April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kuagwa Mengi: Viongozi wa dini watoa ujumbe maalum

Spread the love

VIONGOZI mbalimbali wa dini nchini, wametoa ujumbe maalum wa amani, upendo na umoja wakati wa ibada ya kuagwa Dk.  Reginald Abraham Mengi katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Wakizungumza katika ibada ya kuuaga mwili wa Marehemu Dk. Mengi leo tarehe 7 Mei 2019, viongozi hao wamehimiza serikali na wananchi kwa pamoja kuitunza amani.

Akizungumza katika ibada hiyo, Mchungaji wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Msasani, Mchungaji Kijalo amesema, maisha ya wanadamu yanapaswa kuleta furaha na amani katika maisha ya wengine.

“Dk. Mengi alikuwa hivyo, alitumia maisha yake kuleta furaha na amani kwa wengine kwa kutumia karama na mali zake kusaidia wengine. Hivyo ili kumuenzi inabidi tuishi maisha ya amani na upendo,” amesema Mchungaji Kijalo.

Aidha, Mchungaji Kijalo amewataka Watanzania kuishi maisha ya toba ili waweze kuwa karibu na Mungu.

“Inatakiwa tuombe toba tunapokosea. Tusameheane sisi kwa sisi na pale mwenzako anapokosea umsamehe usipofanya hivyo unajenga chuki na kisasi ambacho si kizuri athari zake ni kubwa,” amesema Mchungaji Kijali.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi  Mussa amesema, Marehemu Dk. Mengi alikuwa mpenda amani na mahusiano katika jamii, hivyo ili kumuenzi ni vyema Watanzania kufuata nyayo zake.

“Wamekufa watu lakini kamwe mema yao hayatakufa, lakini wako watu hai ambao ni sawa na wafu kwa kuwa hawana mema.

“Unapomzungumzia Dk. Mengi unamzungumzia mtu aliyemwema na bora katika jamii, alinufaisha wengikifikra hata kutumia fedha zake hakubagua mtu. Mema yake hayatasahaulika,” amesema Sheikh Mussa.

Baba Askofu Nelson Kisare amesema, kama Mungu angempa nafasi ya dakika moja Dk. Mengi kufufuka kwa ajili ya kutoa wosia, angehimiza Watanzania kuienzi amani.

Askofu Kisare amesema “Tunapotafakari maisha ya Mengi tunakumbuka aliyoyafanya Mungu ya kuumba nchi ya Tanzania na kuipa rasilimali nyingi kwa ajili ya wananchi, lakini aliweka changamoto na kwamba kazi ni kubadili changamoto hizo kuwa fursa na kubadili maisha ya watanzania.

“Enzi za uhai wake Dk. Mengi, alitatua changamoto zilizopo ili kuhakilisha kwamba, Watanzania wananufaika na rasilimali zao, na alifanikiwa kufanya hayo kwa kuwa kuna amani na upendo. Hivyo tifuate nyayo zake kwa kuienzi amani na kusaidia wenye uhitaji.”

Katibu Mkuu wa TEC, Father Kitima amesema, enzi za uhai wake Dk. Mengi hakuwa mbinafsi, alitumia karama na mali zake kuinua wengine sambamba na kukuza sekta binafsi kwa kuanzisha viwanda na kutoa ajira kwa Watanzania wengi. Hivyo ni busara walio hai kuuenzi na kuendeleza mchango wake.

“Kifo cha Mengi sisi kama Kanisa Katoliki kimetugusa kwa namna ya kipekee sababu alikuwa karibu na kanisa letu katika kuwatumikia Watanzania. Aliwatumikia watu wenye uhitaji maalumu, alisaidia walemavu,” amesema Father Kitima.

error: Content is protected !!