July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Korosho zote Mtwara zanunuliwa na kusafirishwa nje

Meli ambayo imebeba shehena za korosho ikiwa bandarini Mtwara tayari kwa kusafirishwa nje ya nchi

Spread the love

 

HATIMAYE leo tarehe 22 Juni, 2022 meli ya mwisho kupitia kampuni ya Sibatanza ya nchini Vietnam imeng’oa nanga katika Bandari ya Mtwara na kusafirisha korosho tani 15,800 zilizokuwa zimesalia katika mavuno ya msimu uliopita nchini. Awali kampuni hiyo ilinunua tani 80,000 za korosho katika msimu huo. Anaripoti Gabriel Mushi, Mtwara … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Mtwara, Mwenyekiti Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Brig. Jenerali Mstaafu Aloyce Damian Mwanjile amesema kuondoka kwa meli hiyo kumeiongezea nafasi bandari ya Mtwara kujiandaa kwa makusanyo ya msimu ujao wa mwaka 2022/2023.

Pia amesema kununuliwa kwa korosho hizo, kumedhibitishia kwamba korosho za Tanzania bado zinauzika hivyo kuifanya Bodi hiyo kuendelea kuweka msisitizo kwa ajili ya zao hilo ambalo mavuno yanatarajiwa kuongezeka katika msimu unaofuata 2022/2023.

“Msimu huu wa 2022/2023 tunatarajia kuzalishaji tani 400,000 za korosho nchi nzima kama lengo la wizara ya Kilimo lilivyowekwa, mwaka jana tulizalisha tani 240,000.

“Zamani ilikuwa mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Tanga na Pwani ndiyo inayozalisha korosho kama mikoa asilia lakini sasa jumla ya mikoa 18 inalima korosho,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho, Francis Alfred amesema jukumu la Bodi hiyo ni kufungamanisha uchumi wa korosho na sekta nyingine.

“Sasa tunakwenda kuchagiza uchumi wa nchi kupitia bandari. Bandari ya Mtwara inapopata meli nyingi inakuza uchumi kupitia shughuli za kijamii na kuongeza mapato.

“Mwaka jana tulipata ruzuku ya lita za maji za viuatilifu milioni 1.4, sulphur tani 13,000 na kuongeza uzalishaji kutoka tani 210,000 mpaka tani 240,000 ikiwa ni ongezeko la asilimia 14. Ongezeko hilo limeongeza mapato kwenda kwa wakulima kutoka Sh bilioni 478 hadi 498 mwaka huu,” amesema Mkurugenzi huyo.

Amesema zao la korosho lina mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa lina faida mara mbili iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake.

“Kikubwa naomba ushirikiano kwa wadau wote ili tufikie lengo la kuchangia mapato kutoka Sh bilioni 500 hadi Sh trilioni moja kwa mwaka,” amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania, Brig. Jeneral Mstaafu, Aloyce Damian

Aidha, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari mkoani Mtwara, Norbert Kalembwe amesema baada ya meli hiyo ya mwisho kuondoka, sasa wanategemea kuwasili kwa meli nyingine ya viuatilifu kwa ajili ya korosho.

“Ujio wa meli hizi unatuwezesha kuboresha uchumi wa mkulima na bandari kwa ujumla kwani hata maisha ya mtu mmoja mmoja yanaboreshwa,” amesema.

Amesema mafanikio hayo yanatokana pia na upanuzi wa gati katika bandari hiyo ambao ulikamilika Disemba 2020.

Amesema ujezi huo uliogharimu Sh bilioni 157.8, umewezesha bandari ya Mtwara sasa kuhudumia tani milioni moja kwa mwaka kutoka tani 400,000 za awali.

error: Content is protected !!