Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kongamano kudai katiba lamponza Mbowe, Polisi wafukua makosa yake
Habari za SiasaTangulizi

Kongamano kudai katiba lamponza Mbowe, Polisi wafukua makosa yake

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, aliyekamatwa jijini Mwanza alfajiri ya jana, anahojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za makosa ya jinai. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mbowe na wenzake 14, walikamatwa jijini Mwanza jana tarehe 21 Julai 2021, kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko isiyo halali na uhalifu, baada ya kuandaa kongamano la kudai katiba mpya, lililopangwa kufanyika jijini humo.

Akizungumza na wanahabari mapema leo tarehe 22 Julai 2021, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mwanza, Ramadhan Ng’azi, amesema jana walimsafirisha Mbowe kuelekea jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu tuhuma za makosa ya jinai zinazomkabili.

Kamanda Ng’azi amesema, waliamua kumpeleka Mbowe Dar es Salaam, baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya mkoa huo, kumhitaji kwa ajili ya mahojiano kuhusu makosa anayodaiwa kufanya akiwa mkoani humo.

“Mbowe alikamatwa na Jeshi la Polisi Mwanza na wakati tunaendelea kumhoji ile alfajiri, wenzetu wa Dar es Salaam walikuwa wanamhitaji kwa makosa mengine. Ile asubuhi saa 1 . 30 tulimsafirisha kwenda huko, ambako ana makosa mengine ya jinai,” amesema Kamanda Ng’azi.

Kamanda Ng’azi amesema kuwa, baada ya Mbowe kumaliza mahojiano na Jeshi la Polisi la kanda hiyo, atarudishwa Mwanza, kwa ajili ya kuunganishwa na watuhumiwa wengine waliokamatwa jijini humo, kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko isiyo halali.

“Baada ya mahojiano hayo ya makosa ya jinai Dar es Salaam , nimewasiliana na kamanda wa kanda maalumu atamrudisha Mwanza, kuungana na wenzake katika kesi inayomkabili,” amesema Kamanda Ng’azi na kuongeza:

“Sasa hivi yuko kwenye mahojiano ya makosa ambayo yalikuwa yakimkabili siku za nyuma.”

Mbali na Mbowe, wengine waliokamatwa katika sakata hilo, ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema Taifa, John Pambalu. John Heche na Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Azaveli Lwaitama.

John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema

Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu, Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema, amesema Mbowe ameanza kuhojiwa asubuhi ya leo, katika Kituo cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

“Mpaka sasa ndiyo ameanza kuhojiwa kama dakika 10 zilizopita, baada ya muda tutajua wanamhoji kwa tuhuma zipi. Taarifa tumezipata jana kwamba wanafikiria kumpa kesi isiyo kuwa na dhamana,” amesema Mrema.

Mrema amesema, wafuasi wengine wa Chadema waliokamatwa pamoja na Mbowe, bado wanashikiliwa jijini Mwanza, kwa mahojiano.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Bavicha, lilizuiwa kufanyika kwa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel, aliyepiga marufuku mikusanyiko, ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na Virusi vya Corona (Covid-19).

Gabriel alitoa marufuku ya mikusanyiko tarehe 20 Julai 2021, siku moja kabla ya kongamano hilo kufanyika.

Kongamano hilo limeahirishwa kwa mara ya pili, baada ya kuzuiwa mara ya kwanza tarehe 17 Julai 2021, kufuatia kukosa kibali cha Jeshi la Polisi mkoani Mwanza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

Habari za Siasa

CCM yakemea ufisadi, yaipa kibarua TAKUKURU

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekemea vitendo vya ubadhirifu wa...

Habari za Siasa

Bajeti ya Ikulu 2024/25 kuongezeka, bunge laombwa kurudhia Sh. 1.1 trilioni

Spread the love  WIZARA ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa...

error: Content is protected !!