WAKATI joto la mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/21 kati ya watani wa jadi, Simba dhidi ya Yanga likipamba moto, Kocha Mkuu wa Yanga, Nadreddine Al Nabi amewaita mashabiki wa mpira, kuja kushuhudia mtanange huo. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Nabi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, tarehe 7 Mei, 2021, ikiwa ni siku moja imesalia kabla ya mchezo huo kupigwa kesho Jumamosi, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Hii itakuwa ni ‘Derby’ ya kwanza kwa Nabi tangu alipoanza kuwafundisha mabingwa hao wa kihistoria Tanzania.
Katika mkutano huo na waandishi, Nabi alikuwa akitumia lugha ya Kifaransa na Nahodha wa timu hiyo, Haruna Niyonzima, alikuwa akitafasiri kwa Kiswahili.
“Naheshimu kila timu na mchezo wa Simba sio mwisho wa dunia, kila mechi naanda timu ila naangalia wapi kwa kurekebisha, ila ninatazama kiufundi na sio kama shabiki,” amesema.
Nabi amesema; “mchezo wa kesho nimejiandaa vizuri, najua haitakuwa mechi rahisi kwake lakini nimekiandaa kikosi changu vizuri, nawakaribisha mashabiki wa soka kuja kuangalia mchezo ambao utakuwa mzuri.”
Akiichambua Simba ambayo akiifundisha timu ya El Merreikh ya Sudan, walikutana kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika na kutoka suluhu, Nabi amesema; “ni kweli nimeshawahi kukutana na Simba na nawapongeza kwa kiwango walichokionesha kwenye michuano ya Afrika, ila kwenye mpira, kila timu inauzuri wake na ubaya wake, ninawaheshimu ila siwahofii.”
Kocha huyo amesema, anatarajia kufanya mabadiliko kwenye kikosi hicho na “sio tatizo kwa sababu, nataka kusaidia timu na mtarajie kesho mabadiliko yatafanyika ili kufanya mchezo uwe mzuri.”
Alipoulizwa kama kuna wachezaji majeruhi, amesema “kawaida yangu sio lazima kutaja wachezaji watakaokosekana kesho au kutokuwepo kwa sababu, kuna nafasi leo ya mazoezi ya mwisho, mengine mtayaona kesho.”
“Tarajieni kesho kuona mabadiliko kutoka kwenye kikosi kilichoanza kwenye mchezo uliopita,” amesema Nabi.

Kwa upande wake, Niyonzima amesema “nimecheza hizi mechi nikiwa pande zote mbili na utakuwa mchezo mzuri. Mechi kubwa hucheza na wachezaji wakubwa na timu itakayojiandaa vizuri itaibuka na ushindi,”
Alipoulizwa kama atacheza, Niyonzima amesema “mimi naijiandaa ili nicheze, ila maamuzi yote yapo kwa mwalimu, kama nikipata nafasi nitacheza nisaidie timu yangu kwa sababu nimezoea kucheza hizi mechi.”
Niyonzima amesewataka mashabiki wa Yanga waje kwa wingi uwanjani kwani wamejiandaa vizuri na wao kama wachezaji hawana presha na hawezi kusema wamejiandaaje na hii mechi lakini wao wanaihitaji zaidi.
“Ni mechi kubwa na tunaiheshimu na tutafuata masharti ya Mwalimu aliyotuambia kila mchezaji anatamani kukutana na mechi ya kesho na wenzangu ninawaamini,” amesema Niyonzima.
Leave a comment