Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kuachwa huru kwa Mbowe: Askofu Mwamakula amtega Rais Samia
Habari za Siasa

Kuachwa huru kwa Mbowe: Askofu Mwamakula amtega Rais Samia

Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki, Emmaus Mwamakula
Spread the love

 

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Moravian Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki, Emmaus Mwamakula, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, aruhusu mchakato wa upatikanaji katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, ili azidi kuijengea heshima yake kwa Taifa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kiongozi huyo wa dini ametoa wito huo leo Ijumaa, tarehe 4 Machi 2022, jijini Dar es Salaam, akizungumzia hatua ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, kumuondolea mashtaka ya ugaidi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake.

Askofu Mwamakula amesema kuwa, kitendo cha  kufutwa kwa kesi iliyokuwa inamkabili Mbowe katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, kimemjengea heshima Rais Samia.

“Kufutwa kwa kesi  hii iwe mwanzo wa kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Sababu Rais  Samia amejijengea heshima kwa tukio lile,  heshima yake itakuwa endelevu na ya maana endapo ataongoza kupatikana kwa tume huru  na katiba mpya,” amesema Askofu   Mwamakula.

Askofu Mwamakula amesema “huu ukawe mwanzo wa uhuru wa kujieleza,  tusitegemee mambo mengine ya kukamata kamata.”

Askofu Mwamakula amewaomba Watanzania na wananchama wa Chadema, watibu majeraha yao na washikamane kwa ajili ya kuijenga nchi.

“Niwaombe Watanzania hasa Wanachadema, mmeumia sana lakini furaha yenu iachilie  pia maumivu na chuki, tusonge mbele tushikamane kama nchi,” amesema Askofu Mwamakula.

Akizungumzia kesi hiyo, Askofu Mwamakula amesema “Rais Samia  tuliweza kumwambia pasipo kusita kwamba aelekeze Ofisi ya DPP kufuta mashtaka ya Mbowe bila masharti yoyote, kesi ilikuwa inachafua Tanzania, inamchafua yeye kama Rais.”

Mbowe na wenzake watatu, waliokuwa makomando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya, walikuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021.

Kesi hiyo ilikuwa na mashtaka matano ya ugaidi, ikiwemo kula njama za kutaka kudhuru viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro,  Lengai Ole Sabaya.

Mashtaka mengine ni, kupanga kulipua vituo vya mafuta na maeneo yenye mikusanyiko ya watu,  kushiriki vikao vya kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi na kupanga maandamano yasiyo na kikomo.

Shtaka lingine lilikuwa la kukutwa na silaha aina ya bastola,  kinyume cha sheria, lililokuwa linamkabili mshtakiwa  wa pili, Kasekwa na shtaka la kutoa kiasi cha fedha Sh. 699,000, kwa ajili ya kufadhili vitendo vya ugaidi lililokuwa linamkabili Mbowe.

Mbowe na wenzake walidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Mei na Agosti 2020, kwenye maeneo ya mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Morogoro, lengo likidaiwa kutia hofu  wananchi na kuionesha Serikali imeshindwa.

DPP Mwakitalu, kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, aliwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka hayo, kisha mahakama hiyo mbele ya Jaji Joachim Tiganga ikaifuta kesi  na kuwaacha huru washtakiwa.

Hati hiyo iliwasilishwa wakati Mbowe na wenzake wakijiandaa kuanza kujitetea, baada ya mahakama hiyo kuwakuta wana kesi ya kujibu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!