April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Komu atangaza kung’atuka Chadema

Mbunge wa Moshi Vijijini Anthony Komu

Spread the love
MBUNGE wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu, ametangaza “kukihama” chama chake cha sasa; na kuelekea NCCR- Mageuzi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Jumapili, Komu amesema, ameamua kuchukua uamuzi huo, kufutia kushindwa kuelewana na wenzake ndani ya Chadema.

Hata hivyo, Komu amesema, hataondoka ndani ya Chadema sasa, bali atafanya hivyo baada ya kumaliza muda wake wa ubunge, Julai mwaka huu.

“Nimeamua kuutangazia umma, kuwa nitaondoka Chadema mara baada ya kumaliza kipidi changu cha ubunge,”ameeleza Komu na kuongeza: “Nimeamua kulisema hili mapema, ili kukiwezesha Chadema, kutafuta mgombea mwingine kwenye jimbo hilo.”

Kwa taarifa kamili ya kile alichokieleza Komu, soma taarifa yake hii ambayo ameitoa kwa waandishi wa habari. Fuatilia…

Ndugu Wanahabari;

Kwanza,nichukue nafasi hii, kuwashukuru sana kwa kuitikia wito wangu wa kuja kunisikiliza katika mkutano huu muhimu.Niwapongeze pia kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kutafuta habari na kutoa habari, jambo linalotuuganisha na watu wengine ulimwenguni na kutufanya tuchukue hatua stahiki zinazoendana na wenzetu.

 Ndugu Wanahabari;

Leo ninavyozungumza nanyi, dunia nzima inakabiliwa na changamoto kubwa ya ugonjwa hatari wa COVID 19; na nanyi mmekuwa mstari wa mbele kutufahamisha juu ya janga hili na kusaidia kufikisha maelekezo ya viongozi na elimu ya kujikinga kwa jamii yetu.

Mimi kama mwakilishi wa wananchi niwaombe muendelee kuifanya kazi hiyo takatifu, tena kwa nguvu zaidi. Ugonjwa huu ni mtihani mkubwa kwetu na ili ufaulu mtihani wowote ule, huna budi kufuata maelekezo kwa umakini mkubwa na kujiandaa vema kabla ya siku ya mtihani wenyewe.

Kupitia kwenu, niwaombe wananchi wenzangu tufuate maelekezo mbalimbali yanayotolewa kwa makini na bila kuchoka na bila kuzembea na serikali iendelee kujiandaa vizuri ili ikitokea tatizo hili limekuwa kubwa zaidi, uwezo wetu uwe mzuri zaidi kuliko ilivyokuwa jana na juzi.

Aidha, tufuate ushauri wa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Dr Tedros Adhanom, kuwa tufanye mashambulizi dhidi ya gonjwa hili tusilisubiri.

 Ndugu Wanahabari;

Pili,nimeomba kukutana nanyi ili kuweka bayana mwelekeo wangu kisiasa. Hii ni kwa sababu, kwa muda mrefu kumekuwepo na mijadala juu ya mwelekeo wangu wa baadaye wa kisiasa. Wapo waliosema bila kigugumizi kuwa nina mpango wa “Kuunga Mkono Juhudi” yaani kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wengine wakadai na bado wanaendelea kudai, kwamba nina mpango wa kujiunga na chama cha ACT – Wazalendo, kwa kuwa huko nimeahidiwa cheo kikubwa. Kana kwamba hiyo haitoshi, nimeitwa majina kadhaa, yakiwamo msaliti, muasi, mwoga na mroho wa madaraka.

Kiini cha yote haya ni kwa kuwa tu natofautiana na wenzangu katika uendeshaji wa chama chetu – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) – jinsi ya kukiongoza chama chetu kimuundo, namna ya kupangana katika nafasi mbalimbali ndani ya chama na vipaumbele vyetu katika azma yetu ya kushika dola.

Kwa muda mrefu nimenyamaza ili wanaofahamu ukweli wanisemee, bahati mbaya waliojaribu kunisemea nao walituhumiwa, vita ya maneno ikawa kubwa.  La kujiuliza ni je; yote haya ni kwa faida ya nani?

