June 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kubenea abaini madudu fedha za jimbo

Spread the love

SAED Kubenea, Mbunge wa Ubungo, Dar es Salaam ameeleza kubaini kuwepo kwa ufujaji wa fedha za miradi ya maendeleo ya jimbo hilo na baadhi ya viongozi wa mitaa, anaandika Faki Sosi.

Hayo yamebainishwa jana wakati alipokuwa kwenye ziara ya kukagua na kutoa fedha za kusaidia miradi mbalimbali ya baadhi ya kata ambazo zipo kwenye jimbo hilo.

Kubenea amebaini kwamba katika kata hiyo ya Kimara zimeliwa Sh. Milioni 4, ambazo zilitolewa kipindi kilichopita hivyo kuwataka viongozi wa kata hiyo kuhakikisha waliozila wanachukuliwa hatua.

“Kikundi cha Women Group kinachojihusisha na kulea watoto yatima kitapata Sh. milioni 2, kununulia vyerehani lakini kwa wale viongozi waliotafuna Sh. Milioni 4 wachukulie hatua za kisheria,” amesema Kubenea.

Baada ya kutoka hapo ambapo ameshuhudia pia kusimama kwa ujenzi wa kituo cha polisi ambao umechangiwa na kuliwa fedha hizo zilizokuwa zimetolewa na mfuko huo.

Katika ziara hiyo, Kubenea ametembelea Kata za Makuburi ambako amekagua eneo la kujenga kisima kinachotarajiwa kugharimu kiasi cha Sh. Milioni 8.

Akiwa kata ya Mabibo mbunge huyo amekabidhi Sh. milioni 5 ikiwemo na matofali 500 ili kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Kata ya Makuburi.

Kata ya soko la Mabibo amekagua eneo ambalo linatarajiwa kuchimbwa kisima kwa matumizi ya wakazi wanaoishi jirani na wafanyabiashara wa soko hilo katika shughuli mbalimbali.

Kwa upande wa eneo la Sinza Kontena amekabidhi Sh. mil 11 kusaidia kikundi shirikishi kusaidia kuendesha miradi yao ya biashara.

Akizungumza baada ya kumaliza ziara hiyo, mbunge Kubenea amesema fedha zilizokuwa zimetengwa za mfuko wa jimbo ni Sh. milioni 41 ili zisaidie miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Baada ya kutembelea miradi hiyo, nimebaini kuwepo kwa upotefu wa fedha za serikali ambazo zilitolewa kusaidia kata kadhaa lakini nyingi hazikuwafikia walengwa,” anasema Kubenea.

Anabainisha kwamba kutokana na fedha hizo kutafunwa na baadhi ya wajanja katika siku zilizopita hivi sasa ametoa wito kwa viongozi kuhakikisha zinafanyiwa kazi kwa malengo yaliyopangwa na wale waliokula zilizopita watachukuliwa hatua za kisheria.

“Fedha ni za wananchi haiwezekani zipotee hivi hivi lazima zifahamike zimetumikaje na wale waliokula wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,”alisema Kubenea.

error: Content is protected !!