October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kosa la Mwigulu ni nini?

Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango

Spread the love

 

KWA wanaofahamu jinsi serikali inavyofanya kazi, wanaofahamu kutungwa kwa muswada, kufikishwa kwa mswada huo bungeni na hadi kuwa sheria, hakuna shaka kuwa watakubaliana na mimi katika swali hili. Kwamba, “Kosa la Mwigulu, ni lipi?” Anaripoti Mwandishi Maalum … (endelea).

Kwamba, utaratibu wa kupeleka hoja kwenye Baraza la Mawaziri, unaanzia mbali kidogo. Hoja inaanzia kwa wataalam wa wizara chini ya Katibu Mkuu na wakurugenzi wake. Baada ya kuchambua na kujiridhisha na kile wanachokipendekeza, huwasilisha jambo hilo kwa waziri.

Kazi ya waziri, ni kulifikisha wazo hilo kwenye Baraza la Mawaziri, kupitia kitu kinachoitwa, “Cabinet Paper.” Mkutano wa Baraza la Mawaziri unaongozwa na Rais.

Wazo hilo la wataalam wa wizara likishafikishwa kwenye Baraza na iwapo libakubaliwa, linaondoka kwenye mikono ya wizara na kupelekwa kwa Kamati ya Makatibu wakuu wa wizara – Inter Ministerial Technical Committee (IMTC).

Kamati hii, hulichakata wazo lililoletwa na wakishajiridhisha wanalirudisha kwenye Baraza chini ya Katibu Mkuu Kiongozi.

Nalo Baraza likiona liko vizuri, maelekezo yanatolewa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kuandika muswada kulingana na maelekezo au mtazamo wa Kamati ya Wataalam ya makatibu wakuu kama ilivyopata baraka za Baraza la Mawaziri chini ya Mheshimiwa Rais.

Kwa muktadha wa sakata la tozo, wote ni mashahidi kuwa wazo lilianzia kwa aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Yustino Ndugai. Alilitaka Bunge kuagiza serikali kuandaa muswada kwa ajili ya tozo za miamala ya simu na benki.

Katika mazingira hayo, ni serikali gani duniani itakwenda kinyume na maelekezo ya Bunge, tena ambayo yametolewa na Spika mwenyewe?

Katika suala zima la tozo, Serikali inaweza kusamehewa katika lawama na badala yake Ndugai na Bunge lake, ndiyo inauyopaswa kuwajibishwa.

Hii ni kwa kuwa Ndugai alikuwa na ajenda binafsi na jambo hili, hasa juu ya mkopo wa Sh. 1.3 trilioni ambazo serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ilikopa kutoka mashirika ya fedha ya kimataifa.

Job Ndugai

Ndugai alilenga kuonyesha umma, kuwa Rais Samia anaingiza nchi kwenye mikopo isiyokuwa na tija na hivyo, msimamo wake wa kuleta tozo, umelenga kuwaondolewa wananchi mzigo wa madeni. Kwamba, taifa hili, linaweza kujiendesha bila mikopo au misaada kutoka nje.

Kwa ufupi, alikuwa amejitosa rasmi kwenye mbio za urais 2025. Ndio msingi wa maneno yake, kwamba “ikifika 2025, wananchi wataamua wenyewe, wachague wanaotaka kuendesha nchi kwa mikopo au wanaoweza kuendesha nchi kwa mapato ya ndani.”

Hivyo basi, kwa kuwa tumeonesha jinsi mchakato wa sheria unapoanzia; shinikizo la Bunge lilivyokuwa kubwa katika sakata hili, unaweza kuona dhahiri kwamba kumlaumu Mwigulu, ni kutaka kumtoa kafara.

Kutaka Bunge kukaa pembeni na kulitupia suala hili lote mikononi mwa Mwigulu, ni kutaka kumuonea. Hii si haki!

Hakuna asiyefahamu jinsi Rais Samia anavyoheshimu demokrasia shirikishi, tangu akiwa waziri katika serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Waliokuwapo bungeni wakati huo, wanaweza kuwa mashahidi wa hili.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Elieza Feleshi

Kwamba, Rais Samia – wakati huo, akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), alikuwa anashirikisha hata wapinzani wake wa kisiasa, kwenye mambo yanayohusu maslahi ya umma.

Kwa mwenendo wake huo, Rais hakuzuia wabunge wa chama chake, kuchangia mjadala huu wa tozo kwa uwazi ndani ya Bunge. Hakuzuia maoni ya wabunge wake wala kuwalazimisha kupitisha hoja hiyo. Kila mbunge alikuwa huru kuchangia na kutoa maoni yake.

Kile ambacho kinaonekana sasa, ni hatua ya baadhi ya wabunge – wakiwamo wale waliounga mkono hoja ya Ndugai kuhusu tozo – kutaka kujiweka kando na sakata hili. Hili haliwezi kukubarika.