 Ndugu Wanahabari;

Ni kweli kwamba nina tofautiana kwa kiasi kikubwa na viongozi wenzangu ndani ya Chadema, lakini niliamini kuwa hayo ni mambo ya kawaida sana kwa taasisi kubwa na inayokuwa kama ya kwetu. Lakini bahati mbaya sana, kuwa na mtazamo tofauti kwa kiwango kikubwa, umechukuliwa kama uasi ndani ya chama na hivyo kusababisha kutoaminika.

Jambo hilo limenifanya kushindwa kukisaidia chama chetu, hata pale ambapo ningeweza kutoa mchango mzuri na wenye tija kwa chama na taifa. Mfano mzuri wa kutokuaminika na kushindwa kupata ushirikiano hata pale baadhi yetu tunapopata fursa au uwezo wa kuchangia katika maendeleo ya chama chetu, ni matibabu ya Mheshimiwa Tundu Antipas Lisu.

Ndugu Wanahabari;

Mara tu baada ya Mheshimiwa Lisu kufikishwa Nairobi nchini Kenya baada ya jaribio la kutaka kumua, nilipata ushauri toka kwa Mtanzania anayeishi Nchini Ubelgiji kuwa tufanye kila linalowezekana tumhamishie Ubelgiji kwa kuwa zipo fursa za kuweza kupata matibabu bora zaidi na ya uhakika zaidi kutokana na maendeleo makubwa ya kiteknolojia na hata kwa gharama nafuu mara dufu.

Kwa kuwa nilimfahamu vizuri mtu huyo, nilifanya safari ya kwenda Nairobi kumshauri Mheshimiwa Freeman Mbowe, mwenyekiti wetu wa Chama juu ya fursa hiyo.  Mheshimiwa Mbowe alihoji mambo ya msingi sana ikiwa ni pamoja na uendelevu wa matibabu yenyewe, uangalizi wa mgonjwa hasa ukizingatia umbali kati ya Dar es Salaam na Ubelgiji, hadhi ya hospitali na suala zima la usalama wake.

Yote haya tuliyafanyia kazi kwa kuunda Kamati ya Watu 6 huru, akiwepo Mheshimiwa Saed Kubenea, mbunge wa Ubungo; huku wengine wote wakiwa wa nje ya chama na labda si wanachama wa Chadema.

Kwa ushirikiano wa pamoja, tukaamua kujitolea kufanikisha upatikanaji wa taarifa hizo kwa uhakika; na zote zikapatikana ikiwa ni pamoja na kwenda mpaka Ubelgiji kuona hospitali iliyokusudiwa kupelekwa Mheshimiwa Lissu na kupata uhakika wa usalama wake akiwa nchini humo.

Ndugu Wanahabari;

Baada ya kupata taarifa hizo, niliziwasilisha kwa mwenyekiti wetu, lakini bado maneno yakaendelea eti tunatumiwa na serikali kupitia mume wa huyu Mtanzania; huku baadhi ya vijana walionekana kutumwa sijui kwa maslahi ya nani, kutushambulia na kututukana kupitia mitandao ya kijamii.

Kwamba sisi tunatumika kwa ajili ya kumpeleka Lissu Ubelgiji kwa kisingizio cha matibabu bora na nafuu zaidi ili aweze kudhuriwa kirahisi. 

Ulitengenezwa uongo mkubwa sana hata wa kuhusisha raia wa nchi jirani kuwa watatumika na serikali kumuangamiza Mheshimiwa Lissu.Lakini baada ya kujiridhisha kuwa dhamira zetu ni njema, na kuombwa na kutiwa moyo na Ndugu zake wawili – Ndugu Alute kaka yake mkubwa Lissu na Vicent, mdogo wake ambaye alikuwa mmoja ya mwana-Kamati yetu ya watu Sita – tuliamua kusonga mbele.

