Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Komandoo wa JWTZ aeleza alivyohojiwa kuhusu Mbowe
Habari za Siasa

Komandoo wa JWTZ aeleza alivyohojiwa kuhusu Mbowe

Spread the love

 

ALIYEKUWA Komandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Gabriel Samheta Mhina, akitoa ushahidi wake katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, amedai kuwa alihojiwa na Askari Polisi, waliomkamata mkoani Tabora, kama anamfahamu Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Mhina ametoa madai hayo leo Jumatano, tarehe 1 Desemba 2021, mahakamani hapo.mbele ya Jaji Joachim Tiganga, akitoa ushahidi wake katika kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mohammed Ling’wenya, yasipokelewe katika kesi ya msingi.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika keso hiyo ni Ling’wenya, Adam Kasekwa na Halfan Hassan Bwire, ambao wote walikuwa makomandoo wa JWTZ, kikosi cha 92 Sangasanga

Yafuatayo ni mahojiano kati ya Mhina na Wakili Dickson Matata.

Matata: Unakumbuka nini kuhusu tarehe 19 Septemba 2020?

Shahidi: Septemba 19 2020 nikiwa maeneo ya nyumbani kuna rafiki yangu anaitwa Dida alinisihi kuna sehemu kuna Pub tukaangalie mpira.

Matata: Nyumbani wapi?

Shahidi: Mkoani Tabora

Matata: Pub gani?

Shahidi: Inaitwa Oxigen pub. Nilipojaribu kufika katika lile eneo ghafla nilikamatwa na Task Force Polisi

Matata: Walikuwa wangapi?

Shahidi: Niliowakuta pub walikuwa wawili lakini niligundua hawakuwa wawili wengine walijificha sehemu wakiona hatua gani ningechukua baada ya kukamatwa na wale askari

Matata: Kabla ya kukukamata walifanya nini?

Shahidi: Waliniuliza kwa kuwa na wewe ni Taski Force unajua kuna jukumu gani hapa mkoani

Matata: Kabla ya kukukamata walifanya nini kwanza?

Shahidi: Kuna afande alitoa pisto akaniambia nahitajika kwa RCO kwa kuwa nilijua naenda sehemu salama ilinilazimu kupanda gari kuelekea Kituo cha Polisi cha Mkoa

Matata: Ilikuwa gari gani?

Shahidi:Toyota land cruiser

Matata: Ndani ya gari mlikuwa wangapi?

Shahidi: Nilikutana na dereva mmoja na askari wawili jumla tulikuwa wanne, wao watatu na mimi wa nne.

Matata: Ulikaa sehemu gani ndani ya hilo gari?

Shahidi:Mimi nilikaa mbele kabisa wao walikaa nyuma

Matata: Hapo mbele ulikuwa na nani?

Shahidi:Nilikuwa na dereva

Matata: Umesema wakati unakamatwa mlikamatwa na wawili, wengine uligundua walijificha au wao ilikuwaje?

Shahidi: Niligundua baada ya kufika kituo cha mkoa nyuma kulikuwa na msururu wa magari unatufuata nyuma yetu, ambao magari wenyewe walikuwepo kwenye magari yanayotufuata.

Matata: Mlipofika pale Central Polisi Tabora mlifikia wapi?

Shahidi: Kitu cha kwanza wakati wanafikiria kuniunganisha na RCO walinifunga pingu wakanipeleka ndani ya kituo cha polisi kwa nyuma kabisa

Matata: Nikurudishe nyuma kidogo wakati unakamatwa ulisema askari aliyekutolea pisto kuna maneno alikwambia, maneno gani?

Shahidi: Alinitolea vitisho vya kutaka kuniua akaniambia nitakumaliza ukikataa kwenda kituo cha polisi, ikabidi nitii amri nikiamini ninakokwenda salama

Matata: Akakwambia maneno gani mengine?

Shahidi: Baada ya kutokea ubishi kati yao na mimi wakasema unajua mkoani kesho yake kuna nini? Hiyo kesho yake ilikuwa kwa ajili ya ujio wa rais kwa ajili ya kampeni

Matata: Umesema rais unamaanisha na kwenye kampeni alikuwa anagombea kupitia chama gani?