Yaani mtu amekuwa mbunge au waziri, ameliona jambo hili likipitishwa kote huko na yeye akiwamo, lakini hukulipinga wala kutoa maoni mbadala, kisha leo anataka kuwa wa kwanza kuonekana mtetezi wa wananchi, hili haliwezi kunyamaziwa.

Kuna taarifa zisizo na mashaka kwamba baadhi ya watu wanaokosoa tozo hizo hadharani au kuwatumia baadhi ya wananchi, wanafanya hivyo, kwa maslahi yao binafsi.

Hii ni kwa sababu, baadhi ya wanaopinga tozo sasa, walikuwa na nafasi ya kufanya hivyo ndani ya Bunge. Yawezekana hawakuweza kunyanyua mdomo kwa kuwa walimuhofia Ndugai. Kama madai hayo ni kweli, basi watakuwa wamepoteza sifa ya kuwa viongozi wa umma.

Hauwezi kuwa kiongozi wa umma, kisha ukawa mwoga wa kutetea maslahi ya wananchi au chama chako.

Wengine waliopo kwenye mradi huu, wameshiriki vikao vya Baraza la Mawaziri, ambako hoja hii ilipelekwa baada ya maelekezo ya Bunge la Ndugai. Hawakusema huko, hawakusema bungeni wala hawakusema kwenye vikao vya chama.

Kushindwa kujadili athari za tozo kwenye Baraza la Mawaziri, bungeni au kwenye kikao cha chama, ni hujuma dhidi ya Rais Samia na serikali anayoingoza.

Kwa muktadha huo, zigo hili, haliwezi kuachwa linasukumizwa kwa mtu mmoja – Mwigulu Lameck Nchemba – kwa baadhi ya watu kutaka kukimbia dhana ya uwajibikaji wa pamoja.

Kuendelea kumsakama Mwigulu kwenye hili, kunaweza kuthibitisha madai ya baadhi ya watu, kwamba kinachotafutwa hapa siyo tozo. ni Mwigulu.

Kwamba, watu wameona walitumie jambo hili, kummalizia kisiasa, lengo hasa likiwa uchaguzi mkuu wa 2030 (urais) na ule wa mwaka 2025, hasa kwenye wadhifa wa uwaziri mkuu.

Kwamba, kwa kutumia tozo, kutengenezwe mkakati wa kumpoteza yule anayeweza kuonekana kuwa mshindani wa kundi fulani.

Na huu ndio utaratibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nani asiyejua kuwa Edward Lowassa, alisukiwa zengwe katika sakata la Richmond kwa sababu ya urais na uwaziri mkuu?

Nani asiyejua kuwa Hans Kitine, aliyekuwa waziri wa utawala Bora, katika serikali ya Benjamin Mkapa, alisulubiwa kwa sababu ya mbio za urais?

Kitine – mkurugenzi wa zamani wa usalama wa taifa (TISS) na baadaye mbunge wa Makete – alituhumiwa kujinufaisha binafsi katika matibabu ya mkewe nchini Canada.

Aliyeibua sakata hilo bungeni, akatoa nyaraka na kuaminisha umma kuwa waziri huyo, ametumia madaraka yake vibaya, haikuwa muda alijitambulisha rasmi kuwa yuko upande gani kwenye mbio za kumrithi Mkapa.

Hata kilichompata Iddi Simba, mmoja wa wanasiasa mashuhuri na waziri mwenye nguvu katika serikali ya Mkapa, aliyelazimishwa kujiuzulu katika kilichoitwa, “kashifa ya sukari,” ilikuwa ni mbio za urais za mwaka 2005.

Shamsi Vuai Nahodha, aliyepata kuwa waziri Kiongozi wa Zanzibar na baadaye akateuliwa na Kikwete kuwa waziri wa mambo ya ndani, anaweza kuingizwa kwenye orodha ya walioathirika na mbio za urais.

Ni baada ya wabunge kumshikia bango ajiuzulu, kufuatia ripoti ya Kamati Teule ya Bunge juu ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza, kuwataja maofisa wa polisi kutenda uhalifu.

Lakini ndani ya mioyo ya wasuka mkakati, hoja haikuwa Tokomeza. Bali, ni mbio za urais wa Zanzibar mwaka 2020. Vuai na wenzake watatu – Balozi Khamis Sued Kagasheki, Emmanuel Nchimbi na Mathayo David – walilazimishwa kujiuzulu 20 Desemba 2013.

Kwa muktadha huu, kinachotengenezwa dhidi ya Mwigulu sasa kupitia tozo, ni mwendelezo uleule wa kutengenezeana kile ambacho Kikwete alikiita kwa Lowassa, “ajali ya kisiasa.” Kwamba, anayetafutwa hapa ni mtu, sio tozo. Tusidanganyane.

Soma Makala hii pia kwenye gazeti la Raia Mwema la leo Jumatano

error: Content is protected !!