Tuliyapuuza maneno hayo na bila msaada wowote wa Chama tulipambana ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha za kutanguliza hospitali, kama kiasi cha Euro €55,000 karibu Sh. 130 milioni, kulipia Bima ya kuanzia matibabu yake na usafiri wake pamoja na wasaidizi wake, na mahali pakufikia wakati wakimuuguza. Hakika tulifanikiwa; na ukweli iliwezekana kwa kuwa naye Mheshimiwa Lisu alichagua njia hiyo.

Ndugu Wanahabari;

Pamoja na ukweli kuwa mpaka leo Mheshimiwa Lisu yupo salama na hapajawahi kutokea tishio lolote la usalama wake na kwa zaidi ya miaka miwili aliyokaa hospitali nchini Ubelgiji akipewa matibabu ya hali ya juu, chama na wasamaria wema hawajawahi kudaiwa hata shilingi moja, tofauti na miezi minne ambayo Mheshimiwa Lisu alitibiwa Nairobi ambapo walilipa zaidi ya Sh. 700 milioni.

Hata hivyo, pamoja na jitihada zote hizo na ukweli kuwa mpango huo, umekiondolea Chama mzigo mkubwa sana wa gharama, bado wapo baadhi ya viongozi wakubwa wanaoendelea kuniandama mimi binafsi na Mh. Kubenea, kwamba tulitumia shambulio alilofanyiwa Mheshimiwa Lisu kujitafutia umaarufu kisiasa na kumuhujumu Mwenyekiti wetu.

Haya yote yanavyoendelea yanafahamika kwa mapana ndani ya chama, lakini hakuna hatua zozote za makusudi zilizochukuliwa na uongozi wa chama, kusahihisha au kufafanua jambo hili, ili mbegu ya chuki iliyopandwa dhidi yetu na ambayo imezalisha majina kama usaliti isiendelee kushamiri.

Hali hii ya viongozi wangu kunyamazia tuhuma za aina hii, imenihuzunisha na kunikwaza sana.

Ndugu Wanahabari;

Bahati mbaya zaidi, jitihada za kutaka kuondokana na hali hii, ili tubaki tukiwa wamoja tunapoelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, zinaonekana zimeshindikana.

Kwa mtazamo wangu, pamoja na kwamba ni ukweli kuwa mpinzani ni sawa na kuwa na vita dhidi ya watawala, na silaha moja muhimu, ni kuwa wamoja na kuaminiana, kwa sasa, nikiri dhana nzima ya kupendana na kuaminiana imeondoka na badala yake tunatuhumiana, kubaguana na kujengeana uadui dhidi yetu wenyewe.

Hali hii imeongezeka zaidi baada ya uchaguzi wa ndani ya chama ambao umekiacha chama na majeraha makubwa yanayohitaji tiba; bila hivyo madhara yake ni mabaya.

Aidha, malumbano haya yametuondoa kabisa katika agenda zetu za msingi kama vile, ushirikiano wa vyama na madai ya Katiba Mpya ambayo yaliwaunganisha wapinzani wote na makundi mengine muhimu, hadi kuzaliwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Kiongozi mmoja wa dini aliniuliza; mbona ninyi mnajipendelea? Mmeamua kudai Tume Huru ya Uchaguzi kwa kuwa inawahusu? Nikajitetea sana mpaka nikatumia maneno ya Kwame Nkurumah, kwamba tupate kwanza uhuru wa kisiasa, mengine yatafuata.

Ujumbe hapa ni kwamba, kiongozi huyu wa Dini anatuambia, tumeacha agenda za umma. Tumeacha kuwaratibu au tumeshindwa kuratibu matatizo yao.  Kwamba, tumeanza kusahau vipaumbele vya watu wetu kama walivyo watawala.

Kwamba, Wanahabari wanataka kuona agenda zao zikiendelezwa, mfano sheria ya Magazeti, Makosa ya Mtandaoni, na mengineyo na kwamba kila mmoja angependa eneo lake lipewe uzito wa kwanza.

