kwa kuahidiwa uongo wakati wana shida nyingi za kimaisha, kama vile ajira kwa vijana na mitaji ya kusaidia shughuli za kipato kwa Mama Ntilie.

“Wa UKAWA tunataka wananchi wajue tofauti ya kungoza na kutawala… CCM inatawala badala ya kuongoza watu ndio maana wanajiamulia na sio kushirikisha watu,” amesema.

error: Content is protected !!