December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Krisimasi yaweza kuwa mwarobaini wa  uhasama wa kidini?

Spread the love

KILA mwaka, siku kama ya leo – tarehe 25 Desemba – Wakristo duniani kote, huungana kusheherekea sikukuu ya Krisimasi. Anaandika Mwanadishi Maalum … (endelea).

Ni siku maalum inayoelezwa na waamini wa dini hiyo, kwamba ni sherehe ya kuzaliwa kwa Yesu, nabii mkuu katika dini za Kikristo.

Hata hivyo kuna mataifa mengine sikukuu hii haitambuliki kabisa au inatambulika kwa kidogo sana.

Miongoni mwa mataifa ambayo Krismasi haitambuliwi kama sikukuu rasmi, ni mataifa ya Kiislamu. Mfano ni nchini Uturuki, tarehe 25 Desemba, huwa siku tu ya kawaida kwenye kalenda.

Wala sikukuu hii haipo kwenye kalenda za Kiyahudi, Kihindi au Kiislamu.

Miongoni mwa Waislamu, ukuu wa sikukuu ya Krismasi unakaribiana tu pengine na sikukuu za Eid ambao ndio wakati Waislamu hukutana, hualikana, hupika, hutembeleana, hutoa sadaka, huvaa wakapendeza na huenda msikitini kwa ibada.

Kufahamu tofauti hizi ni muhimu sana, usije kumtakia Mwislamu Heri ya Sikukuu ya Krismasi.

Lakini si kwamba Yesu hatambuliwi kwenye dini ya Kiislamu. La hasha!

Issa Mwana-Mariam (Jesus au Yesu), ametajwa kwenye Qurani tukufu; kila mwaka Waislamu husherehekei siku ya kuzaliwa kwa Yesu, lakini humuenzi.

Waislamu huonyesha heshima kuu kwa nabii huyu na humtambua kama sehemu muhimu ya imani yao.

Ndani ya kitabu hicho kikuu cha waislamu, kumeelezwa utukufu wa Issa na utume wake.

Koran humchukulia Yesu kama mmoja wa manabii wa kuheshimiwa sana waliomtangulia Mtume Muhammad (S.A.W- Sallā Allāhu ʿalayhi Wa-sallam).

Yesu kwa Kiarabu hufahamika kama Issa, na ametajwa mara nyingi sana kwenye Koran, hutajwa sana hata kumshinda Muhammad kwenye Koran.

Isitoshe, yupo mwanamke mmoja pekee aliyetajwa kwa jina kwenye kitabu hicho kitukufu cha dini ya Kiislamu. Huyo siyo mweingine, bali ni Maryam (Mary).

Mwanamke huyo, Bikira Maria, ambaye kwa Kiarabu hujulikana kama Maryam, ameangazia kwenye sura zima kwenye Koran, ambapo inasimuliwa kuhusu alivyomzaa mtoto akiwa bikira.

Lakini simulizi ya kuzaliwa kwa Yesu kwenye Uislamu haijamtaja Yusufu popote, wala wale manajimu kutoka Mashariki, wala kulazwa kwenye hori ya kuwalishia ng’ombe.

Maria anajifungua akiwa peke yake jangwani, akiwa amejikinga chini ya mtende uliokauka.

Mwujiza unatokea na tende zilizoiva zinaanguka kutoka kwenye mtende huo na kuwa chakula chake.

Aidha, mto wenye maji safi unachipuka kutoka miguuni mwake na kumpa maji.

Hadithi ya Maria na kujifungua kwake akiwa bikira inafahamika sana. Mwanamke ambaye hajaolewa kujifungua ni kisa ambacho kinazua maswali mengi sana kuhusu maadili yake.

Lakini mtoto huyo – Yesu/Issa – anapozaliwa, anaanza kuzungumza kama nabii wa Mungu. Mwujiza huo unamuondolea doa mamake. Ni hadithi ya ushindi dhidi ya ubaguzi na hukumu.

Waislamu wanapomrejelea Yesu, huwa wanatakiwa kutamka A.W. (ʿalayhi Wa-sallam), kwa maana ya Amani Iwe Naye, sawa na wafanyavyo kwa Mtume Muhammad na manabii wengine.

Ndani ya kitabu kitukufu cha Qurani na hata Torati – kitabu cha Nabii Mussa na ambacho Waislamu wanakiamini na kukiona sehemu ya Qurani takatifu – kumebashiriwa kuwa anayetarajiwa kurejea duniani kabla ya kusimama Kiyama na kurejesha haki duniani, ni Issa Mwana-Mariam. Ni Yesu.

Huo utakuwa ndio ujio wake wa pili, na kutukuzwa kwake katika vitabu vya Kiislamu sio tu katika Koran.

Mwanafalsafa wa Kisufi Al-Ghazali anamweleza kama “nabii wa nyoyo.”

Ibn Arabi anaandika kumhusu yeye kuwa “muhuri wa watakatifu.”

Katika nchi nyingi za Kiislamu, kuna wavulana wanaopewa jina Issa (Yesu) na wasichana wanaoitwa Maryam, kutokana na Maria au Mary. Hilo halina shida kwa Waislamu.

Lakini swali la kujiuliza: Unaweza kuona mtu kutoka familia ya Kikristo akimbatiza mtoto wake jina Muhammad?

Dini ya Kiislamu inamfahamu vyema Yesu, kwa sababu kufikia wakati wa kuwa dini katika karne ya 7, dini ya Kikristo ilikuwa tayari imekita mizizi Mashariki ya Kati.

Ingawa dini ya Kiislamu humuenzi Yesu, katika karne za baadaye, ni kweli kwamba dini ya Kikristo haikuwa inarejesha fadhila hizo.

Kufahamu kuhusu Yesu na Uislamu, pamoja na kufahamu umuhimu wake katika dini hiyo kwa sasa kunaweza kuwasaidia Waislamu na Wakristo kutafuta maridhiano. Kunaweza kusaidia kumaliza uhasama uliopo.

error: Content is protected !!