Wapo wanaoona marekebisho ya kwanza yanayotakiwa kufanywa ni kwenye sheria ya utakatishaji wa fedha na uhujumu uchumi. Wengine wanataka kuangaliwa kwa Muundo wa Muungano na kero zake; na wengine wanataka kuwapo kwa madai ya Mahakama ya Kadhi na wengine kupunguzwa kwa mamlaka ya Rais.

Ndugu Wanahabari;

Kwa maoni yangu malumbano yetu wenyewe yanayoendelea ndani kwa ndani, yametuondoa kwenye wajibu wetu huo muhimu – kama chama kikuu cha upinzani nchini – wa kuwaunganisha Watanzania katika kudai mazingira bora zaidi kwenye kila nyanja.

Wanaokingoza chama chetu wameona kuwa hili siyo tatizo na hakuna sababu yoyote ya kulishughulikia. Kwa kifupi, wamelidharau.

 Ndugu Wanahabari;

Tatu, kuhusu madai kuwa naweza kuwa natumiwa na Chama Cha Mapinduzi, naomba nieleze kwa kifupi historia yangu katika kujenga Mageuzi ndani ya nchi yetu; siyo tu kuwa sijawahi kutumika na CCM, bali pia sijawahi kuwa mwanachama wake.

Nilikata shauri la kupinga mfumo wa chama kimoja nikiwa jeshini kwa mujibu wa sheria baada ya kuhoji mipango ya chama hicho nikaadhibiwa vikali kwa madai nilikuwa nachochea uasi.

Ndugu Wanahabari;

Mwaka 1988 nilikuwa mmoja wa viongozi wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, niliongoza harakati za kuiondosha CCM katika kuhodhi vyama vya wanafunzi kupitia UV-CCCM na kuwezeshwa kuanzishwa vyama huru vya wanafunzi kama DARUSO.

Katika harakati hizo ndipo nilipata bahati ya kufahamiana na watu waliokuwa na kiu ya uwepo wa mfumo wa vyama vingi, tukaunganisha nguvu tukaanzisha kitu kilichoitwa, “Multi Party Steering Committee” tukiwa na jumla ya watu 11 tu.

Kamati hii ndio ilikuja kuzaa baadaye Kamati ya Marekebisho ya Katiba kwa Kiingereza “The National Committee for Constitutional Reforms” (NCCR) iliyokuwa Tanzania Bara na KAMAHURU kwa upande wa Zanzibar.

Ndugu Wanahabari;

 Tukio hili lilitokea katika Mkutano wa Wananchi kutoka nchi nzima ambao uliofanyika kwa siku mbili – tarehe 11na 12 Juni 1991 jijini Dar es Salaam, ambapo nami nilikuwa mtoa mada.

Moja ya maazimio katika mkutano huo, lilikuwa kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wakati huo, ndani ya mwaka mmoja, kurekebisha sheria na kuhalalisha mfumo wa vyama vingi nchini, vinginevyo wananchi wangeanzisha vyama vyao vya siasa.

Hili likawezekana tukaanzisha NCCR- Mageuzi (National Convention for Construction and Reforms – Mageuzi); nami nikapewa kadi Na. 7. Nilitumikia NCCR – Mageuzi katika nafasi mbalimbali ngazi ya taifa, ikiwamo Mkurugenzi Mtendaji, mpaka mwaka 2003, nilipojiunga na Chadema.

Ndugu Wanahabari;

Ndani ya Chadema, nilianza kwa kupewa nafasi ya afisa fedha kwa muda mfupi na baadaye kuwa Mkurugenzi wa Fedha na utawala, nafasi niliyoitumikia kwa miaka 14 mfulilizo.

Kwa kupitia nafasi hiyo, niliweza kuwa Katibu wa Baraza la Wadhamini, na niliweza kuingia vikao vyote vya kitaifa. Nimefanya kazi hiyo kwa weledi na uaminifu mkubwa.

Nimeondoka katika nafasi hiyo mwaka 2016, kwa moyo mkunjufu na baada ya marekebisho ya taratibu za uendeshaji zilizowaondoa wabunge katika nafasi za utendaji.

