April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kuachwa wahujumu uchumi: DPP amjibu JPM

Spread the love

OMBI alilolitoa Rais John Magufuli la kuwaacha huru wahujumu uchumi iwapo watakuwa tayari kurudisha fedha, limeambatana na masharti. Anaripoti Martin Kamote…(endelea).

Biswalo Mganga, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini amesema, ofisi yake iko tayari kufanyia kazi mapendekezo ya Rais Magufuli, kuhusu watuhumiwa wa uhujumu uchumi walio tayari kuomba msamaha na kurejesha fedha.

Rais Magufuli alitoa ushauri huo tarehe 22 Septemba 2019, wakati anawaapisha viongozi mbalimbali aliowateuwa hivi karibuni, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Leo tarehe 23 Septemba 2019, DPP Mganga ametoa muongozo kwa watuhumiwa hao, namna ya kufanya ili maombi yao ya msamaha yasikilizwe na kufanyiwa kazi.

DPP Mganga amesema, wahusika wanatakiwa kuandika barua yenye maudhui ya kutubu na kuifikisha kwa mkuu wa gereza alilopo, kwa ajili ya kufikishwa katika ofisi yake.

“Utaratibu ni kwamba, mtuhumiwa aliyeko mahabusu anatakiwa kuandika barua kupitia mkuu wa gereza,  akikiri kosa na kuomba kutubu haraka iwezekanavyo, na sisi tutachukua hatua,” amesema DPP Mganga.

Aidha, DPP Mganga ametoa sharti lingine, kwamba watuhumiwa hao wanatakiwa kuandika barua hizo wenyewe, na si kutumia mawakili kwa ajili ya kuepusha mgongano wa kisheria.

“Ni mtuhumiwa mwenyewe ndiye anatakiwa kuandika barua na sio wakili, unajua wakili anaweza kubadilika na hata mtuhumiwa kumkana kuwa sijamtuma kufanya kwa niaba yangu. Ndio maana mara zote watuhumiwa wanaoomba msamaha na kukiri, wanaandika barua kwa mkono wao na kumpa mkuu wa gereza,” ameeleza DPP Mganga.

Miongoni mwa watuhumiwa watakaoguswa na masharti hayo ni pamoja na Mkurugenzi wa VIP Engineering, James Rugemalira na Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Harbinder Sing Sethi.

Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi ikiwemo kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22 milioni.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo mwaka 2013 ambapo walikamatwa na kupandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza mwaka 2017.

error: Content is protected !!