Shahidi: Alikuwa hayati Magufuli kipindi hicho alikuwa anakuja mkoani kwa ajili ya kampeni

Matata: Kitu gani kingine walikuambia?

Shahidi: Nilipofika kituoni niliambiwa kwamba nina uhusiano na Mbowe huku wakinipiga vibaya mno wakiniambia nikiri uhusiano wangu na Mbowe.

Matata:Tabora maeneo gani mahsusi walikuwa wanakupiga?

Shahidi: Ukiingia kituoni kuna meza nilipelekwa nyuma kabisa kwenda kule kufanya mahojiano na mimi haikuwa ofisini ilikuwa nyuma ya kituo cha polisi lakini bado tunakuwepo katika mazingira yaleyale ya kituoni.

Matata: Ulikuwa unapigwa wapi?

Shahidi: Walikuwa wananipiga na fimbo pia nilikuwa napigwa ngumi za taya

Matata: Walikuwa askari wangapi?

Shahidi: Walionipiga siwakumbuki ila namkumbuka Goodluck Minja, Jumanne Mahita halafu na Aziz.

Matata: Hilo zoezi la kukupiga lilichukua muda gani?

Shahidi: Almost masaa matatu baada ya kuona nilikataa kutomfahamu walienda kunilaza kituo cha polisi cha reli sababu tayari hali yangu haikuwa nzuri

Matata: Ulienda na kina nani?

Shahidi: Nilienda nao wote waliokuwa wananisulubu baada ya hali yangu kuwa sio nzuri waliniacha pale wakarudi tarehe 20 Septemba 2020.

Walivyokuja asubuhi baada ya kuona nakataa kumfahamu Mbowe, waliniuliza unamfahamu Ling’wenya na una uhusiano nae gani?

Matata: Ukajibu vipi?

Shahidi: Nilikiri kumfahamu sababu niliwahi fanya naye kazi na hata alipotoka kazini aliendelea kuwa rafiki yangu wa karibu.

Matata: Walikuambia nini shahidi?

Shahidi: Waliniambia unajua sasa hivi Ling’wenya yuko wapi, lakini kipindi kile nilikuwa sifahamu mahali ambapo Ling’wenya yupo.

Matata: Kikaendelea nini baada ya kuwajibu hujui walipo?

Shahidi: Wakaniambia baada ya kuona siwapi ushirikiano wowote tarehe 20 Septemba tukaelekea Nzega .

Matata: Mkaondoka saa ngapi?

Shahidi: Asubuhi walinifunga kitambaa kutokana na hali niliyokuwa nayo nilikuwa tofauti na mahabusu wengine sababu muda wote nilikuwa nimefungwa pingu. Baada ya kuwa nimefika Nzega nilijaribu kuwauliza wale niliokutana nao ambao walikuwa mahabusu sababu nilichanganywa na mahabusu wengine.

Matata: Mlifikishwa kituo gani?

Shahidi: Kituo cha Polisi pale Nzega.

Matata: Baada ya kuuliza nini kiliendelea?

Shahidi: Baada ya pale waliniacha na mahabusu wao wakaondoka sikufahamu walikwenda wapi.

Matata: Huyo mtu Malema alikuwa nani?

Shahidi: Aliwahi kuwa komandoo siku za nyuma, nilijua mazingira aliyokuja nayo yalikuwa kama ya kwangu alikuwa anasumbua Polisi, alipoulizwa yeye ni nani na anatoka wapi ndipo alipojitambulisha yeye alikuwa komandoo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

Habari za Siasa

CCM yakemea ufisadi, yaipa kibarua TAKUKURU

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekemea vitendo vya ubadhirifu wa...

Habari za Siasa

Bajeti ya Ikulu 2024/25 kuongezeka, bunge laombwa kurudhia Sh. 1.1 trilioni

Spread the love  WIZARA ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa...

error: Content is protected !!