Leo naweza kujivunia mafanikio makubwa ya Chadema kama mmoja niliyechangia katika uongozi ambao mimi nilikuwa sehemu yake.

Chama kilipata mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na ukuaji wa ruzuku kutoka Sh. milioni 5 kwa mwezi, mwaka 2000 hadi zaidi ya Sh. Milioni 300 mwaka 2015. Kwa upande wa Wabunge wa majimbo, tulitoka wabunge 4 hadi 35.

Wabunge wa Viti Maalum, kutoka mmoja  aliyekuwapo mwaka 2000 hadi 36; na kwa upande wa Halmashauri, tumeweza kuongeza Halmashauri 23 kutoka 3 zilizokuwapo.

Ndani ya kipindi changu tuliweza kuanzisha miongozo mizuri ya Usimamizi wa Fedha na Rasilimali, tulibuni mbinu mbalimbali za kupata rasilimali na kuzitumia vema kwa maendeleo ya Chama na ndio maana haikuwa rahisi kupata hati chafu toka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kama ukifuata miongozo hiyo, lakini sisi ndio pia tuliodai CAG kukagua vyama vya Siasa.

Aidha, nilisimamia kikamilifu kutengeneza Kanunni sahihi iliyotafsiri michango ya kikatiba ya wabunge wa Chadema na mimi nikawa mmoja wa wabunge waliochanga michango hiyo kila mwezi kwa mujibu wa maelekezo ya chama.

Lengo ni kuwa fedha hizo ambazo zilikadiriwa kuwa zingefikia Sh. 4.2 bilioni hadi kumalizika kwa muda wa Bunge hili, zingetumika kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

Tulibuni chanzo hicho cha uhakika cha mapato kutokana na uzoefu katika chaguzi zilizopita ambapo mipango ya kitaasisi inakuwa migumu kutokana na kutokuwa na fedha kwa wakati.

Aidha, uchaguzi mkuu wowote mahitaji ya fedha ni muhimu sana katika kulinda ushindi. Ni Bahati mbaya kusikia minong’ono kwamba fedha hizo nazo zilishatumika kwa malengo mengine.  Niliondoka Chadema nikiwa nimeacha akaunti yake ikiwa na akiba ya Sh. 992 milioni.

Mbali na hayo nimeshiriki kuanzisha na kujenga taasisi zinazopigania Demokrasia, utawala wa sheria na haki za Binadamu kama Tanzania Center for Democracy (TCD).

Ndugu Wanahabari;

Nimeeleza yote hayo siyo kwa sababu nataka kutumia wasifu wangu kama kinga ya kutokosolewa au kuwajibishwa panapostahili, lahasha. Bali, nimekumbuka ule msemo usemao: “Asiyekujua hakuchagulii Tusi.”

Ndugu Wanahabari;

Nne, baada ya kueleza hayo yote, sasa napenda kumaliza hotuba yangu kwa kueleza yafuatayo:

Kwa kuwa sijaamua kustaafu siasa, na kwa kuwa ninajiona bado naweza kutumika;

Na kwa kuwa bado ninaamini sababu zilizonifanya nijiunge na wanaharakati ambao walianzisha vuguvugu la kudai mfumo wa vyama vingi nchini, bado zipo na zina mashiko zaidi sasa kuliko wakati ule;

Na kwa kuwa hata vitabu vitakatifu vinafundisha kuwa na msimamo thabiti kwenye kila jambo (Ufunuo 3: 15 -16)…na kwa kuwa unafiki siyo jambo zuri;

Basi ninaweka bayana hapa kuwa nitaondoka CHADEMA mara nitakapomaliza kipindi changu cha ubunge kwa kuwa ninao wajibu wa kisheria na kikatiba wa kutumikia wananchi wa Moshi Vijijini, mpaka uchaguzi mkuu ujao utakapoitishwa;

Na kwa sababu hiyo, ifahamike pia kuwa sitagombea ubunge kupitia CHADEMA na ikiwa nitatakiwa kugombea nafasi yoyote nitafanya hivyo kupitia Chama cha NCCR -Mageuzi katika Jimbo ambalo chama hicho kitaamua.

