KIKAO cha 14 cha Bunge la Jamhuri kimeanza leo tarehe 29 Januari 2019 ambapo pamoja na shughuli zingine, wabunge wameuliza maswali mbalimbali. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Maftaha Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF) amesema, serikali haisemi ukweli juu ya ununuzi wa Korosho kwa kuwa, sasa hivi kuna usumbufu mkubwa na wakulima hawajalipwa.
Nachuma ametoa kauli hiyo leo tarehe 29 Januari 2019 bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kwa kuitaka serikali ieleze ni kwanini imekuwa ikisababisha hasara kwa wakulima wa Korosho kwa kutonunua Korosho hiyo kwa muda wa miezi mtatu sasa.
Nape Mnauye, Mbunge wa Mtama (CCM) alitaka kujua ni hatua gani ambazo zimechukuliwa na serikali kutokana na kauli ya Kasim Majaliwa, Waziri Mkuu kuwa, ununuzi wa Korosho umeghubikwa na vitendo vya rushwa.
Awali katika swali la msingi la Nachuma, kama serikali ipo tayari kuondoa changamoto ya uuzaji wa wake kwa wakulima ili kuweza kuongeza tija.
Akijibu maswali hayo Omari Mgumba, Naibu Waziri wa Kilimo amesema kuwa mpaka sasa wafanyakazi wanne wamekamatwa pia baadhi ya watumishi wa TAMISEMI wanaohusika na vitendo vya rushwa ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo Mgumba amesema kuwa, changamoto zilizopo ni pamoja na kuyumba kwa bei ya Korosho katika Soko la Dunia kutokana na kuuzwa ikiwa ghafi bila kuongezewa thamani.
Pia serikali imesema kuwa, katika mwaka 2017 na 18 imewafikisha mahakamani waajiri tisa kutokana na kukiukwa kwa utaratibu na sheria za ajira.
Hayo yalielezwa leo tarehe 29 Januari 2019 bungeni na Anthony Mavunde, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Hadija Nasri, Mbunge wa Viti Maalum (CCM).
Mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mikakati gani ya kulinda wafanyakazi kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi juu ya waajiri kwa kutozingatia sheria ya ajira.
Akijibu swali hilo Mavunde amesema, serikali inaendelea kusimamia sheria ya ajira Na.6 ya mwaka 2004 na sheria Na.7 ya mwaka 2004.
Gimbi Masaba, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) ameitaka serikali ni kwanini imekuwa ikiruhusu uingizwaji wa dawa ya pambana ambayo haiuwi wadudu.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni Gimbi alihoji, ni kwa sababu gani serikali imekuwa haipeleki pembejeo za kilimo hususani kwa wakulima wa pamba pamoja na kuchelewa kupeleka dawa ya kuua wadudu na hata inayopelekea, haiuwi wadudu?
Akijibu maswali hayo Inosent Bashungwa, Naibu Waziri wa Kilimo amesema kuwa, siyo kweli kuwa dawa zinazopelekwa kwa wakulima wa pamba haziuwi wadudu.
Amesema kuwa, serikali haiwapangii wakulima bei ya kuuza pamba bali huratibu upatikanaji wa bei nzuri ya pamba kwa wakulima.
“Sheria ya Pamba Na 2 ya mwaka 2001 inaipa serikali kupitia Bodi ya Pamba jukumu la kukaa na wawakilishi wa wakulima na kampuni za kununua pamba kukubaliana bei elekezi ambayo inazingatia gharama za uzalishaji.
“Kwa wastani gharama za uzalishaji wa ekari ya pamba inakadiliwa kuwa sh.488,000,ekari iliyotunzwa vizuri hutoa wastani wa kilo 1000 sawa na kuzalisha kilo moja kwa shilingi 488 alisema Bashungwa.
Leave a comment