November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kocha wa Samatta atimliwa Aston Villa

Spread the love

 

TIMU ya Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza, imemfukuza kazi kocha wake mkuu, Dean Smith. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Smith (50) aliyejiunga na Villa Oktoba 2018, amefukuzwa leo Jumapili, tarehe 7 Novemba 2021, baada ya mwenedo wa timu hiyo katika ligi kuwa mbaya.

Kati ya michezo 11 iliyocheza, imejikusanyia pointi 10 pekee ikiwa nafasi ya 15 kati ya timu 20 zinazoshiriki ligi hiyo.

“Msimu huu, hatujaona mabadiliko ya timu, matokeo mazuri na nafasi tulipo kwenye ligi si mzuri. Kutokana na sababu hizo, tumeamua kufanya mabadiliko ili aje kocha mpya,” amesema Christian Purslow, Ofisa wa timu hiyo

Smith, atakumbukwa na Watanzania wengi, baada ya kuwezesha Mtanzania wa kwanza, Mbwana Samatta kucheza Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Samatta ambaye ni nahodha wa kikosi cha soka cha Tanzania ‘Taifa Stars’ anayecheza nafasi ya ushambuliaji, alisajiliwa na Aston Villa, Januari 2020 akitokea KRC Genk ya nchini Ubelgiji.

Kabla ya kutua Villa Park, Samatta alicheza kwa misimu minne KRC kuanzia mwaka 2016-2020 akitokea TP Mazembe ya Congo.

Hata hivyo, Samatta hakuwa na wakati mzuri ndani ya kikosi hicho cha Smith na Septemba 2020, alipelekwa kwa mkopo Fenerbahce ya Uturuki.

Septemba 2021, Samatta alirejea kwa mara nyingine Ubelgiji na safari hii akijiunga kwa mkopo na Royal Antwerp inayoshiriki ligi kuu nchini humo.

error: Content is protected !!