 Ndugu Wanahabari;

Msimamo huu nimeutoa mapema kwa manufaa mapana ya upinzani. Moja, itaondoa majungu yanayoendelea kwa kisingizio changu labda eti nataka nihakishiwe kuteuliwa kugombea tena ubunge; na au eti nataka kurudi katika nafasi ya ukurugenzi wa fedha; na eti nataka kumpindua Mwenyekiti wetu n.k.

Aidha, vyama vinavyotuhumiwa kunitumia kuvuruga Chadema navyo vitakuwa na amani na waliojipa hiyo kazi ya kuzusha watakuwa hawana namna nyingine, na hivyo labda watakwenda kufanya kazi zenye manufaa.

Ndugu wanahabari; 

 Nimeamua kufanya maamuzi haya ili kukipa chama changu cha sasa hususani katika Jimbo la Moshi Vijijini fursa ya kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa Oktoba mwaka huu wakijua bayana kuwa mimi sitakuwepo.

Huu ni utamaduni mzuri na ambao ni vema ukaigwa na wengine ambao wanayo mipango yao mfukoni tofauti na ile ya vyama vyao.

Mimi nimeiga utaratibu huu kwa wenzetu wa Kenya ambapo Naibu Rais, Mheshimiwa William Rutto, ameshasema bayaa kuwa uchaguzi ujao wa 2022 atagombea, lakini siyo kwa chama chake cha sasa.

Hivyo ni imani yangu kuwa chama changu cha sasa – Chadema – kitalichukulia suala hili kwa mtazamo chanya na kwa kuzingatia misingi tuliyojijengea wenyewe katika Katiba yetu na sera zetu.

Ndugu Wanahabari;

Katiba ya Chadema, Toleo la mwaka 2016, Sura ya Nne, Kifungu 4.0(4.1.4) uk. 8 – 9, imeeleza vizuri dhana ya uamuzi wangu huu kwa maneno   yafuatayo:

“Kuhakikisha mtu ana uhuru wa kwenda mahali popote ndani ya mipaka ya Nchi na kwamba anaweza kushirikiana na mtu yoyote ndani na nje ya nchi katika kuendeleza maslahi halali ya washirika na kuwa kuna uhuru wa kukutana…”.

Aidha, sera za Chadema zinasisitiza katika kifungu cha 1.2 kwa maneno haya: “…Chadema itakikisha  kwamba kila mwananchi anakuwa na uhuru kamili wa kueleza fikra zake, kupata na kutoa habari, kukusanyika na kujiunga na kikundi au chama chochote kwa hiari na  utashi wake.”

 Ndugu wanahabari;

Uamuzi wangu huu si wa kukurupuka wala wa kibabe. Nimewashirikisha watu wengi kiasi, ninaoamini wana mapenzi mema na nchi yetu na baadhi yao kwa namna moja au nyingine, wamechangia katika mafanikio niliyoyapata katika harakati zangu za kisiasa.

Hawa wanatoka kwenye familia yangu, Taasisi za dini, Asasi zisizo za kiserikali, wanasiasa na wanaharakati huru wa ndani na nje. Wengi wamenipa baraka zao.

Ninamwomba kila mmoja atakayeguswa kwa namna yoyote na uamuzi huu, aungane na walionipa baraka za kwenda mbele kwa kuwa tunajenga nyumba moja na hivyo, kwa nini tunyang’anyane fito?

Kwa misingi hii, ninaamini kuwa chama changu cha sasa, kitaheshimu uamuzi wangu huu bila mizengwe. Mimi sikuingizwa kwenye siasa na mtu wala sikufuata mtu; na au sikikusumwa na maslahi binafsi, bali maslahi mapana ya kitaifa.

Hivyo basi, uamuzi huu unaendelea kuzingatia misingi hiyo hiyo.

