September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kortini kwa kutafuna fedha Manispaa ya Kinondoni

Spread the love

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Kinondoni imewapandisha kizimbani watu wawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, wakikabiliwa na makosa matano ikiwemo ubadhirifu wa fedha umma, anaandikaFaki Sosi.

Massana Machali (41) na Athumani Mtono (34), wanatuhumiwa ‘kuchota’ fedha za serikali na kuzitumia kwa matumizi binafsi Novemba mwaka 2013 na Oktoba mwaka jana, jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Vera Ndeoya, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, mbele ya Hakimu Is – Haq Kuppa, amedai kwamba watuhumiwa hao walitenda makosa hayo katika Wilaya ya Kinondoni.

Katika shitaka la kwanza, Vera amedai kwamba Oktoba 27, mwaka huu wakiwa waajiriwa wa Manispaa hiyo, walitoa fedha 3,500,000/- (milioni tatu na nusu), kutoka katika akaunti ya benki ya DCB nambari 031012000304 yenye jina la “Kamati ya Maendeleo Kata ya Saranga.”

Katika shitaka la pili, Vera amedai kuwa, tarehe 20 Novemba, mwaka 2013 watuhumiwa hao wakiwa katika ofisi za Kata ya Saranga, waliweka saini katika hundi namba 042980 iliyokuwa na jina la “Akaunti ya Maendeleo ya Saranga.”

Watuhumiwa hao pia, wanakabiliwa na tuhuma za ubadhirifu na ufujaji wa fedha za umma ambapo katika maelezo ya kosa hilo, wanadaiwa kujipatia fedha kiasi cha Sh. 3,500,000/- baada ya kutia sahihi katika hundi namba 042980.

Hata hivyo, watuhumiwa hao wamekana mashtaka hayo huku mwanasheria wa serikali akidai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea.

Hakimu Kuppa amesema, tuhuma zinazowakabili watu hao zinadhaminika kisheria na hivyo kuwataka watuhumiwa kuwa na wadhamini wawili ambao kwa kila mmoja ataweka saini ya bondi ya Sh. 2 Milioni.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 12, mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza hoja za awali.

error: Content is protected !!