HALI ya kutoaminiana kati ya mataifa mawili yenye historia moja na watu wanaofanana – Korea Kaskazini na Kusini – inazidi kuongeza wasiwasi, sasa wamekata mawasiliano yote. Unaripoti mtandao wa BBC … (endelea).
Korea Kaskazini imeeleza, imekata mawasiliano yake yote na Korea Kusini saa 6 mchana ya leo Jumanne tarehe 9 Juni 2020, ikiwemo mawasiliano ya simu, kijeshi na mipaka ukiwemo wa Kaesong.
Korea Kaskazini imeeleza, hii ni hatua yake ya kwanza dhidi ya taifa hilo la Kusini kwa madai, haliaminiki na limekuwa likiendeleza uadui wake kwao.
Licha ya mataifa hayo mawili kukutana mwaka 2018 ili kupunguza wasiwasi wa usalama miongoni mwao, bado hali ya kuviziana, kutoaminiana na kukomoana vimeendelea kushihudiwa.
Korea Kaskazini na Kusini zipo kwenye vita mpaka sasa kwa kuwa, hakuna makubaliano ya amani yaliyofikiwa na kufanikiwa tangu kumalizika kwa vita yao 1953.
Mamlaka ya Korea Kaskazini imeeleza, “Tunakata mawasiliano na kufunga miunganiko yote ya mawasiliano katika mamlaka hizi mbili kuanzia saa 6 mchana tarehe 9 Juni 2020.”
Jana Jumanne, Mamlaka ya Korea Kusini ilieleza, kwa mara ya kwanza katika miezi 21 iliyopita, taifa hilo lilipigia simu mamlaka ya Korea Kaskazini saa tatu asubuhi na saa 11 jioni lakini haikujibiwa.
“Tumefikia uamuzi kwamba, hakuna sababu ya kukaa pamoja na mamlaka ya Korea Kusini na hakuna sababu ya kujadiliana nao chochote,” imeeleza mamlaka ya Korea Kaskazini bila kufafanua zaidi.
Wiki iliyopita, Kim Yo-jong, dada wa kiongozi wa Korea Kaskazini alitishia kufunga ofisi zote za Korea Kusini na kuitaka mamlaka ya nchi hiyo kuacha kutuma watu kulipekua taifa lao.
Alisema, hatua inayochukuliwa na Korea Kusini kuifuatilia na kuipekua Korea Kaskazini inavunja makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2018, mjini Panmunjom kati ya Rais Moon Jae-in (Kusini) na Kim Jong-un (Kaskazini).
Leave a comment