Ndugu wanahabari,

Mnaweza kujiuliza: Kwa nini nimeamua kurejea NCCR- Mageuzi? Sababu ni hizi zifuatazo:

Mosi, ni itikadi yake ya UTU. Kwa maoni yangu tumeacha kuheshimiana. Itikadi ya UTU inatukumbusha kuwa sisi sote ni sawa na kila mmoja anastahili kutendewa sawa na mwingine.

Mbili, ni utulivu na ukomavu uliopo sasa hivi ndani ya chama hicho, hasa baada ya kupitia matatizo makubwa.

Kihistoria baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 ambapo NCCR- Mageuzi, kiliibuka chama kikuu cha Upinzani nchini kikiwa na wabunge 16 wa kuchaguliwa na wabunge 3 wa Viti Maalumu, na kupata madiwani wengi kuliko chama chochote cha upinzani, kilikumbwa na mgogoro wa mkubwa wa kiuongozi.

Mgogoro huu kati ya Kamati Kuu (CC) na aliyekuwa mwenyekiti wake, Augustine Mrema, ulisababisha kupoteza wabunge wake wote katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na badala yake tukapata mbunge mpya mmoja tu – Kifu Gulam Hussen Kifu aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini – ambaye naye hadumu baada ya kuondolewa na Mahakama.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, NCCR- Mageuzi, hawakupata hata mbunge mmoja. Wakaendelea kujipanga, mwaka 2010 wakapata jumla ya wabunge wanne.

Pamoja na ushiriki wao kwenye UKAWA katika uchaguzi wa mwaka 2015, wakapata mbunge mmoja tu. Historia hii inaifanya NCCR – Mageuzi, kuwa na uzoefu wa kipekee na ndio maana inao utulivu wa ndani wa kutosha kulinganisha na vyama vingine.

Kwa maoni yangu, hali hii ikitumiwa vizuri, itakuwa ni fursa ambayo inaweza kutumika kurejesha agenda ambazo zilikuwa ndio sababu ya Watanzania kuunga mkono Upinzani.

Ndugu wanahabari;

Sababu ya tatu, ni kauli iliyotolewa na uongozi wa juu wa NCCR- Mageuzi kupitia mwenyekiti wake Ndugu James Francis Mbatia, kwamba

anaomba msamaha wote waliokwazwa na chama hicho na kuamua kuondoka katika chama chao na kujiunga na vyama vingine au kuacha siasa.

Alitoa rai kuwa warejee katika chama chao kwenda kuendeleza harakati za kujenga mfumo thabiti na endelevu wa vyama vingi katika azma yake ya kutwa Dola na kufanya marekebisho mengi na kujenga upya nchi yetu.

Mimi binafsi kauli hii ilinigusa na kuiona ni ya kiungwana na yenye upevu wa juu sana. Hakika, imenivuta na kunishawishi.  Naona kuwa wamejifunza na kutambua kuwa tunahitajiana, hata katika tofauti zetu.

Ndugu wanahabari;

 Nami niungane naye kuwaomba radhi sana tena sana wote ambao mienendo yangu katika harakati hizi nimewahi kuwakwaza. Mimi nilikuwa NCCR- Mageuzi. Nikaondoka nikajiunga CHADEMA na nikafuatwa na watu wengi na kabla ya kujiunga nilikuwa mstari wa mbele kutaka NCCR – Mageuzi kuungana na Chadema kizaliwe chama kipya ambacho kingeitwa Umoja wa Demokrasia Tanzania (UDETA).

Niliombe radhi sana kundi hilo liloongozwa na Ndugu Prince Mahinja Bagenda, nikianza na yeye mwenyewe.  Niwaombe kwa moyo wa dhati wale waliobaki NCCR- Mageuzi wakati ukifika, wanipokee tena nyumbani.

Nawashukuruni sana. Asanteni sana kwa kunisikiliza

 Naomba Mungu aendelee kutuimarisha. Mungu Ibariki Tanzania.

 Anthony Bahati Komu,

Mbunge wa Moshi Vijiji (Chadema),

29 Machi 2020,

Dar es Salaam.

error: Content is protected !!