JESHI la Polisi mkoani Mwanza, limezingira Ukumbi wa Tourist Hotel, ambao Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( Chadema), kilipanga kufanya kongamano lake la kudai katiba mpya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano, tarehe 21 Julai 2021 na Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema, akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu.
Mrema amedai kwamba, Askari Polisi wakiwa na magari ya maji ya washawasha wamezingira barabara kuelekea ukumbi huo.
“Polisi wamefunga barabara zote wilayani Nyamagana, eneo la ukumbi wa Tourist ulioko barabara ya Bwiru . Wanaweka magari ya maji ya washawasha katika barabara za Mwanza hakuna watu kupita, kuna Polisi zaidi ya 400 wamezingira maeneo ya ukumbi wote,” amedai Mrema.
Naye Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami, amedai kwamba, Polisi hao wamewapiga marufuku wasikanyage katika ukumbi huo.
Amesema kwa sasa baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema, wako katika ofisi za chama hicho Kanda ya Victoria, jijini humo.
“Wamepiga marufuku mtu yeyote kufika eneo la tukio, sisi kwa sasa tuko katika ofisi ya Kanda ya Victoria. Wametukaza kwa kisingizo kwamba wanadhibiti ugonjwa unaosababishwa Virusi vya Corona, Covid-19,” amedai Mnyawami.

MwanaHALISI Online imemtafuta kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng’anzi, kwa ajili ya ufafanuzi wa tukio hilo, lakini hakutoa ushirikiano kwani kila alipopigiwa simu, alikuwa anakata.
Na hata alivyotumiwa ujumbe ufupi kuhusu suala hilo hakujibu.
Hatua hiyo ya Polisi kuzingira ukumbi huo imelenga kuzuia kongamano hilo kufanyika, ikiwa ni maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel, ya kuzuia mikusanyiko kwa maelezo ya kudhibiti Covid-19.
Mbali na Polisi kuzingira ukumbi huo, limemkamata Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, usiku wa kuamkia leo pamoja na wanachama kadhaa wa chama hicho.
Pia, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Pambalu naye ni miongoni mwa waliokamatwa.
Kongamano hilo liliandaliwa na Bavicha, ambapo limeshazuiwa mara mbili kufanyika. Mara ya kwanza lilipangwa kufanyika tarehe 17 Julai 2021, lakini Jeshi la Polisi lilizuia kwa madai ya kukosa kibali.
Mara ya pili lilipangwa kufanyika leo, lakini limezuiwa kwa maelekezo ya Gabriel.
Leave a comment