May 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea abebeshwa msalaba wa Wazanzibari

Spread the love

SAED Kubenea, mwandishi mahiri wa habari za uchunguzi nchini, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma za kuandika makala inayodaiwa kuwa ya uongo kuhusu mgogoro wa kisiasa Visiwani Zanzibar, anaandika Faki Sosi.

Kubenea ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliandika makala hiyo katika gazeti la MwanaHALISI linalochapishwa kila siku ya Jumatatu, akielezea kile alichokiita mateso wanayopata wananchi wa Zanzibar. 

Makala inayodaiwa na watawala kuwa ni ya uongo, ilibeba kichwa cha habari: “Yuko wapi atakayeiokoa Zanzibar?” Ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI, ukurasa wa 10&11 toleo Na. 349 la Julai 25 hadi 31 mwaka huu.

Mbele ya Wilbard Mashauri, Hakimu Mkazi katika mahakama hiyo, mwendesha mashitaka Dereck Mkatabanzi amedai kuwa Kubenea alitangaza habari za uongo, ambazo zingeweza kuleta hofu na taharuki kwa jamii.

Mkatabanzi amedai kuwa Kubenea alitenda kosa hilo tarehe 25 Julai, mwaka huu akiwa mtaa wa Kasaba Wilaya ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo Kubenea amekana shitaka hilo huku upande wa mashataka ukidai kuwa upelelezi umekamilika na kwamba wameiomba mahakama kupanga tarehe ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.

Kabla ya kuhairishwa kwa shauri hilo, Peter Kibatala, wakili wa upande wa utetezi, alitoa hoja za kupinga hati ya mashtaka iliyosomwa kwa mteja wake kwa madai ya kuwa ina upungufu kisheria.

Hakimu Wilbard Mashauri amemtaka Kibatala kusubiri siku ya usomwaji wa maelezo ya awali ya kesi hiyo ili kuweza kuwasilisha hoja hizo.

kubenea amedhaminiwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh. 5 milioni na shauri hilo litatajwa tena tarehe 31 Oktoba mwaka huu.

Makala aliyoandika Kubenea katika gazeti la MwanaHALISI ilieleza uonevu wa Jeshi la Polisi dhidi ya wananchi kisiwani Pemba ikiwemo, kuwawabambikiza kesi, kuwapiga na kuwatesa wananchi hao kwa madai ya kuipinga serikali iliyopo madarakani.

Kubenea aliandika makala hiyo baada ya kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Pemba kufuatilia kile alichokitaja kama “mateso, unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wananchi.”

Miongoni mwa wahanga waliozungumza na mwandishi huyo wa habari, ni Hijja Hassani aliyetangazwa kuwa ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani katika uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba, kabla ya Jecha Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta uchaguzi huo na matokeo yake.

Kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huru na haki Visiwani, ndiyo chanzo cha mgogoro wa kisiasa ulioikumba Zanzibar.

 

error: Content is protected !!